Watafiti wakitoa sampuli za damu kutoka kwa sokwe mtu katika utafiti wa Ukimwi huko Gabon |
Dawa yao inaweza kutumika kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa.
Mmoja wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili aliwaambia
waandishi wa habari juzi mjini Philadelphia, Marekani kuwa tofauti na
utafiti mwingine, wao wamegundua namna ya kukiondoa kirusi kilichoingia
kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye kukiua.
Alisema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.
Dk Khalili alisema ugunduzi wao ni wa hali ya juu
zaidi kwa sababu teknolojia ya kutengeneza dawa hiyo ni tofauti na
nyingine zilizokwisha kugunduliwa ambazo hazina uwezo wa kupenya ndani
ya seli za binadamu, bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake, ndani ya
mfumo wa damu.
“Dawa yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila
kuiathiri seli yenyewe na kukiua. Hivyo dawa hii itatumika kwa muda
fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna haja ya kuitumia wakati
wote kama ilivyo dawa ya kufubaza VVU (ARV).”
ARV huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na
kuendelea kuviacha hai vile ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4, hivyo
kufanya virusi kuzuka upya pindi mwathirika anapoacha kutumia dawa.
Mmoja wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya
Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford
Majani ameuelezea utafiti huo kama mwanga mpya katika teknolojia ya
kukabili VVU.
“Kama imepatikana teknolojia ya kukiondoa kirusi
ndani ya seli ni hatua nzuri ya kukabili VVU. Hili lilionekana kuwa gumu
mwanzoni,” alisema Majani.
Alisema imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya
seli na hata baadhi ya wanasayansi wamejaribu kutengeneza dawa
itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo likawa gumu.
“Inaweza ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua
seli zilizoathirika) lakini ikawa inaathiri vitu vingine ndani ya mwili.
Hilo halikubaliki. Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza kukifuata
kirusi kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa
zikiwamo ARV,” alisema.
Hata hivyo, Majani alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya dawa hiyo ni usalama wakati wa matumizi.
“Lazima dawa hiyo ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo
vingine pamoja na utendaji wa mwili kwa ujumla. Maana hapo ndipo dawa
nyingi zinaposhindwa… Tusubiri tuone hii inaweza kuwa na matumaini
zaidi,” alisema Majani.
Mkutano wa Ukimwi
Ugunduzi huo umekuja wakati wanasayansi, waunda
sera na wadau wa mapambano ya VVU wakiwa wanatoa kauli za kukata tamaa
kwenye mkutano wa Ukimwi unaomalizika kesho huko Melbourne, Australia.
Wanasayansi kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa
za utafiti za VVU wameweka wazi kuwa tafiti nyingi zilizokuwa na
matumaini zimeshindwa kufanya kazi kwa asilimia 100 baada ya dawa zake
kufanyiwa majaribio kwa sababu dawa zake zinapotumika, vipimo huonyesha
wamepona lakini baada ya muda VVU hurejea upya.
“Kinachoonekana ni kwamba virusi hivi hujificha
sehemu fulani ya mwili ili visiathirike na kusubiri mtu aache dawa ili
virejee upya kushambulia CD4,” alisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti
ya wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty ya Australia,
Profesa Sharon Lewin.
Dawa mpya inavyofanya kazi
Dk Khalili alisema wametengeneza dawa yao kwa
protini maalumu ambayo inakata sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi
cha Ukimwi na kukivuta nje.
Baada ya kukivuta, dawa huachana na seli hiyo na
kuiacha ikijitibu yenyewe na kupona kabisa kiasi cha kuendelea na kazi
zake za kinga mwilini mwa binadamu bila tatizo.
VVU kwa kawaida hushambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama kiwanda cha kuzalishia virusi vingine.
Kwa kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi, huacha kazi yake ya kinga ya mwili na badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU.
“Dawa yetu inafanya kazi kwa haraka, kwa makini na bila kuathiri seli,” alijigamba Dk Khalili.
Alisema tayari imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa wamehamishia majaribio kwa wanyama.
Katika maabara, alisema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100.
Dk Khalili anaamini kwamba majaribio hayo
yatawachukua miaka michache... “Lakini tunaamini ni mfumo ambao utaweza
kufanya kazi vizuri kwa binadamu.”
Alisema wanachofanya sasa ni kuangalia mfumo ambao utakuwa mzuri zaidi kwa ajili ya tiba ya binadamu.
Kwa namna teknolojia ya dawa hiyo ilivyo, alisema
wanaweza kuitumia kwa ajili ya kuwatibu wale ambao tayari wameambukizwa
na hata kuwakinga wale ambao siyo waathirika.
Uzuri wa dawa hiyo, pia alisema inaweza kutumiwa na mtu ambaye anatumia ARV pasipo kuingiliana kiutendaji.
Ugunduzi wao ulichapishwa kwenye Jarida la Taifa
la Elimu ya Sayansi la National Academy of Science la Marekani na
kuonekana kuvuta hisia za wengi.
Hali ya Ukimwi duniani
Akizungumza kwenye mkutano wa Melbourne, Profesa
Lewin alisema tafiti za sasa zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 14
duniani wanaishi na VVU.
Alisema mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambao bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika.
Alisema ingawa tafiti nyingi hazijaonyesha
matumaini waliotarajia ya kupata kinga na chanjo, bado juhudi
zinaendelea ili kuhakikisha wanafikia mahali HIV inakuwa haina nafasi
katika mwili wa mwanadamu.
Alisema pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza
kwenye tafiti nyingi, bado anaamini kwamba ipo siku chanjo na tiba
vitapatikana.
Wanasayansi waliohudhuria mkutano huo waliitaka
dunia isiogope kutokana na kushindwa kwa baadhi ya tafiti kama
ilivyokuwa kwa mtoto wa Jimbo la Mississippi, nchini Marekani ambaye
alitangazwa amepona na baadaye virusi vikaibuka upya.
No comments:
Post a Comment