MWANASHERIA Yastinter Rwechungura (44), mkazi wa Boko-Njiabanda,
jijini Dar es Salaam, anayekabiliwa na kesi ya kumfanyia ukatili
msichana wake wa kazi, Merina Mathayo, amerudishwa rumande bada ya
kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Masharti hayo ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi yenye
thamani ya sh milioni 4 kila mmoja, lakini alishindwa kuyakamilisha kwa
kukosa mdhamini mmoja tu.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Amaria Mushi,
alisema mshitakiwa huyo arudishwe rumande kwa kuwa ameshindwa kutimiza
masharti kutokana na kuwa na mdhamini mmoja. Kesi imeahirishwa hadi
Julai 29, mwaka huu itakapotajwa tena.
Awali Mwendesha Mashitaka, Wakili wa Serikali, Masini Mussa, alidai
mgonjwa ambaye ndie mlalamikaji, afya yake inaendelea vizuri, hivyo
hapingi suala la dhamana kwa mtuhumiwa kwani ni haki yake kisheria.
Mshitakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 6 mwaka huu nyumbani
kwake maeneo ya Boko-Njiapanda kwa kumpiga Merina kichwani kwa kutumia
waya wa kompyuta na brenda, hali iliyomsababishia majeraha makubwa.
No comments:
Post a Comment