Wednesday, 9 July 2014

Magaidi waingia arusha na kurusha mabomu


Majeruhi Deepak Gupta aliyepoteza mguu wake kutokana na shambulio la bomu lililotokea juzi usiku katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine, jijini Arusha

Milipuko ya mabomu nchini inazidi kuongezeka baada ya bomu jingine kulipuka mjini Arusha na kujeruhi vibaya watu wanane wenye asili ya Kiasia katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine ulioko eneo la Arusha Gymkhana.
Mlipuko huo, uliotokea majira ya saa 4:30 usiku juzi karibu na eneo la Mahakama Kuu, ni wa tano kutokea jijini Arusha baada ya ule uliotokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti, kwenye mkutano wa kampeni za udiwani wa Chadema, Baa ya Arusha Night Park na nyumbani kwa Imam wa Msikiti wa Answar Sunna.
Mbali na Arusha, ambayo inategemewa kuingiza fedha nyingi kutokana na sekta ya utalii, mji mwingine ambao umekuwa ukikumbwa na milipuko ya mabomu ni Unguja, ambao pia ni maarufu kwa utalii.
Mlipuko wa juzi ulitokea wakati watu hao walipokuwa wakipata chakula na burudani kwenye mgahawa huo ambao mara nyingi wateja wake ni raia wa kigeni. Mmoja wa majeruhi hao aliyetambulika kwa jina la Deepak Gupta(25), alipoteza mguu wake wa kushoto uliokatwa kutokana na kujeruhiwa vibaya.
Taarifa za mashuhuda zinasema washambuliaji hao walitumia usafiri wa pikipiki katika kutekeleza azma yao.
Mbali na Guptam, majeruhi wengine katika tukio la juzi ni Vinod Suresh, Ritwik Khandelwal, Raj Rajin, Prateek Javey, Manci Gupta, Marisa Gupta na Mahushi Gupta ambao ni ndugu na walipelekwa katika Hospitali ya Selian.
Mkurugenzi wa tiba wa Hospitali ya Selian, Dk Paul Kisanga alisema walipokea majeruhi wanane kati yao wanawake ni watatu ambao baada ya kufanyiwa uchunguzi wameonekana wana vipande vya vyuma kwenye miili yao.
“Kuanzia jana usiku (juzi) tumekua tukiwapa matibabu hadi asubuhi. Wagonjwa wengine wanaendelea vizuri isipokuwa mmoja ndiye amepoteza mguu wake wa kushoto na yuko katika chumba cha uangalizi maalumu,” alisema Dk Kisanga.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na milipuko ya mabomu inayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini kwa kutoshiriki katika mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu alitoa tahadhari hiyo jana alipozungumza jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kutokea mlipuko huo Arusha.
Kamishna Mngulu alisema tayari jeshi hilo linafanya operesheni maalumu kubaini chanzo cha mlipuko huo wa jana na wameshawakamata washukiwa wawili wanaodhaniwa kuhusika na mlipuko huo.
“Mlipuko huo umetokea siku chache baada ya kutokea kwa mlipuko mwingine wa aina hiyo baada ya bomu kurushwa sebuleni kwa Sheikh Sudi Ally Sudi usiku wa Alhamisi wiki iliyopita na kumjeruhi yeye pamoja na mgeni wake. Kuhusu tukio hilo tulishawakamata washukiwa sita,” alisema
Alieleza kwamba wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kubwa na kutilia mashaka kila nyendo za watu wanaokutana nao au wanapokuwa wamekaa katika maeneo ya mapumziko au mikusanyiko.
Alisema wamebaini kwamba wahusika wana mtandao mpana ambao upo nchi nzima na wanaendelea kuuchunguza ili kuumaliza na kuepusha madhara zaidi kwa wananchi.
“Watu wawe makini dhidi ya kila mtu aliye kando yake. Hili ni suala muhimu zaidi katika kujizatiti na kujiepusha na maafa, na wanapobaini au kuhisi mtu asiye mwema wachukue hatua za haraka kuwakwepa na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama,” alisema.
Miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa yakitikiswa na milipuko ya mabomu ni Zanzibar, hatua ambayo inatoa ishara za kuwapo kwa mkakati maalumu wa kuvuruga amani katika miji inayoongoza kwa utalii nchini.
Alieleza kwamba hadi sasa wameshakamata watu wasiopungua 25 wanaohusishwa na milipuko yote iliyotokea Zanzibar na Arusha, huku akieleza kwamba hakuna kikundi kinachoweza kuhusishwa moja kwa moja na milipuko hiyo.

No comments: