Chelsea ilishinda mabao 3-2 wakati huu ikijiandaa
na michuano mbalimbali msimu ujao, lakini walilazimika kukabiliana na
Akinfenwa ambaye alikuwa katika ubora wake.
Hadi wakati anatolewa uwanjani dakika ya 60,
Chelsea ilikuwa imekufa 2-0 huku Akinfenwa akimuhenyesha Terry na
wenzake. Hata hivyo baadaye walifunga mabao matatu ya haraka haraka
yaliyobadili matokeo ya mechi wakati Akinfenwa akiwa nje ya uwanja.
Licha ya umbo lake kubwa, Akinfenwa aliyezaliwa
jijini London Mei 10, 1982 anadaiwa kuwa na kilo 86 tu lakini ana uwezo
wa kubeba uzito wa kilo 180 ambazo ni mara mbili na uzito wake.
Tayari Fifa wamempitisha kama mchezaji mwenye
nguvu zaidi duniani huku wakimuingiza katika Video zao za michezo ya
kompyuta huku umbo lake likionekana kuwa kivutio kwa mashabiki wengi
duniani.
Mlinzi wa klabu ya Vale iliyo daraja la kwanza
England ambaye alicheza timu moja na Akinfenwa Northampton, Dan Jones
anaeleza kwamba ni kujisumbua tu kujaribu kutumia nguvu kumkaba mchezaji
huyo.
“Soka lake halibadiliki tangu tulipokuwa
Northampton. Anapenda kuuficha mpira miguuni na inajionyesha wazi kwamba
hana mpango wa kukimbia nao. Anapenda kukaa na mpira mguuni huku
akiwasukuma walinzi kwa nguvu zake.” Anasema Jones.
“Hauwezi kushindana naye kwa nguvu kwa sababu
utaishia kumfanyia rafu au atakutupa tu. Inabidi utumie akili sana
wakati wa kumkaba. Inabidi usitumie nguvu nyingi sana kumkaba.”
“Wakati mwingine akipata mpira tunamuachia tu na
kuangalia anachotaka kufanya kwa sababu tunajua hawezi kukimbia, yeye
huwa anaaangalia watu wanaofungua nafasi tu.” Anasema Jones.
Akinfenwa amedai kwamba hajawahi kucheza katika
Ligi Kuu ya England kwa sababu makocha wamekuwa wakiliogopa umbo lake na
kudhani kwamba atakuwa mzigo tu uwanjani kitu ambacho sio cha kweli.
“Nadhani naweza kutisha Ligi Kuu. Nadhani niko
sawa na Didier Drogba tu. Sijacheza madaraja ya juu kwa sababu kuna
mtazamo fulani wa jinsi ambavyo mwanasoka anapaswa kuwa na mimi
sionekani kuwa hivyo,” anasema Akinfenwa.
“Sitaki kuonekana mjinga lakini nimefunga zaidi ya
mabao 150 katika mechi 300. Waulize walinzi au makocha wa timu pinzani
watakwambia jinsi nilivyo balaa.” Anasema staa huyo
“Ningependa kukutana na John Terry na kumuharibu. Ningependa
kukutana na wachezaji kama Nemanja Vidic hili niwaonyeshe inakuaje
unapokumbana na mtu kama mimi.” Alijigamba staa huyo mzaliwa wa
Islington London.
Akinfenwa amekiri kwamba anapenda sana kula lakini hapendi kula vyakula vya kisasa na anapenda kula zaidi vyakula vya Kiafrika.
“Nakula sana, lakini sio McDonald au migahawa ya
vyakula vya haraka haraka. Lakini nadhani inabidi nipewe hisa na
migahawa ya Nandos kwa sababu nakula sana pale.”
Akinfenwa anavaa jezi kubwa (XXL) mara zote
amekuwa akiandamwa na mashabiki wa timu pinzani ambao huwa wanaimba kuwa
mchezaji huyo ana uwezo mkubwa wa kula nyama nyingi kuliko kufunga
mabao mengi.
“NImekubali kwamba inabidi nikutane na
mashambulizi haya. Nakubali kwamba nina umbo kubwa na ningesikitika kama
nisingekuwa hivi. Mara nyingi nakumbana na haya na ninapokumbana nayo
huwa nafunga.”
“Kitu kinachonifurahisha ni pale wanaposema kuwa
mimi ni mnene kama Eddie Murphy. Napenda mashabiki wa timu pinzani
wanaponishambulia kwa sababu mimi uwanjani naendelea kufunga tu.”
“Kama ningekuwa nasijikia kuwa mnene au mvivu,
basi ningefanya kitu kupunguza unene wangu. Sijawahi kufanya mazoezi ya
kupunguza uzito na makocha wengi walionifundisha wanakubaliana na ukweli
kwamba umbo langu ndivyo lilivyo.”
Akinfenwa ni mmoja kati ya wachezaji waliocheza
timu nyingi England. Mpaka sasa akiwa na umri wa miaka 32 licha ya
kutocheza katika Ligi Kuu ya England lakini amecheza klabu 14 za
madaraja ya chini.
Timu hizo ni FK Atlantas, Barry Town, Boston
United, Leyton Orient, Rushden & Diamonds, Doncaster Rovers, Torquay
United, Swansea City, Millwall, Northampton Town,
Gillingham,Northampton Town, Gillingham na AFC Wimbledon.
No comments:
Post a Comment