Thursday, 31 July 2014

Maporomoko yafunika kijiji huko India


maporomoko India
Zaidi ya watu 200 wanahofiwa kukwama katika maporomoko ya udongo nchini India,huku 20 wakithibitishwa kufariki dunia katika kijiji cha kijiji cha Malin karibu na mji wa Pune lilikotokea janga hilo.
Kazi ya uokoaji inaendelea katika eneo hilo huku hali ya hewa mbaya ikidaiwa kuchelewesha harakati hizo.
Vikosi vya uokoaji vimeendelea na kazi ya kuwanusuru waliofukiwa na maporomoko ya udogo huo, japo kuwa mazingira magumu na hali mbaya ya hewa vinakwamisha shughuli hiyo.Maporomoko hayo yaliyokikumba kijiji cha Malin India karibu na jimbo la Maharashtra yamesababisha nyumba nyingi kusombwa huku watu wakihofiwa kunaswa pia katika eneo hilo.
Mwandishi wa BBC Devidas Desh pande aliyepo katika eneo la tukio anasema jingo pekee linaloonekana kunusurika na janga hilo ni ya shule pekee, huku maeneo mengine yakiwa tambarale kabisa.
Narendra Modi ni waziri mkuu wa India na hapa anaelezea hatua wanazozichukua.
Maporomoko ya ardhi ni jambo la kawaida kutokea nchini India hasa kipindi cha mvua zitokanazo na pepo za Monsoon ambazo hunyesha kuanzia mwezi june hadi septemba kila mwaka.

Vijidudu hatari vya malaria vyagundulika


Mbu wa Malaria
Watafiti wametoa tahadhari kuwa vijidudu vya malaria visivyoweza kuuawa kwa dawa vimetapakaa katika maeneo ya mpakani kusini mashariki mwa Asia vikitishia mapambano dhidi ya Malaria.
Vipimo kwa wagonjwa 1000 katika maeneo ya Cambodia, Burma, Thailand na Vietnam vimegundua vijidudu hivyo havizuiliwi na artemisinin dawa inayoaminika katika vita dhidi ya malaria. Utafiti huo umeeleza kuwa kuyarudia
matibabu baada ya kukumbana na maambukizi inaweza kusaidia kupambana na kusambaa kwa Malaria katika Asia na baadae Afrika ndani ya muda mfupi. Mamia ya maelfu ya watu hufariki kutokana na Malaria kila mwaka hasa katika Afrika.

Wednesday, 30 July 2014

Al shababu yaua mwanamama kwa kutojifunga Niqab

Wanamgambo wa kiislamu wa Al Shabab wamempiga mwanamke mmoja risasi na kumuua kwa kukosa kujifunga niqab kichwani.
Jamaa za mwanamke huyo mwenyeji wa mji wa Hosingow kusini mwa Somalia wanasema mwanamke huyo alikataa kujifunika kitambaa kichwani kuambatana na sheria za dini ya kislamu .
''alikuwa ameonywa ajisitiri lakini wapiganaji hao waliporejea wakashikwa na hasira walipopata kuwa hakuwa amejifunika na hivyo wakampiga risasi''.

Al Shabab yaua mama kwa kukosa Niqab
Jamaa zake wameiambia shirika la utangazaji la BBC kuwa Ruqiya Farah Yarow alikuwa amewafokea wapiganaji hao akiwataka waondoke kwake na kusema kuwa angejisitiri baadaye.
Kundi la Al Shabab linalomiliki asili mia kubwa ya maeneo ya Kusini na Katikati ya Somalia na limekuwa likishinikiza kutumiwa kwa sheria kali za kiislamu.
Hata hivyo msemaji wa kundi hilo amekanusha kuwa ni wao waliomuua mwanamke huyo .
Msemaji huyo anasema kuwa licha ya kudhibiti maeneo makubwa nchini humo kundi hilo bado halijatoa maelezo ya vipi wanawake wanastahili kujisitiri.

Mwanamke ajinyonga huko Tabata

Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Irene Ibrahim (22), mkazi wa Tabata Kisukuru manispaa ya Ilala, amefariki dunia baada ya kujinyonga.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema marehemu alikutwa kwenye shamba la Abdallah Mshindo akiwa amejinyonga kwa kutumia khanga aliyoitundika katika tawi la mti aina ya mjohoro.
Minangi alisema, tukio hilo lilitokea Julai 27 majira ya saa 1 usiku, ambako Irene alifika kwenye duka la Oliver Laurent akiwa amebeba pombe tatu aina ya viroba na dawa aina ya Mifupain nyingi mkononi huku akiwaeleza baadhi ya watu kuwa, atasafiri kwenda Amerika kisha kuingia chumbani kwake.
Alisema, baada ya kuingia chumbani kwake, hakuonekana tena mpaka walipoangalia chumbani kwake walikuta maganda ya viroba na dawa bila yeye kuwepo, ndipo alipokutwa akiwa amejinyonga shambani hapo.
Katika tukio jingine, mtu mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha kugonga mti.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Camillius Wambura, alisema ajali hiyo ilitokea Julai 28 majira ya saa 8 usiku eneo la Masaki Kata ya Msasani, Kinondoni barabara ya Kimweri iliyohusisha gari aina ya Toyota Rav 4 yenye namba za usajili T422 AXV iliyokuwa inaendeshwa na dereva anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 20-25.
Wambura aliongeza kuwa, gari hilo lilikuwa linatokea barabara ya Ally Hassan Mwinyi kwenda Coco Beach ndipo lilipoacha njia na kugonga mnazi uliyokuwa kandokando ya barabara  hiyo.

Tuesday, 29 July 2014

Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba (IMTU) wafunguliwa kesi ya Viungo vya binadamu

Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba cha IMTU wakiwa mahakamaniWAHADHIRI wanne wa Chuo Kikuu cha Tiba cha IMTU, Mbezi Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na makosa mawili, likiwemo la kushindwa kufukia viroba 83 vya viungo vya binadamu.
Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Polisi, Magoma Mtani, mbele ya Hakimu Kwey Rusemwa, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Venkat Subbaiah (57), Appm Shankar Rao (64), Prabhakar Rai (69) na Dinesh Kumar (27).
Magoma alidai kuwa washitakiwa hao Julai 2014 katika eneo la Mpigi Majohe, walishindwa kufukia viroba 83 vya viungo vya binadamu walivyovitumia kufundishia wanafunzi wa udaktari kinyume na kifungu cha 128 cha sheria ya kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.
Alidai kuwa washitakiwa hao kwa pamoja, pia walishindwa kuandaa hati kwa Kampuni ya Corona ya kuthibitisha kufukiwa kwa mabaki hayo.
Washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na upande wa jamhuri ukadai upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Rusema, alisema ili washitakiwa wapate dhamana, kila mmoja awe wadhamini wawili ambao ni Watanzania na wanaofanya kazi kutoka kwenye taasisi zinazotambulika kisheria.
Wakati taratibu hizo zikiendelea, Wakili wa Serikali, Salum Ahmed aliingia mahakamani hapo na kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002 kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo, Hakimu Rusemwa aliwaachia huru washitakiwa hao, lakini muda mfupi baadaye walikamatwa na askari wa Jeshi la Polisi na kuwekwa chini ya ulinzi mkali na kupandishwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili KXO 6 EFY na Toyota RV4
yenye namba za usajili T 366 AVG na kuondoshwa katika eneo la mahakama.

mwanamke jambazi sugu na wenzake watiwa mbaroni

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kukamata mtandao hatari wa majambazi kumi, mmoja akiwa ni mwanamke anayeshiriki kikamilifu wakati wa matukio ya ujambazi.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna (CP), Suleiman KovaAkizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna (CP), Suleiman Kova, alisema majambazi hao wamekamatwa katika msako mkali unaoendelea katika harakati za kuhakikisha maisha na mali za wakazi wa Dar es Salaam vinalindwa kikamilifu.
Kova alisema katika msako huo watuhumiwa walipekuliwa katika miili, makazi na maficho yao na wakakutwa na silaha tisa ambazo ni bunduki SMG namba 13975 ikiwa na risasi 11 na magazine mbili, SMG moja bila magazine na namba hazisomeki, bastola aina ya Luger yenye namba 5533K, bastola aina ya Browning yenye namba TZACR83494 S/No.7670 na risasi sita ndani ya magazine.
Alizitaja silaha nyingine kuwa ni shotgun pump action na risasi 55, Marck Iv iliyokatwa mtutu na kitako yenye magazine moja na risasi nne, bastola yenye namba A963858 Browning iliyokuwa na risasi moja, SMG ambayo iko kwa mtaalam wa uchunguzi wa silaha (Balistic), pamoja na shotgun TZ CAR 86192 ambayo ilitelekezwa baada ya msako.
Kova aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Maulidi Mbwate (23), mfanyabiashara mkazi wa Mbagala Charambe, Foibe Vicent (30), hana kazi mkazi wa Mbagala Kibondemaji, Vincent Kadogoo (30), mkazi wa Mbagala Kibondemaji, Said Mlisi (29), dereva wa bodaboda mkazi wa Gongo la Mboto na Hemed Zaga (22), dereva bodaboda mkazi wa Gongo la Mboto.
Wengine ni Mohamed Said (31), fundi kuunga vyuma mkazi wa Kigogo, Lucy Mwafongo (41), mama lishe mkazi wa Vingunguti Ukonga, Rajabu Ramadhani (22), mkazi wa Kariakoo, Deus Chilala (30), mgonga kokoto Kunduchi, mkazi wa Yombo Kilakala pamoja na Marietha Musa (18), mkazi wa Yombo Kilakala.
“Mwanamke pekee katika kundi hilo Foibe Vicent ameshiriki katika matukio ya uporaji wa kutumia silaha, mauaji na mengine mengi, yeye mwenyewe alikuwa akitumia bunduki aina ya SMG. Katika baadhi ya matukio, wananchi walioshuhudia wamekuwa wakitoa taarifa kwamba alikuwepo mwanamke aliyekuwa akifyatua risasi na hatimaye polisi walifanikiwa kumkamata akiwa na wenzake katika kundi hilo,” alisema Kova.

