Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Frank Sanga, mjini Dodoma hivi karibuni |
Ridhiwani (35), ambaye alishinda kiti cha ubunge
wa Jimbo la Chalinze Aprili mwaka huu, alitaja majina hayo katika
mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika mjini Dodoma hivi
karibuni.
Miongoni mwa aliowataja kuwa wana sifa ni makada
watano walio chini ya uangalizi wa CCM wa mwaka mmoja baada ya kubainika
kuanza kampeni za urais mapema, mawaziri wawili waliopoteza nyadhifa
zao katika kashfa ya Operesheni Tokomeza, mwanamke mmoja na Rais wa
Zanzibar.
“Kutaja majina tu, naweza kuorodhesha wengi tu.
Naweza kuorodhesha hata watu 500, kwa sababu tunaona wengi sana,”
alisema mtoto huyo wa Rais Kikwete ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa muda
mrefu akitokea umoja wa vijana wa chama hicho, UVCCM. “Kwa mfano, kwa
upande wa Bara tunao Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja, January Makamba,
Bernard Membe, Steven Wassira, Edward Lowassa na Asha-Rose Migiro,”
alisema.
Aliongeza: “Hawa ni kwa uchache zaidi… ni baadhi
ya watu ambao wanatajwa kwa upande wa Bara, lakini jambo la msingi ni
nani mwenye sifa za kuwa rais.”
Alisema pamoja na kwamba wanasiasa hao wote wanazo
sifa za kuiwania nafasi hiyo ya juu, vikao vya chama ndivyo vitakuwa na
nafasi ya kuwachuja ili kupata wanaotosha. “Kama wanatosha au la, vikao
vya chama vitakaa kuamua licha ya kuwa hao wote niliowataja, kwa sifa
za kugombea urais wote wanajitosheleza. Wana sifa, wana uwezo wa
kugombea na wana uwezo wa kushinda, hao ni kwa upande wa Bara,” alisema.
Alipoulizwa hali ikoje kwa upande wa Zanzibar,
Ridhiwani alisema, “Sisi chama chetu kina utajiri wa watu kwa upande wa
Zanzibar kuna Shamsi Vuai Nahodha, Hussein Ali Mwinyi, Dk Seif Ally Iddi
(Makamu wa pili wa Rais Zanzibar) na Dk Mohammed Ali Shein, Rais wa
Zanzibar. Hawa ni watu ambao wana uwezo na hata wakipewa jukumu la
kuongoza nchi hii wanaweza. Tunao wengi sana.”
Membe, Wassira, Lowassa, Ngeleja na Makamba
walipewa adhabu na Kamati ya Maadili ya CCM ya kutogombea nafasi yoyote
ndani ya chama wala kufanya kampeni baada ya kudaiwa kukiuka taratibu za
chama hicho, wakati Nchimbi na Nahodha walilazimika kujiuzulu nyadhifa
zao za uwaziri kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza ambayo ililenga
kushughulikia majangili, lakini ikahusishwa na vitendo vya ukiukaji
haki za binadamu.
Ridhiwani hakumtaja Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye ambaye pia anatumikia adhabu hiyo ya Kamati ya Maadili ya CCM.
Baadhi kukwama
Hata hivyo, Ridhiwani alidokeza kuwa wapo baadhi
ya wanasiasa watakaokwama kufikia lengo hilo kutokana na kukabiliwa na
kesi ndani ya chama, ambazo hakuzitaja wala kutaja wahusika.
“Kuna watakaopungua kutokana na kesi
zinazowakabili katika chama ambazo zinawafanya wapungukiwe sifa. Kwa
maana hiyo kuna watu kama wanne hivi (wa Bara) unawatoa na ukiwatoa
unabakiwa na watatu, sasa unaweza kujiuliza hao watakaobaki watatu, je,
wanatosha?”
Alipotakiwa kueleza iwapo angepewa nafasi ya kuteua mgombea
mmoja wa CCM atakayepambana na vyama vingine katika uchaguzi mkuu
mwakani, Ridhiwani alijibu kwa ufupi kuwa akisema, “Hilo siwezi kujibu.”
Amsaidia Membe
Ridhiwani pia alizungumzia uchaguzi wa ndani ya
CCM akikiri kuwa alimsaidia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Membe kushinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
“Ni kweli katika uchaguzi wa NEC nilimsaidia
Bernard Membe. Nilimsaidia si kwa sababu ya kuwa katika kundi lolote,
ila nilimwona kuwa ana sifa ya kuingia kwenye NEC, hili jambo lazima
watu waelewe,” alisema Ridhiwani.
Hata hivyo, Ridhiwani alieleza kukerwa na kitendo
cha baadhi ya wajumbe ambao katika uchaguzi wa ndani badala ya kufanya
kampeni kwa mtu wanayemtaka, wanafanya kampeni dhidi ya yule
wasiyemtaka. “Hili ni jambo la ovyo ambalo nimewahi kuliona katika chama
chetu… na tangu nimezaliwa sijawahi kuliona. Kwa mara ya kwanza
nimekuja kuliona kwenye NEC,” alisema Ridhiwani ambaye kitaaluma ni
mwanasheria.
