Mojawapo ya hatua ya kwanza atakayochukua ni kuyagawa mashamba hayo kwa wananchi wa maeneo husika ili yaendelezwe kwa kilimo.
Kauli ya Rais Kikwete ilitokana na malalamiko yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Dastan Kitandula, aliyemuomba Rais kutoa kauli juu ya tatizo la kutelekezwa kwa mashamba ya mkonge na kugeuka vichaka huku wananchi wa wilaya hiyo wakikumbwa na uhaba wa ardhi ya kilimo.
Kitandula alimueleza Rais kuwa kutokana na hali hiyo, wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakipata tabu kubwa sana hasa nyakati wanapokuwa wakitafuta maeneo ya ardhi kwa ajili ya kilimo hali inayosababisha kugeuka maskini.
Alisema tatizo la ardhi katika jimbo hili limekuwa sugu kutokana na mashamba ya mkonge yaliyotelekezwa kwa kipindi cha miaka saba na kusisitiza maeneo mengi yamekumbwa na tatizo hilo ikiwamo maeneo ya Muhinduro na Maramba.
“Mheshimiwa Rais tunaomba utoe uamuzi wa haki ili wananchi wanaoishi kwenye mashamba ya mkonge wilayani hapa ikiwamo Mhinduro na Maramba wapate ardhi, lengo likiwa kunufaika na kilimo,” alisema Kitandula.
Mbunge huyo pia alimweleza Rais changamoto nyingine wanayokumbana nayo wananchi ni pamoja na huduma za Afya huku akisisitiza ahadi ya Serikali ya kuwapatia hospitali ya wilaya kutotekelezwa na wananchi kulazimika kutumia vituo vya afya na zahanati kupata huduma za afya.
Alimueleza Rais Kikwete kuwa katika bajeti ya mwaka uliopita kwenye sekta ya afya wilayani humo, walitengewa Sh milioni 500 kwa ajili ya kuendesha sekta hiyo lakini wakashangaa kupewa Sh milioni 50 tu bila ya kupewa maelezo.
Akijibu malalamiko hayo, Rais Kikwete aliahidi kulifanyika kazi suala hilo na kulipatia ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kukaa na wizara husika.
Wakati huo huo, Rais Kikwete alisema Serikali ipo kwenye mikakati ya kukiongezea nguvu kituo cha afya Mkinga wakati wakiendelea na harakati za kujenga hospitali ya wilaya hiyo ili kuondoa changamoto kukosekana huduma bora za afya kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment