JESHI
la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, jana limelazimika kutumia mabomu
ya machozi na kuwatia mbaroni waumini 29 wa Kanisa la Moravian Usharika
wa Kinondoni, Dar es Salaam baada ya kutokea vurugu za waumini kanisani
hapo.
Akizungumza na mwandishi wetu ,
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura, alikiri jeshi
hilo kuwatia mbaroni waumini hao na kusema kuwa, taratibu zikikamilika
watafikishwa mahakamani.
Hali ya kuvunjika kwa
amani kanisani hapo, ilianza saa moja asubuhi ambapo pande mbili za
waumini hao ambazo zimekuwa zikipingana muda mrefu, zilishindwa
kuelewana na kusababisha vurugu ambazo ziliingiliwa kati na jeshi hilo.
Awali kulikuwa na habari kuwa, zaidi ya watu 30 walikuwa ndani ya kanisa
hilo eneo la juu tangu juzi ambapo jana asubuhi, watu hao walipelekewa
vyakula na waumini wenzao ambao hawakulala ndani ya kanisa hilo.
Wakati waumini hao
wakianza kuingiza chakula ili kuwapelekea wenzao waliokuwa juu wakati
eneo la chini wakiendelea na ibada, ndipo hali ilipoanza kuchafuka baada
ya upande mmoja kuzuia chakula kisipelekwe kwa waumini waliokuwa juu ya
kanisa hilo.
Polisi walifika eneo la
tukio saa 1:40 wakiwa katika gari lenye namba za usajili PT 2118 ya
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kinondoni iliyoandikwa (OCD Kinondoni), ikiwa
na askari ambao walipiga kambi nje ya kanisa hilo.
Askari hao
hawakuingilia mzozo huo lakini waliwaonya waumini hao kuwa kama
mmojawapo ataanza kumshika mwenzake na kusababisha vurugu basi
watamkamata mara moja lakini ikiwa hawatagusana wao hawataingilia.
Waumini hao waliendelea kuzuiana ambapo vyakula vilivyoletwa kanisani
hapo ambavyo ni chipsi, kuku, soda, maji na miswaki vilimwagwa na vyombo
kutupwa nje ya eneo la kanisa hali iliyosababisha waumini hao kuanza
kushikana ambapo wengine walitumia hadi mafagio ili kupigana. Baada ya
kuona hali hiyo Jeshi la Polisi lililazimika kuwakamata wale
waliosababisha vurugu hali iliyosababisha askari mmoja kung’olewa
vifungo vitatu vya shati lake wakati wa vurugu za kuwakamata.
Baadaye polisi waliamua
kuwaachia waumini waliowakamata ambao ndio walioanza kuwagusa wenzao
lakini waliwaachia na kuamua kuondoka eneo la kanisa wakiwa na gari lao.
Dakika chache baadaye, liliingia basi dogo likiwa na waumini zaidi ya
20 ambao inadaiwa walitokea katika Kanisa la Mabibo na kuanza kuimba
ndipo hali ikachafuka ambapo polisi walirudi haraka kanisani hapo wakiwa
wameongeza askari wengine, kupiga mabomu ya machozi na kuwatia mbaroni
waumini hao.
Akizungumza na
waandishi wa habari, Mchungaji wa Kanisa hilo, James Mwakalile, alisema
anajisikia vibaya sana kuona mgogoro ukiendelea na wanaogombana ni walei
si viongozi. Alisema yeye anataka amani katika kanisa hilo na
amejitahidi sana kuwaita upande wa pili ili wazungumze lakini hakuna
lililofanyika.
Majirani waishio jirani
na kanisa hilo, wamesema wamechoshwa na hali ya mgogoro unaoendelea
kwani wanaoleta vurugu hizo wengi si wakazi wa hapo na kuitaka Serikali
kulifunga kanisa hilo kabla mauaji hayajatokea.
No comments:
Post a Comment