Tuesday, 29 July 2014

Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba (IMTU) wafunguliwa kesi ya Viungo vya binadamu

Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba cha IMTU wakiwa mahakamaniWAHADHIRI wanne wa Chuo Kikuu cha Tiba cha IMTU, Mbezi Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na makosa mawili, likiwemo la kushindwa kufukia viroba 83 vya viungo vya binadamu.
Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Polisi, Magoma Mtani, mbele ya Hakimu Kwey Rusemwa, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Venkat Subbaiah (57), Appm Shankar Rao (64), Prabhakar Rai (69) na Dinesh Kumar (27).
Magoma alidai kuwa washitakiwa hao Julai 2014 katika eneo la Mpigi Majohe, walishindwa kufukia viroba 83 vya viungo vya binadamu walivyovitumia kufundishia wanafunzi wa udaktari kinyume na kifungu cha 128 cha sheria ya kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.
Alidai kuwa washitakiwa hao kwa pamoja, pia walishindwa kuandaa hati kwa Kampuni ya Corona ya kuthibitisha kufukiwa kwa mabaki hayo.
Washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na upande wa jamhuri ukadai upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Rusema, alisema ili washitakiwa wapate dhamana, kila mmoja awe wadhamini wawili ambao ni Watanzania na wanaofanya kazi kutoka kwenye taasisi zinazotambulika kisheria.
Wakati taratibu hizo zikiendelea, Wakili wa Serikali, Salum Ahmed aliingia mahakamani hapo na kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002 kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo, Hakimu Rusemwa aliwaachia huru washitakiwa hao, lakini muda mfupi baadaye walikamatwa na askari wa Jeshi la Polisi na kuwekwa chini ya ulinzi mkali na kupandishwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili KXO 6 EFY na Toyota RV4
yenye namba za usajili T 366 AVG na kuondoshwa katika eneo la mahakama.

No comments: