Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wa kundi la Ukawa wakitoka bungeni waliposusia kuendelea kuhudhuria vikao vya bunge hilo, Aprili 16, mwaka huu, mjini Dodoma |
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameanza mkakati mpya wa kunusuru mchakato wa Katiba Mpya kwa kuitisha kikao cha wajumbe 27 wa Kamati ya Mashauriano ili kuondoa mpasuko kati ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wajumbe wengine.
Katika wajumbe hao wamo maaskofu wawili na masheikh wawili ambao Sitta amewateua kutoka katika Bunge la Katiba.
Sitta ameitisha kikao hicho jijini Dar es Salaam
Julai 24 wakati kukiwa na matamko tofauti kuhusu mustakabali wa katiba
hiyo, mengi yakieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyeshikilia
hatima ya mchakato na wapinzani wakisema mkuu huyo wa nchi ndiye
aliyesababisha suala hilo kwenda mrama.
Pia, Sitta ameitisha kikao hicho wakati viongozi
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakieleza kuwa suala la serikali mbili
kwenye muundo wa Muungano, ambalo liligawanya wajumbe, ndiyo msimamo wa
chama na wapinzani wakisema suala hilo halimo kwenye Rasimu ya Katiba na
ndiyo sharti lao la kurejea bungeni.
Akizungumza jana katika mahojiano na gazeti hili,
Sitta alisema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni
pamoja kutazama mwenendo wa majadiliano katika Bunge hilo na sura 15 za
katiba ili kujua yapi muhimu yanayotakiwa kupewa kipaumbele kabla ya
Bunge la Katiba kuanza tena vikao vyake Agosti 5.
“Sisi tumeshapeleka barua kwa wajumbe,
tumehakikisha zimekwenda na katika mkutano huo tutaelewana kuhusu
masuala hayo na mengine. Wasiotaka kuhudhuria wananchi watawaelewa na
wataamua iwapo nia ni kususa pekee au wenzetu wana ajenda ya siri,”
alisema Sitta.
Alisema katika mkutano huo, kutakuwa na utaratibu
maalumu ambao utahusisha viongozi wa dini walio ndani ya Bunge kutoka
madhehebu tofauti na baadhi ya wajumbe wengine kutoka kada tofauti ndani
ya Bunge hilo.
“Kutakuwa na watu karibu 27, mimi nikiwa
mwenyekiti. Atakayevimba kichwa na kudharau, wananchi watajua kuwa nia
yake ni tofauti na katiba,” alisema.
Sitta alisema tatizo kubwa katika Bunge hilo
litakalosababishwa na kutokuwapo kwa Ukawa ni namna ya upigaji kura,
lakini iwapo theluthi mbili ya wajumbe itatimia basi watakwenda kwa
mwenendo huo.
“Yapo mambo muhimu zaidi katika rasimu hii kama
vile tume huru ya uchaguzi, orodha ya haki za binadamu, uongozi wa
asilimia 50 kwa 50 kijinsia na kuwapa Zanzibar nafasi zaidi katika
Serikali ya Muungano, mambo ambayo ni makubwa kuliko muundo...ya nini
kuyapiga teke yote haya na kujikita katika muundo pekee,” alihoji.
Sitta ambaye pia alipingwa kwa kumpanga Rais
Kikwete kuhutubia Bunge hilo baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba tofauti na
kanuni, alisema kuwa kuususia mkutano huo wa Bunge katika kipindi chote
hicho siyo hasara kwa CCM, bali kwa wananchi kwa kuwa nia ni kupata
katiba bora na wala siyo kukomoana.
“Iwapo Ukawa watasusia kila kitu, basi wataonyesha
kuwa siyo wakomavu wa kisiasa,” alisema mbunge huyo wa Jimbo la Urambo
Mashariki.
“Inashangaza kuona kuwa kila maoni yao yanaposhindwa
wanasusa...iwapo watatokea watu ambao wataona Tume ya Uchaguzi haikidhi
haja. Je, watatoka nje ya mkutano?” alihoji.
Kubadili sheria
Pamoja na mambo mengine, Sitta alisema upo
uwezekano wa Ukawa kurudi bungeni lakini wakasusa tena kadiri mjadala
utakavyoendelea. Iwapo itatokea hali hiyo, Bunge litaangalia upya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.
“Katika sheria nyingine hatutakiwi kuangalia
idadi. Katika mkutano wa kibiashara au Bunge la Muungano na hata Baraza
la Wawakilishi, iwapo kuna wajumbe hawajatimia, basi wasiokuwapo
hawahesabiwi,” alisema.
Sitta alishawahi kufanya jitihada za kujaribu
kuwarudisha bungeni Ukawa siku chache baada ya kususia, lakini harakati
zake ziligonga mwamba.
Lipumba atoa masharti
Wakati Sitta akifanya mkakati huo, Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesisitiza msimamo wa Ukawa kutorudi
bungeni akisema ili warudi upande wa CCM unatakiwa kuheshimu rasimu ya
Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba na kuepuka matumizi ya
lugha chafu.
“Msimamo wetu uko wazi tu, kwamba Rasimu ya Katiba
iheshimiwe. Bunge la Katiba lina kazi ya kujadili na kupitisha Rasimu
ya Katiba, kwa hiyo lazima mjadala uongozwe hivyo, siyo vinginevyo,”
alisema Profesa Lipumba.
“Kiini cha rasimu ile ni uwapo wa muundo wa
Serikali ya shirikisho, yaani serikali tatu. Sasa ukienda kwenye Bunge
na kuacha mapendekezo hayo na kuleta serikali mbili, unaitoa wapi?”
alihoji.
Maalim Seif amvaa Kikwete
Katika hatua nyingine, Makamu wa Kwanza wa Rais
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amemtupia lawama Rais Jakaya Kikwete
kuwa amechangia kuukoroga mchakato wa Katiba kwa kufuata msimamo wa
chama chake badala ya maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba.
Akizungumza katika kipindi cha Dk 45 kinachorushwa
na ITV juzi usiku, Maalim Seif alisema kauli alizotoa Rais Kikwete
wakati akilihutubia Bunge la Katiba Machi 21, mwaka huu, zimeondoa imani
ya wananchi kuhusu kupatikana kwa Katiba inayotokana na maoni yao.
“Mchakato huu unamtegemea yeye. Hakuna ambaye amekamilika, Rais
ajiangalie kama alivyofanya ni sawa, kama siyo sawa arekebishe mambo
ili kujenga tena imani kwa wadau wote,” alisema Maalim Seif.
Alisema mwanzoni, Rais Kikwete alilichukulia suala
hilo kwa busara na hekima na alipokuwa akiona mambo yanakwama alikutana
na vyama na kusikiliza wanataka nini, lakini baadaye alijisahau na
kusikiliza matakwa ya chama chake.
“Mfano ni hotuba yake alipokutana na Baraza la
Vyama vya Siasa ilikuwa nzuri, lakini alipofungua Bunge la Katiba
akajisahau kama yeye ni Rais wa Watanzania wote akachukua msimamo wa
chama chake na kuihujumu Tume ya Katiba na mwenyekiti wake (Jaji
Warioba).”
Katibu huyo mkuu wa CUF ambaye ni Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar alisema iwapo Katiba Mpya haitapatikana wa
kulaumiwa ni CCM iliyoacha ajenda kuu na kuonyesha ubaguzi wa wazi.
Alisisitiza kuwa Ukawa wanataka kijadiliwe
kilichomo katika Rasimu ya Katiba na siyo rasimu ya CCM. Pia Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na kanuni za Bunge hilo zifuatwe.
Ushirikiano wa Ukawa
Maalim Seif alisema ushirikiano wa Ukawa utaendelea hata baada ya mchakato wa Katiba kumalizika.
“Hii ni pamoja na kuangalia kama tunaweza
kuachiana majimbo ya uchaguzi iwapo chama kimoja kitaonekana kina nguvu
zaidi kuliko kingine katika eneo fulani,” alisema Maalim Seif.
Alisema kama CCM ikiendelea na mchakato wa kuandika Katiba Mpya ni wazi kuwa Katiba hiyo itakataliwa na wananchi.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Maalim
Seif aligusia jinsi viongozi wa juu wanavyoshirikiana katika uongozi,
lakini akakiri kuwapo tatizo katika ngazi za chini, hasa kwa viongozi
kutokana kutokuwa na elimu kuhusu uendeshaji wa Serikali hiyo.
Alifafanua kuwa kuna jambo ambalo hawakufanya
vizuri wakati wakibadili katiba kuunda SUK kwa kutoweka kamati ambayo
itakuwa inazipitia ilani za vyama vinavyounda Serikali ili kutoa ilani
moja itayayotekelezwa kwa pamoja.
“Katiba yetu inasema ilani itakayofuatwa ni ile ya chama kilichopo madarakani. Hapo kidogo hatukufanya vizuri,” alisema.
Uandikishaji wapiga kura
Pia aligusia uboreshaji wa Daftari la Wapigakura
na kutolea mfano Zanzibar kwamba zimekuwa zikifanyika njama ili
wanachama wa CUF wasiorodheshwe katika daftari hilo.
“Ili ujiandikishe Zanzibar katika daftari, lazima
uwe na kitambulisho cha ukaazi na ili upate kitambulisho hicho lazima
upate idhini kutoka kwa masheha ambao hupewa maelezo na viongozi wa CCM
kuwanyima vitambulisho wanachama wa CUF,” alisema.
No comments:
Post a Comment