Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta akisisitiza jambo juzi, baada ya mkutano wa Kamati ya Maridhiano uliofanyika jijini Dar es Salaam. Picha |
Wakati Bunge Maalumu la Katiba likiazimia kuzifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwabana wajumbe wa Bunge hilo ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), viongozi wa kundi hilo wamesema hawatishwi na uamuzi huo na kwamba wataendelea kususia vikao hivyo.
Kikao kilichokuwa kiwe cha mashauriano
kilichoitishwa juzi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta
kiliazimia kuzifanya marekebisho baadhi kanuni za uendeshaji kwa lengo
la kusimamia nidhamu wajumbe wake, hatua inayotafsiriwa kwamba
inawalenga Ukawa.
Jana Sitta akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi
alisema mabadiliko yanayokusudiwa kufanywa yatahusisha masuala ya
nidhamu, yakiwamo fujo na utoro, mambo ambayo hivi sasa hayawezi
kudhibitiwa moja kwa moja na mwenyekiti wa Bunge hilo.
Sitta alikuwa akitoa ufafanuzi wa taarifa
iliyotolewa na ofisi yake jana na kusomwa mbele ya waandishi wa habari
na Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad, ikieleza maazimio ya
kikao ya usuluhishi alichokuwa amekiitisha kwa ajili ya kutanzua mzozo
unaotishia kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Hata hivyo, Ukawa unaoundwa na wajumbe wa Bunge
Maalumu kutoka Vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na baadhi ya wajumbe
kutoka Kundi la 201 walioteuliwa na Rais, walisusia kikao hicho na
kusababisha uamuzi uliofikiwa kuwa wa upande mmoja.
Hata hivyo, wakizungumza jana kwa
nyakati tofauti, viongozi wa Ukawa ambao ni Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na yule CUF, Profesa Ibrahim Lipumba walisema hawatishwi
na mabadiliko ya kanuni yanayokusudiwa kufanywa na kwamba wataendelea
kususia vikao hivyo hadi hoja zao zitakapozingatiwa.
Ukawa walitoka bungeni siku chache kabla ya
kuahirishwa kwa awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu mwezi Aprili mwaka huu,
kwa madai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatumia wingi wa wajumbe
wake kutaka kufutwa kwa baadhi ya mapendekezo ya wananchi yaliyomo
kwenye Rasimu ya Katiba.
Kauli ya Sitta
Sitta aliongeza kuwa moja ya kasoro
katika uendeshaji wa Bunge ni pale makundi kama Ukawa na Tanzania Kwanza
yanapotambuliwa kama makundi rasmi ya Bunge Maalumu, wakati makundi
rasmi ni wabunge, wawakilishi na Kundi la Wajumbe 201 wa kuteuliwa na
Rais.
“Bunge hili lina uhuru wa ajabu ambao ni mkubwa
kuliko Bunge jingine lolote, Bunge ambalo hata uongozi wake hauwezi
kumchukulia mtu hatua kwa utovu wa nidhamu eti mpaka umuone mtu anafanya
makosa, umpeleke kwenye Kamati ya Kanuni na hivyo ndiyo inakuwa
imekwisha maana kama ana watetezi wake wanamtetea,” alisema Sitta na
kuongeza:
“Matokeo yake wananchi wanalalamika kwamba hakuna
nidhamu bungeni na kwamba kiti kimeshindwa kuchukua hatua, sasa
unachukuaje hatua wakati kanuni zetu ndivyo zilivyo?”
Aliendelea: “Yako mambo mengi yanapaswa kufanyika
na tuna siku 63 tu za kukamilisha kazi tuliyopewa sasa hatuwezi kutumia
fedha za umma na watu wengine wanafanya mzaha, leo huyu anachukua posho,
mara anaondoka, haya mambo lazima yatafutiwe dawa.”
Kauli hiyo ya Sitta inaungwa mkono na taarifa iliyotolewa mapema
jana ikisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge kutokuwa
na vipengele vinavyozuia utoro, ukosefu wa nidhamu na matendo mengine
yanayolenga kuvuruga mchakato wa Katiba, ni kasoro ambayo lazima
itafutiwe ufumbuzi katika kikao kijacho.
Taarifa hiyo inasema kitendo cha Ukawa kuendelea
kususia Bunge, kinapuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja
na madhehebu ya dini na juhudi za usuluhishi za kutaka kuwezesha vikao
vya Bunge hilo viendelee.
