KUNDI
la watu wanaoaminika kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za moto na
mapanga, wamevamia watalii 17 kutoka mataifa mbalimbali na kuwapora
kiasi kikubwa cha fedha, kamera na kompyuta mpakato (Laptop), kisha
kuwajeruhi wanne na kutoweka.
Tukio hilo kubwa kuwahi kutokea siku za hivi karibuni mkoani
Kilimanjaro, limetokea juzi alifajiri eneo la Mailisita kwenye hoteli ya
kitalii ya Weruweru River Lodge inayomilikiwa na mfanyabiashara
Cuthbert Swai, ambaye pia anamiliki kampuni ya wakala wa utalii ya
Ahsante Tours ya mjini hapa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, watalii hao kutoka mataifa
mbalimbali, walikumbwa na mkasa huo wakiwa wamelala ndani ya mahema
majira ya saa 9 alfajiri, ambako walitishwa kwa bunduki na mapanga kabla
ya kuporwa mali zao.
Katika tukio hilo, watalii watatu waliporwa zaidi ya dola 2,090 za
Marekani, mmoja pauni 110 za Uingereza na euro kiasi kisichojulikana, sh
milioni 5.4, kamera zaidi ya nne na moja ikiwa na thamani ya sh milioni
1.5 na nyingine ikiwa na thamani ya dola 3,000 za Marekani, zaidi ya sh
milioni 4.5.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizothibitishwa na Kamanda
wa Mkoa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Robert Boaz,
majambazi hao kabla ya kufanya uhalifu huo, waliwakusanya watalii hao
eneo moja na kuanza kuwapora kila kitu walichokuwa nacho.
Hata hivyo, Kamanda Boaz hakuweza kulizungumzia tukio hilo kwa kina,
ikiwamo kutaja majina ya watalii hao, uraia wao na thamani halisi ya
mali walizoporwa, kutokana na kuwa katika pilikapilika za kwenda uwanja
wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kupokea ugeni wa Spika wa
Bunge la Nigeria.
Kamanda Boaz, aliwaambia waandishi wa habari waliofika ofisini kwake
jana kuwa tukio hilo atalitolea maelezo kamili leo kutokana na kutingwa
na ugeni huo.
Ofisa mmoja wa polisi aliyeomba kutotajwa jina lake, alisema kuwa
miongoni mwa watalii hao walioporwa mali zao, wako wanne waliokuwa
wakijiandaa kuondoka na ndege alfajiri hiyo kupitia KIA.
Aliongeza kuwa watalii hao walijikuta katika mkasa huo, baada ya
dereva wa gari lililokuwa limewabeba kuwashwa kuashiria kuondoka
hotelini hapo, ndipo majambazi hao walipolivamia na kuanza kuwashambulia
na hatimaye kuwapora mali zao ingawa watalii hao waliendelea na safari
yao.
Mmoja wa wakurugenzi wa hoteli hiyo, Stella Shangali alipoulizwa juu
ya tukio hilo, hakukiri wala kukanusha kuwapo, zaidi ya kumtaka
mwandishi kuwasiliana na kamanda wa mkoa kwa ufafanuzi zaidi.
No comments:
Post a Comment