“Pale tunagombea nafasi kumi halafu kibaya zaidi
ni kwamba watu wanakampeni ili mtu asipite. Ndiyo maana mimi nikasimama
kuwaomba watu wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani tumsaidie Membe.
Walionyesha ushirikiano wa kutosha na wakamchagua kwa kura nyingi na
akaingia NEC. Mambo ya makundi mimi sina wala siasa yangu haiangalii
kundi,” alisema.
Je, atamuunga mkono pia kwenye urais? Ridhiwani
anasema: “Hapana. Hiyo siyo tafsiri sahihi. Naomba niseme jambo moja.
Mmoja wa watu walionipigia kura Chalinze ni baba yangu, japo alisema
amempigia kura mgombea wake, lakini nafahamu kuwa mgombea wake ni mimi
kwa sababu ninatoka katika chama chake, hiyo ni tafsiri ya kawaida
kulingana na maneno yake aliyoyasema.
“Baba yangu aliponipigia kura kuwa mbunge, kesho
nitakapogombea nafasi ya uenyekiti wa CCM wa mkoa, mfano Mkoa wa Pwani
halafu akanikataa, tafsiri haiwezi kuwa baba kamkataa mwanaye.”
Alisema jambo la msingi ni kuwa mtu anatosha
katika nafasi gani, hivyo ikitokea Membe akawa katika nafasi hiyo na ana
sifa kuliko wengine waliojitokeza, atamsaidia katika kuhakikisha
anafanikiwa.
“Lakini ikitokea kwamba kuna watu wana sifa zaidi
yake hatuwezi tukakubali kuipeleka hii nchi katika misingi ya kujuana.
Tutaangalia mwenye sifa ni nani,” alisema kwa kujiamini.
Sifa za rais ajaye
Akizungumzia sifa za mtu atakayerithi kiti hicho,
Ridhiwani alisema: “Matamanio yangu ni kumwona rais atakayefuata awe mtu
mwenye uwezo wa kuendeleza pale Bwana Jakaya Kikwete alipoachia. Siyo
rafiki yangu, mchumba wangu wala si mshikaji wangu wala mshiriki wangu
katika baishara. La msingi ni mtu ambaye anaweza.”
Ridhiwani alisema ndani ya CCM kuna watu wengine ambao wana sifa
na uzuri wa CCM haiangalii ni nani amejitokeza bali pia wanaangalia
watu ambao wapo nje ya utaratibu wao, lakini ni makada wazuri ambao hata
wakiletwa, wana sifa za kutosha.
“Ndiyo maana siwezi kujiingiza katika suala la
kushabikia nani awe rais. Tutaangalia ni nani mwenye sifa atajitokeza na
nani ambaye tukimuunga mkono anaweza kututoa hapa tulipo na kutupeleka
kuzuri zaidi. Hakuna urafiki katika suala la nchi, tunaangalia masilahi
ya nchi. Siyo masilahi ya nchi tu, ila masilahi makubwa ya nchi,”
alisisitiza Ridhiwani.
Alisema pamoja na kwamba kwenye vitabu vya
mwongozo zimetajwa sifa za mgombea urais, yeye binafsi akiulizwa sifa za
rais anayetakiwa ni kuwa lazima awe mtu ambaye atakuwa sehemu ya kupata
ufumbuzi wa matatizo na siyo sehemu ya walalamishi.
Alisema mgombea lazima awe mtu ambaye ukimwambia
kwamba wananchi hawana chakula, atakuja na suluhisho ya nini kifanyike,
ukimwambia shilingi imeshuka atakuja na ufumbuzi, akiambiwa kuhusu suala
la ajira, atatafuta ufumbuzi na siyo na yeye kuwa sehemu ya
walalamishi.
“Tunamtaka rais ambaye atatambua anaongoza watu
gani kwa sababu tuna tatizo kubwa ambalo ni tishio kwa nchi yetu sasa,
mgawanyiko wa madaraja katika maisha ya watu. Rais lazima ajue anaongoza
watu wa namna gani. Wakati mwingine unakuwa na mtu ambaye anaangalia
kundi la watu wake wanaomzunguka tu, akidhani kuwa ndiyo nchi, rais wa
namna hiyo hapana,” alisema.
Aliongeza: “Rais ninayemtaka anapaswa awe mtu ambaye anaweza kushughulikia mambo yanayogusa maisha ya watu wote.”
“Pia, rais ninayemtaka lazima ajue misingi ya
chama chetu. Tuna tatizo kubwa kwa wanasiasa wetu wa leo wengi
hawafahamu nini umuhimu wa chama…Tuna wabunge wa CCM ndani ya Bunge
ambao tangu wameingia bungeni ni miaka mitano, hawajawahi kuchangia
chama.