“Mambo hayo yote yanazua mashaka kuhusu lengo la
wasusiaji kwamba pengine ajenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo
upatikanaji wa Katiba. Kwa mtindo huu wa kususa ni vigumu kuweza kupata
mwafaka” inasomea sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Sitta.
Mbowe na Lipumba
Akizungumzia uamuzi huo, Mbowe alisema haamini
kwamba kauli kama hizo zimetolewa na Sitta ambaye ni msomi na mwanasiasa
mzoefu anayefahamu misingi ya hoja na maridhiano.
“Kanuni hazitungi Katiba, Katiba inatungwa na
utashi wa wale tuliopewa dhamana ya kufanya kazi hiyo, sasa ni kwa
bahati mbaya kwamba Sitta anafikiri vitisho vya kutunga kanuni za
kutubana vitasaidia, haviwezi kusaidia chochote,” alisema Mbowe na
kuongeza:
“Ukawa hatutishwi na mabadiliko ya kanuni, waende
wakabadilishe ili dunia nzima iwashuhudie wakipitisha Katiba ya upande
mmoja, wasikwepe hoja wanapaswa kutafakari mantiki ya hoja zetu na siyo
kutoa vitisho vya kutulazimisha kwenda bungeni, Katiba ni hiari na wala
haitungwi kwa vitisho.”
Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba alisema
Bunge Maalumu la Katiba haliwezi kubadili kanuni ili kumbana au kumfuta
mjumbe wa Bunge hilo bila kwanza kubadilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba.
“Kwanza, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa
kufanyiwa marekebisho na Bunge la Jamhuri ya Muungano na siyo Bunge
Maalumu la Katiba. Pili, hata Rais aliyeteua wajumbe 201 wa Bunge la
Katiba hawezi kuwafukuza kwa sababu haijaelezwa katika Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, sasa Bunge la Katiba litaweza vipi kuwafukuza,”
alihoji.
Profesa Lipumba alisema wajumbe 201 waliteuliwa
kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kufafanua kuwa hata
wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi nao hawawezi
kufukuzwa kwa kubadilishwa kwa kanuni za Bunge la Katiba.
“Mbunge wa Jamhuri ya Muungano au Baraza la
Wawakilishi ili apoteze sifa za kuwa mjumbe wa Bunge la Katiba ni lazima
kwanza apoteze sifa za kuwa mbunge,” alisema.
Alisema kuwa msimamo wa Ukawa ni kutoshiriki kikao
cha Bunge hilo hadi hapo wajumbe wote 629 wa Bunge hilo
watakapokubaliana kuheshimu Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya
wananchi yenye msingi wa muundo wa serikali tatu na siyo serikali mbili.
Taarifa ya Kamati
Mapema katika taarifa iliyosainiwa na Sitta kisha
kutolewa kwa waandishi wa habari na Hamad, inaeleza kuwa vikao vya Bunge
Maalumu hilo vitaendelea mpaka mwisho hata kama Ukawa wataendelea
kususia vikao vyake.
“Kuanzia Agosti 5 Bunge liendelee kwa kuzingatia
upya baadhi ya kanuni zake ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kuwa
kazi ya kujadili na kupitisha Katiba inayopendekezwa inakamilika ndani
ya siku 63 zilizosalia kisheria, yaani 60 za nyongeza na tatu pungufu ya
zile siku 70 za awali,” inasomeka taarifa hiyo.
Hamad alisema kikao cha juzi kimeamua Bunge hilo
kuendelea kutokana na kuwa na masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo
yanawaunganisha Watanzania, yakiwamo usawa wa kijinsia katika nafasi za
uongozi, kuikarabati Tume ya Uchaguzi (Nec), kurekebisha kikatiba
masuala ya muungano na ukomo wa vipindi vya uongozi.
Taarifa hiyo ilieleza kukerwa na mikutano ya Ukawa
inayofanyika katika mikoa mbalimbali nchini. “Hatua ya baadhi ya
wajumbe wa Ukawa kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo mwafaka
na siyo wakati wake. Bunge la Katiba liwajibike katika siku za usoni
kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa Katiba kadiri
ulivyojitokeza” alisema Hamad.
No comments:
Post a Comment