“Ni kweli nilishiriki kwenye maziko kwa sababu mimi kama Balozi wa Tanzania wakati huo ndiye nilikuwa mwakilishi wa Serikali pale Washington, lakini jambo la pili ni kwamba binafsi nilimfahamu Ballali kwa muda mrefu, kwa hiyo hata kama nisingekuwa balozi lazima ningekwenda kuzika tu.” Balozi Ombeni Sefue.
Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania BOT), Marehemu Daudi Ballali aliacha wasia unaotaka maiti yake isionyeshwe hadharani atakapofariki dunia na wala maiti yake isiletwe Tanzania kwa ajili ya maziko.
Ballali aliyefariki Mei 16, 2008 na kuzikwa Mei 23
mwaka huohuo katika makaburi ya Gate of Heaven, eneo la Silver Spring,
Maryland nchini Marekani alifahamu kuhusu kifo chake wiki mbili kabla,
baada ya matibabu kushindikana.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa nchini Marekani
kwa siku kumi kufuatilia suala hilo, alibaini kuwa kiongozi huyo
alilazwa mara ya pili katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha George
Washington, April 2008 na alirejea nyumbani kwake, Washington DC wiki
mbili kabla ya kukutwa na mauti.
Habari kutoka ndani ya familia yake zinasema baada
ya madaktari kushindwa kumtibu walimwambia kwamba asingeweza kuishi kwa
zaidi ya wiki mbili, hivyo walimshauri ahamie kwenye ‘hospice’ ambayo
ni nyumba maalumu ya kusubiri kifo kwa watu ambao magonjwa yao
yameshindikana.
Hospice hutumika kwa ajili ya kuwaweka wagonjwa
wanaohitaji faraja hasa kutoka na maumivu makali chini ya uangalizi wa
washauri na wauguzi kwa lengo la kuwaongezea wagonjwa husika siku za
kuishi.
Baadhi ya hospice hutoa huduma za kiroho, kijamii
na kifedha na wakati mwingine huduma hizo hutolewa kwa wagonjwa ambao
wanaugulia nyumbani. Hata hivyo, gazeti hili lilidokezwa kwamba Ballali
alikataa kwenda kwenye nyumba hiyo na badala yake kutaka apelekwe
nyumbani kwake.
“Alikataa kwenda kwenye hospice, aliwaambia
madaktari kwamba yeye hawezi kwenda huko ijapokuwa kuna huduma nzuri na
uangalizi wa nesi (muuguzi). Aliwaambia kwamba nitakwenda kufia nyumbani
kwangu maana nina nyumbani kwangu,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Aliporejeshwa nyumbani, alikuwa anazungumza kama
kawaida lakini kadri siku zilivyosogea hali ilikuwa ikibadilika na kama
sikosei siku mbili au tatu za mwisho (za uhai wake) alikuwa anajitambua
lakini alikata kauli, hakuwa akizungumza chochote”.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa katika siku hizo za
mwisho za uhai wake, Ballali aliacha maelekezo kwamba pindi
atakapofariki dunia, mwili wake usiwekwe hadharani kwa maana ya
kutazamwa na watu nje ya familia wala kusafirishwa kuja Tanzania kwa
ajili ya maziko.
“He said, he doesn’t like to be turned into a
laughing staff (alisema asingependa kugeuzwa kichekesho), sababu watu
wasingekuja kutoa heshima za mwisho, bali wangekuja kumdhihaki kuangalia
Ballali aliyetuhumiwa kwa ufisadi wa EPA na siyo Gavana,” kilisema
chanzo hicho.
Kifo, mazishi yake
Habari kutoka ndani ya familia yake zinasema Ballali alifariki
Mei 16, 2008 saa 8:00 mchana saa za Marekani, sawa na saa 03:00 za
Tanzania akiwa nyumbani kwake, Maryland.
Baada ya kifo chake, mwili wake ulihifadhiwa
kwenye nyumba ya maiti iitwayo Vol Funeral Home iliyopo Washington DC
kwa siku nne na siku ya tano Mei 23 uliondolewa na kupelekwa Kanisani
kwa ajili ya Ibada kisha kupelekwa makaburini kwa ajili ya maziko.
Siku hiyo ya Mei 23 saa nne asubuhi, familia ya
Ballali ikiongozwa na mjane wake Anna Muganda pamoja na watoto wake
wawili, mtalaka wake na wanafamilia wengine, walikwenda Vol Funeral Home
ambako walitoa heshima za mwisho kwa marehemu.
“Katika tukio hilo familia ilikubaliana kwamba
matakwa ya marehemu yaheshimiwe, kwa hiyo hakuna aliyeruhusiwa kupiga
picha zozote. Kwa hiyo ni ndugu tu wa familia walioruhusiwa kuona mwili
wa Ballali, baadaye tulifunga casket (jeneza) na tukaondoka kwenda
Kanisani,”kilisema chanzo chetu nchini Marekani.
