BEKI wa Chelsea, John Terry, amesema kazi zote alizokuwa
akifanya Frank Lampard kwenye kikosi hicho zimepata mrithi makini na
kusisitiza kwamba Cesc Fabregas anaiweza kazi hiyo.
Lampard, 36, ameruhusiwa kuondoka klabuni hapo
baada ya mkataba wake kumalizika na kwenda kujiunga na klabu ya Ligi Kuu
Marekani, New York City.
Baadaye Chelsea ikamnasa Fabregas kutoka Barcelona
na kumsainisha mkataba wa miaka mitano huku akitua Stamford Bridge kwa
ada ya Pauni 30 milioni.
Lakini, wakati mashabiki wakiwaza itakuwaje kwa
kiungo mpambanaji wao Lampard kuondoka klabuni hapo. Terry, anaamini
Fabregas ataweza kuvaa
vyema viatu vilivyoachwa na Mwingereza huyo ambaye ni kinara wa mabao wa nyakati zote klabuni hapo.
“Huu ni usajili makini sana,” alisema Terry alipozungumza na Jarida linalochapishwa na klabu hiyo.
“Ni mzuri sana anapokuwa na mpira. Ni kiungo
anayecheza goli hadi goli. Pia amekuwa akifunga mabao kwa wingi na
kupiga pasi za maana. Nakumbuka alichokuwa akikifanya alipokuwa Arsenal.
Nina hakika atakuwa mtu muhimu sana klabuni
Chelsea kwa sasa na miaka ijayo.” Lampard alitangaza uamuzi wake wa
kuihama Chelsea Juni mwaka huu na Terry anakiri wazi kuumizwa na jambo
hilo kwa sababu alikuwa swahiba wake wa karibu sambamba na Ashley Cole,
aliyetimkia AS Roma.
No comments:
Post a Comment