Alisema katika hali hiyo, anahitajika rais
anayefahamu kuwa chama kinatakiwa kisemewe na demokrasia ya chama lazima
iwe kubwa. “Mfano watu wa CCM wanatakiwa kupewa uhuru wa kusema katika
yale ambayo yanawafurahisha na yale ambayo wanaona hayafurahishi ili
ituwezeshe sisi wanachama kubadilika. Mojawapo ya sifa ya chama ni
kubadilika kutokana na wakati na mazingira ambayo ndiyo moja ya sifa ya
chama na chama chetu sisi kimethibitisha hilo,” alisema.
Ridhiwani alisema ni vizuri apatikane rais ambaye
ni muwazi katika demokrasia na atakayeweza kulinda usalama wa nchi hii
kwa sababu nchi iko katika kipindi kigumu na kiongozi huyo awahakikishie
wananchi kuwa anaweza kutengeneza nyanja mpya za watu kupata ajira.
Ajira 1,000,000 za JK
Ridhiwani, ambaye mwaka 2010 alikuwa mmoja wa
wanachama wa CCM waliopewa jukumu la kuzunguka nchini kutafuta watu wa
kumdhamini baba yake ili apitishwe kugombea tena kiti cha urais, pia
alizungumzia ahadi ya Rais Kikwete ya ajira milioni moja, akisema kuwa
imetimia lakini wapo watu wengine milioni tatu wasiokuwa na ajira.
“Tumeona hapa Rais Kikwete alipokuwa anaingia
madarakani alituahidi ajira milioni moja, lakini mipango ya Serikali
ikafungua vyuo vingi, leo hii ukihesabu ajira milioni moja kwa Serikali
zimefika, lakini tuna wengine milioni tatu bado wapo benchi wanasubiri
ajira,” alisema.
Aliongeza kusema: “Sasa tunafanyaje, huyu rais anayekuja lazima
atupe ufumbuzi wa hilo. Siyo ufumbuzi wa kuangalia nyuma kwamba watu
wanaohitaji chakula ni watu kumi, lakini huangalii kumi hao ambao baada
ya kula watazaa, kwa hiyo kesho haitakuwa watu kumi, watakuwa zaidi ya
watu 20.
“Hili ni jambo ambalo kwangu naona ni changamoto
ambayo rais anayekuja lazima alitambue hilo. Pamoja na hilo rais
anatakiwa pia awe na uwezo wa kutambua michango ya wenzake
waliotangulia. Siyo shughuli kubwa ya rais atakayekuja iwe ni kuanza
kukosoa wenzake kwamba huyu alifanya jambo la ovyo; hapana. Afanye kama
vile ambavyo waliotangulia wamefanya,” alisisitiza.
Alitoa mfano wa jinsi marais walivyosahau ya nyuma na kusonga mbele.
“Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
alipomaliza muda wake alipokuja Mwinyi hakuangalia Nyerere alikosea
wapi, alichoangalia ni kuwa nchi inakabiliwa na changamoto gani na
tunakwendaje mbele.
“Ametoka Rais Mwinyi, akaja Mkapa ambaye pia aliangalia nchi inakwenda wapi, amekwenda mbele.
Akaja Rais Kikwete ameangalia nchi inakwenda wapi
na akaendelea mbele. Hivyo rais anayefuatia lazima awe na uwezo huo.
Aangalie mwenzake ameishia wapi na aendeje mbele. Yamefanyika mambo
mengi nchini, ni vipaumbele vipi alivyonavyo. Lazima uwe na rais wa
namna hiyo.
“Rais ajaye atambue watu katika matabaka yote.
Tunao wafanyabiashara, wacheza muziki, waigizaji wa filamu hivyo lazima
rais awatambue na lazima awe tayari kuwasaidia, atumie nafasi yake
kuhakikisha kwamba watu hawa wanapatiwa haki zao.
“Rais ambaye anakuja lazima atambue watu katika
kada mbalimbali. Mfano, waandishi wa habari wana malalamiko yao, lazima
afungue mlango kwa kukutana nao na azungumze nao ili waseme shida zao
kama suala la sheria. Hapa tunazungumzia muswada wa kuletwa bungeni,
hiyo sheria tunafanyaje? Rais lazima atambue hayo.
“Rais lazima atambue juhudi zinazofanywa na
wanamichezo wetu. Jinsi gani yeye anaweza kushiriki na kusaidia
kunyanyua kile kiwango ambacho michezo yetu imefikia kwa kushirikiana na
vyombo mbalimbali vya michezo.”
Kuhusu jimbo lake la Chalinze, Ridhiwani alisema
limekaa kwa miaka mitatu bila mtu wa kuwasemea kwa sababu mbunge wao,
Said Bwanamdogo alikuwa mgonjwa na baadaye kufariki dunia. Hivyo
anahitaji kutumia muda uliosalia kufidia pengo hilo.
“Mimi nimekuja humu ndani (bungeni) lazima nifidie
ile miaka mitatu ya nyuma. Lazima tuikumbushe Serikali kwamba ilikuwa
na mipango kadhaa kwa ajili ya jimbo la Chalinze na kwa nini
haijatekelezwa hadi sasa.
Ile ya kuipa nguvu, tunaipa nguvu, zile za kushirikiana tunaangalia jinsi gani tunashirikiana,” alisema.
No comments:
Post a Comment