Kauli hiyo inaungwa mkono na maelezo yaliyotolewa
kwa gazeti hili Agosti 25, 2013 na dada wa Marehemu Ballali, Margaret
Mpango kwamba shughuli za kuaga mwili wa marehemu, ibada na baadaye
maziko vilikuwa ni kwa ajili ya familia pekee.
Akizungumza na Mwandishi wa Mwananchi, nyumbani
kwake mjini Kigoma, Margaret Mpango aliweka bayana kwamba: “Familia
isingeweza kuruhusu watu wengine kushiriki, haikuwa na maana yoyote
kwani tayari kulikuwa na maneno mengi yanayomhusu”.
Dada huyo anayezaliwa tumbo moja na Marehemu
Ballali ni mke wa Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania,
Dayosisi ya Kasulu, Kigoma, Dk. Gerald Mpango ambaye alikuwa miongoni
mwa walioongoza Ibada ya maziko ya Ballali.
Margaret alilithibitishia gazeti hili kwamba
mumewe (Dk. Mpango), alishirikiana na mapadre wa Kanisa la Mtakatifu
Stephen, Washington D.C. kuongoza ibada ya mwisho ya Ballali ambaye siku
hiyohiyo alizikwa katika makaburi yanayomilikiwa na Kanisa Katoliki ya
Gate of Heaven.
Alisema miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo ni
aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani wakati huo, Balozi Ombeni
Sefue, ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi.
Kauli ya Sefue
Jana Balozi Sefue akizungumza na Mwandishi wa
Mwananchi, alithibitisha kwamba kweli alishiriki kwenye Ibada ya kumuaga
Ballali na baadaye kwenye maziko ya Gavana huyo katika makaburi ya Gate
of Heaven
“Ni kweli nilishiriki kwenye maziko kwa sababu mimi kama Balozi
wa Tanzania wakati huo ndiye nilikuwa mwakilishi wa Serikali pale
Washington, lakini jambo la pili ni kwamba binafsi nilimfahamu Ballali
kwa muda mrefu, kwa hiyo hata kama nisingekuwa balozi lazima ningekwenda
kuzika tu,” alisema Balozi huyo.
Picha zake zasakwa
Taarifa zaidi ambazo gazeti hili lilizipata
Washington DC, zinasema kulikuwa na jitihada za kutaka kupiga picha
mwili wa marehemu wakati wa kutoa heshima za mwisho, lakini zilikwama
baada ya ndugu wa marehemu kuzima jaribio hilo.
“Mmoja wa waliokuwapo kwenye msiba baada sisi
kumaliza kutoa heshima za mwisho alitaka kupiga picha kwa madai kwamba
anataka kubaki na sura ya ndugu yetu, lakini tulikataa na kumwambia
kwamba tulishakubaliana kutofanya hivyo kwa heshima ya marehemu,”
kilieleza chanzo chetu na kuongeza:
“Baadaye tulipata taarifa kwamba wapo watu tena
kutoka Tanzania ambao walikuwa wakihitaji picha hiyo kwa udi na uvumba
na walikuwa wameahidi kuinunua kwa Dola za Marekani 35,000”. Kiasi hicho
ni sawa na Sh57.7 milioni kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha
ambavyo ni wastani wa Sh1650 kwa dola moja.
Safari ya Marekani
Safari ya Mwandishi wa Mwananchi nchini Marekani
ilianza Alhamisi Juni 26, 2014 hadi Jumapili, Julai 6. Mwandishi wa
habari hizi aliligundua kaburi hilo baada ya kwenda makaburi ya Gate of
Heaven kwa siku tatu mfululizo.
Siku ya kwanza, mwenyeji wa mwandishi ambaye jina
lake tunalihifadhi kwa sasa alimfikisha katika makaburi hayo, lakini
kaburi la Ballali halikuonekana na hata mwandishi alipokwenda siku ya
pili peke yake, kaburi hilo pia halikuonekana kwa kutokana na ukubwa wa
eneo hilo.
Siku ya tatu, Mwandishi wa Mwananchi alilazimika
kuomba msaada wa Ofisi ya Makaburi ya Gate of Heaven, ambayo ilimsaidia
kuonyesha eneo lilipo kaburi hilo, hivyo kuwezesha kupata picha zake.
Kaburi lake liko katika msitari wa mwisho kabisa
na Ukanda wa Kijani wa miti iliyozunguka makaburi ya Gate of Heaven,
likiwa limeandikwa jina la kiongozi huyo, pamoja na maneno ya Kiingereza
yanayosomeka “When the heart weep for what it has lost, the soul
rejoices for what it has found”.Maana ya maneno hayo ni kwamba, “Wakati moyo ukiomboleza kwa kile
kilichopotea, roho hufurahi kwa kile kilichopatikana”. Kaburi hili
limezungukwa na makaburi mengine kadhaa ambayo si ya Watanzania, kwani
kwa haraka kutokana na mazingira yalivyokuwa, Mwandishi wa Mwananchi
hakuweza kuona kaburi jingine lenye majina yenye asili au kuwa na
mwelekeo wa asili ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment