KATIKA
kuhakikisha uchaguzi mkuu wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), unaendeshwa kwa uwazi na umakini ili kuepuka mitego ya
kuchomekewa wasaliti, chama hicho kimejipanga upya na kuusogeza hadi
Septemba 14 badala ya Agosti 31.
Hatua hiyo ni baada ya Kamati Kuu kubaini kwamba hakuna chombo cha
kuusimamia uchaguzi huo, na sasa imeamua jukumu hilo lifanywe na Baraza
la Wazee Taifa.
Kwa mujibu wa ratiba mpya iliyotangazwa jana na Mkurugenzi wa
Oganaizesheni na Uchaguzi, Benson Kigaila, uchaguzi wa Baraza la Wazee
ndio utatangulia kufanyika Septemba 6, ili kutoa nafasi kwa chombo hicho
kusimamia uchaguzi mkuu.
Kigaila alisema kuwa mkutano mkuu wa kuwachagua mwenyekiti, makamu
mwenyekiti Bara na Visiwani, utatanguliwa na chaguzi za mabaraza ngazi
ya kitaifa.
“Hadi kufikia Julai 30, uchaguzi wa kata utakuwa umekamilika na
Agosti 15, mwaka huu, uchaguzi wa majimbo na wilaya nao unapaswa
kukamilika ili kuruhusu uchaguzi ngazi ya mkoa uanze hadi Agosti 30
mwaka huu,” alisema.
Kigaila alisema uchaguzi wa Baraza la Vijana (Bavicha) utafanyika
Septemba 10 huku ule wa Baraza la Wanawake (Bawacha) ukipangwa kuwa
Septemba 11.
“Baada ya chaguzi hizo za mabaraza kukamilika, Kamati Kuu ya sasa
itakutana Septemba 12 kwa ajili ya kuandaa kikao cha Baraza Kuu
kitachaofanyika Septemba 13 mwaka huu, ili kuandaa mkutano mkuu wa
Septemba 14,” alisema.
Alisema baada ya mkutano mkuu, Baraza Kuu litakaa Septemba 15 kwa
ajili ya kumchagua Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Visiwani ili
Kamati Kuu mpya iweze kutambulishana.
Kigaila aliwataka wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali
za kitaifa kuchukua fomu kuanzia Agosti 10 hadi 25 katika ofisi za
majimbo, wilaya, makao makuu ya mabaraza hayo na ofisi za chama.
Alisema fomu hizo zinaweza kupatikana pia katika mitandao ya mabaraza
hayo na chama, lakini alionya kwamba lazima fomu hiyo baada ya kujazwa
irejeshwe katika makao makuu ya mabaraza hayo na chama ili iweze
kulipiwa.
“Gharama zinazotozwa kwa mgombea wa uenyekiti, katibu, mratibu wa
uenezi, mweka hazina na mwenyekiti wa kamati ya uratibu kama kwenye
wilaya kuna jimbo zaidi ya moja ni sh. 10,000.
“Gharama za kugombea nafasi ya mwenyekiti, makamu wenyeviti, katibu
mkuu, naibu katibu Bara na Visiwani ni sh. 50,000… mratibu wa uenezi na
mweka hazina ni sh. 30,000, wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu ni sh.
25,000,” alisema Kigaila.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Antony Komu, alisema CHADEMA
inatarajia kutumia sh. milioni 700 katika uchaguzi huo, hivyo aliwataka
wagombea wote kuhakikisha wanalipia fomu baada ya kujaza.
Hata hivyo, aliwaomba wanachama na wapenzi wa chama hicho kujitolea
kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo ambao alisema utakuwa na watu
zaidi ya 1,000 ambao watatoka nje ya Dar es Salaam.
Kaimu Mwenyekiti wa Bawacha, Suzan Lyimo, aliwataka wanawake nchini
kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi
zinazoendelea ili kuwa na uwiano sawa na wanaume.
No comments:
Post a Comment