Saturday 19 July 2014

Kocha wa Simba mbioni kutimuliwa

Kocha wa Simba
TAARIFA za chini ya kapeti ambazo mtandao huu umezipa kutoka chanzo cha uhakika, uongozi wa klabu ya Simba chini ya rais, Evans Aveva umedhamiria kumtimua kocha mkuu wa klabu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic.  Sababu kubwa iliyoelezwa na chanzo hicho makini ni kuwa Loga amekuwa akiwasumbua viongozi wa klabu hiyo kwa kukataa wachezaji wanaoletwa na viongozi kwa ajili ya kusajiliwa.  Simba wapo katika harakati za kuimarisha kikosi chao, lakini Loga amekuwa akiwapiga chini wachezaji wanaoletwa na viongozi kwa madai kuwa hawana viwango vizuri.  Hata hivyo mtandao huu umepenya ndani na kujua kuwa Loga amekuwa na msimamo mkali kwa viongozi hao akihitaji kuchagua mwenyewe wachezaji.  Kwa siku nyingi, kundi maarufu katika klabu ya Simba, Friends of Simba (F.O.S) linaloundwa na mamilionea, limekuwa likishutumiwa kuwapangia makocha wachezaji wa kusajiliwa na kupangwa kucheza katika mechi.  Aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo  kabla ya kuja kwa Mfaransa Patrick Liewig, Mserbia, Milovan Circovic aliwahi kulalamika kuwa viongozi wa wakati ule walioongozwa na mwenyekiti Ismail Aden Rage na makamu mwenyekiti, Geofrey Nyange `Kaburu` walikuwa wanaingilia upangaji wa kikosi chake.  Milovan alieleza kuwa viongozi ambao ni wanachama wa kundi la F.O.S walikuwa wanampangia wachezaji wa kucheza kinyume na taratibu za ualimu.  Kukosa uhuru kwa makocha katika upangaji wa kikosi, ni kinyume na mpira wa kisasa unaomtaka kocha kuwa mwamuzi wa mwisho kujua nani anacheza na nani hatacheza.  Mbali na kuwapangia makocha wachezaji wa kucheza, pia kundi hili limekuwa likiingilia mchakato wa usajili na kuleta wachezaji wasiokuwepo kwenye mipango ya kocha.  Kitaalamu, kocha ndiye mwenye mamlaka ya kuamua mchezaji gani asajiliwe na nani aachwe. Lakini kwa klabu mbili za Simba na Yanga, kuna baadhi ya wachezaji wanaletwa na viongozi na sio matakwa ya benchi la ufundi.  Kwa taarifa za uhakika, Simba wapo katika mazungumzo na kocha wa Gor Mahia ya Kenya, Bobby Williamson.  Kabla ya kuja kwa Loga, Williamson alikuwa katika rada za Simba baada ya kuacha kazi ya kuifundisha timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes.  Mtandao huu unafuatilia kwa kina suala hilo ili kujua nini hatima yake.

No comments: