Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (Kulia) akiteta jambo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbrod Slaa wakati wa kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana Dar es Salaam |
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kinaamini kilishinda uchaguzi wa rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 chini ya mfumo wa vyama vingi.
Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbrod Slaa, ambaye
pia alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi huo,
alibainisha hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano maalumu na waandishi
wa gazeti hili.
Dk Slaa alisema kuwa ana uhakika kuwa chama chake
kilipata kura nyingi zaidi za urais, tofauti na mgombea wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete aliyetangazwa mshindi.
“…Baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, tulikataa
kumtambua Rais Kikwete, ingawa wakati ule hatukujua kwa uhakika kama
tulishinda. Kadiri nilivyozunguka, ndiyo kadiri tulivyoanza kuamini
kwamba tulishinda,” alisema Dk Slaa.
Alisema kuwa takwimu walizonazo zinaiaminisha Chadema kwamba ilishinda Uchaguzi Mkuu wa urais mwaka 2010.
“Sababu, unafika kwenye jimbo wanakusomea kura
ulizopata katika uchaguzi ule wakizilinganisha na alizozipata Kikwete na
Profesa Ibrahim Lipumba… wanasema Dokta hapa ulimshinda… kwa kura
20,000, pale ulimshinda kwa kura 15,000 pale ulimshinda kwa kura…,”
alifafanua na kusisitiza:
“Sasa ndiyo, tuna uhakika kama tulishinda na ndiyo
maana Kikwete hajawahi kwenda kwa wananchi kushukuru kwa kumchagua,
tofauti na tabia yake. Anachofanya sasa ni kwenda kuzindua miradi.”
Hata hivyo, Dk Slaa alisema hawakuweza kuendelea
na madai yoyote kwa sababu kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi,
mshindi wa urais akishatangazwa hairuhusiwi kupinga kwa namna yoyote
hata mahakamani, akieleza kuwa hiyo pia ndiyo sababu ya kuhitaji Katiba
Mpya.
Tume ya uchaguzi na CCM
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema
anasubiri kwanza kusoma kwenye vyombo vya habari alichokisena Dk Slaa
ndiyo ataweza kuzungumzia suala hilo.
“Kwa kuwa wewe ndiyo umeniambia Dk Slaa amesema hivyo, ngoja nione kwanza halafu tume itatoa maelezo,” alisema Jaji Lubuva.
Alipopigiwa simu Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara,
Philip Mangula ili atoe ufafanuzi kuhusu suala hilo, alimsikiliza
mwandishi wetu, kisha akasema yupo katika kikao na kukata simu
Wizi wa kura
Alipoulizwa kama wanaelewa kura zinavyoibwa
kutokana na malalamiko ya mara kwa mara ya Chadema na vyama vingine vya
upinzani, Dk Slaa alisema:
“Watu wengi wanafikiri huo ni wimbo tu wa kila
siku, sasa kama tunaibiwa tunyamaze? Tuseme uongo kama hatukuibiwa
kura…? Hakuna uwanja sawa katika uchaguzi.
“Uchaguzi kimsingi ni uwanja wa mpira. Umeshaona
kama katika uwanja wa mpira upande mmoja kuna kichuguu na kinaachwa
pale? Kinaondolewa. Kilichokosekana nchi hii ni dhamira ya kuondoa
vichuguu katikati ya kiwanja cha mpira; usipoondoa hivyo vichuguu
hutapata uchaguzi wa haki hata siku moja.”
“Kumbuka Arumeru tulitangaza, tukasema tumegundua
vituo hewa 55 vyenye jumla ya wapigakura 20,000, tulitangaza. Bahati
nzuri pale tuliweza kusimamia na mnakumbuka pale tulivyotukanana na
ofisa wa polisi ambaye leo ni DCI, unaweza kumpigia simu Mwigulu Nchemba
akueleze jinsi tulivyotunishiana misuli… tukafanikiwa pale kuokoa kura
20,000,”alisema.
Aliongeza: “Kalenga tulipiga kelele mwanzoni
kabisa kuhusu kuwapo majina mapya kwenye Daftari la Kudumu la
Wapigakura, kama daftari liliboreshwa… yaliingiaje kwenye daftari hili
la 2010. Ndiyo maana hatuna imani na Tume ya Uchaguzi….”
Alibainisha: “Mimi nina uzoefu wa kesi za uchaguzi
katika ushindi wangu mara tatu Jimbo la Karatu hakuna hata mara moja
ambayo sijapelekwa mahakamani.
“Mara ya mwisho niliponea chupuchupu, ndiyo akili
ikafunguka. Hukumu ilitolewa niwafungulie CCM kesi ya kughushi. “Kwa
sababu mahakama ilikuta kura zaidi ya 5,000 kupitia fomu namba 21b
(result form) siyo sandukuni ndipo walipoibia, lakini kwenye matangazo
ya awali nilishinda kwa kura 1,060, wamekwenda mahakamani wakasema
wamenishinda kwa kura 177.
“Kwa miezi mitatu niliangalia bila kugundua,
nikipiga hesabu naona ni kweli, kumbe walitengeneza vituo hewa na katika
vituo vya kujumlisha kura na kuvipa namba kama iliyopo kwenye fomu
halali za matokeo na kujaza kura za wizi. Waliipa CCM kura 300, Dk Slaa
kura 20, za kwao zilipanda zangu zilishuka, makahama imesema kazi hiyo
haikufanywa kijijini bali na wataalamu, ndiyo maana tunataka Tume Huru
ya Uchaguzi ili kuwa na uwanja sawa katika uchaguzi.”
Wingi wa wanachama CCM/Chadema
Kuhusu wingi wa wanachama wa Chadema na CCM, Dk
Slaa alisema: “Kwa taarifa yako nina taarifa ya mkaguzi aliyewauliza CCM
orodha ya wanachama wake ikashindwa kutoa. Kama hawana orodha ya
wanachama, hiyo milioni sita wanaitoa wapi? Uongo, ‘nawachalenji’ watoe
hadharani….”
“Ushahidi wa pili, kujua kama una wanachama ni
uhai wa wanachama. Taarifa ya CCM ya 2010 inaonyesha kwamba walikuwa
wanapata kutoka kwa wanachama wao Sh9 bilioni za kadi kama ada,
zimeshuka hadi Sh2 bilioni, utahesabu ni wangapi hao. Wasitudanganye…,
tuna vyanzo vingi vya kupata taarifa.
Mimi sitakupa leo nina wanachama wangapi kwa sababu tunafunga
kompyuta kwenye kila kanda, jimbo na kata, tumeanzisha ‘data base’ baada
ya kukamilika nitakwambia tuna wanachama wangapi,” alisema na kuongeza:
“Uongo wa CCM usikudanganye kwamba nguvu yao ni
wanachama, kama nguvu yao ni wanachama, uchaguzi haupigiwi kura na
wanachama, kura zinapigwa na wapigakura, wananchi wanaotaka huduma kwa
sababu wanalipa kodi.
Wanapiga kura ili wapate kiongozi ili asimamia kodi zao, waondokane na maisha magumu, wapate huduma za afya na elimu bora...”
No comments:
Post a Comment