Chadema Yaendelea kujiweka sawa

Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi, Benson KigailaKATIKA kuhakikisha uchaguzi mkuu wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), unaendeshwa kwa uwazi na umakini ili kuepuka mitego ya kuchomekewa wasaliti, chama hicho kimejipanga upya na kuusogeza hadi Septemba 14 badala ya Agosti 31.
Hatua hiyo ni baada ya Kamati Kuu kubaini kwamba hakuna chombo cha kuusimamia uchaguzi huo, na sasa imeamua jukumu hilo lifanywe na Baraza la Wazee Taifa.
Kwa mujibu wa ratiba mpya iliyotangazwa jana na Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi, Benson Kigaila, uchaguzi wa Baraza la Wazee ndio utatangulia kufanyika Septemba 6, ili kutoa nafasi kwa chombo hicho kusimamia uchaguzi mkuu.
Kigaila alisema kuwa mkutano mkuu wa kuwachagua mwenyekiti, makamu mwenyekiti Bara na Visiwani, utatanguliwa na chaguzi za mabaraza ngazi ya kitaifa.
“Hadi kufikia Julai 30, uchaguzi wa kata utakuwa umekamilika na Agosti 15, mwaka huu, uchaguzi wa majimbo na wilaya nao unapaswa kukamilika ili kuruhusu uchaguzi ngazi ya mkoa uanze hadi Agosti 30 mwaka huu,” alisema.
Kigaila alisema uchaguzi wa Baraza la Vijana (Bavicha) utafanyika Septemba 10 huku ule wa Baraza la Wanawake (Bawacha) ukipangwa kuwa Septemba 11.
“Baada ya chaguzi hizo za mabaraza kukamilika, Kamati Kuu ya sasa itakutana Septemba 12 kwa ajili ya kuandaa kikao cha Baraza Kuu kitachaofanyika Septemba 13 mwaka huu, ili kuandaa mkutano mkuu wa Septemba 14,” alisema.
Alisema baada ya mkutano mkuu, Baraza Kuu litakaa Septemba 15 kwa ajili ya kumchagua Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Visiwani ili Kamati Kuu mpya iweze kutambulishana.
Kigaila aliwataka wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za kitaifa kuchukua fomu kuanzia Agosti 10 hadi 25 katika ofisi za majimbo, wilaya, makao makuu ya mabaraza hayo na ofisi za chama.
Alisema fomu hizo zinaweza kupatikana pia katika mitandao ya mabaraza hayo na chama, lakini alionya kwamba lazima fomu hiyo baada ya kujazwa irejeshwe katika makao makuu ya mabaraza hayo na chama ili iweze kulipiwa.
“Gharama zinazotozwa kwa mgombea wa uenyekiti, katibu, mratibu wa uenezi, mweka hazina na mwenyekiti wa kamati ya uratibu kama kwenye wilaya kuna jimbo zaidi ya moja ni sh. 10,000.
“Gharama za kugombea nafasi ya mwenyekiti, makamu wenyeviti, katibu mkuu, naibu katibu Bara na Visiwani ni sh. 50,000… mratibu wa uenezi na mweka hazina ni sh. 30,000, wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu ni sh. 25,000,” alisema Kigaila.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Antony Komu, alisema CHADEMA inatarajia kutumia sh. milioni 700 katika  uchaguzi huo, hivyo aliwataka wagombea  wote kuhakikisha wanalipia fomu baada ya kujaza.
Hata hivyo, aliwaomba wanachama na wapenzi wa chama hicho kujitolea kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo ambao alisema utakuwa na watu zaidi ya 1,000 ambao watatoka nje ya Dar es Salaam.
Kaimu Mwenyekiti wa Bawacha, Suzan Lyimo, aliwataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi zinazoendelea ili kuwa na uwiano sawa na wanaume.