Machafuko nchini Libya si tu kwamba yamekuwa ni kitu cha kila
siku, bali kadiri muda unavyopita, ndivyo machafuko hayo
yanavyoongezeka. Habari zinasema kuwa, mapigano yanaendelea kwa siku
kadhaa sasa karibu na Uwanja wa Ndege wa Tripoli na hii ni katika hali
ambayo mji wa Benghazi nao unaendelea kushuhudia mauaji dhidi ya
wanasiasa, maafisa wa kijeshi na raia wa kigeni. Tukio la karibuni
kabisa huko Benghazi ni kuchinjwa na kukatwa kichwa kibarua mmoja raia
wa Ufilipino. Habari nyingine zinasema kuwa, wawakilishi wawili kutoka
miji ya Benghazi na Janzur katika Congress ya Taifa ya Libya (Bunge)
wametekwa nyara na watu wenye silaha. Mauaji dhidi ya maafisa wa kijeshi
wa Libya nayo yanaendelea mashariki mwa nchi hiyo. Hivi sasa hali ya
Libya ni mbaya sana; na jambo hilo linaonekana katika miundo yote ya
kisiasa, kiuchumi ya kijamii ya nchi hiyo. Katika upande wa kisiasa na
licha ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi na kujulikana muundo wa Bunge la
nchi hiyo, lakini hadi hivi sasa zoezi la kukabidhi madaraka kutoka
Congress ya Taifa kwenda kwa bunge jipya halijafanyika. Sababu yake ni
kuwa hali ya Libya haiiruhusu nchi hiyo kutangaza siku ya kufanyika
kikao cha kwanza cha bunge hilo jipya. Katika upande wa masuala ya
kijamii pia ni kwamba, hakuna umoja na mshikamano wowote wa kitaifa
nchini Libya. Kila sehemu nchini humo imo mikononi mwa kabila au pote
fulani la watu na kwamba ni viongozi wa kikabila ndio wanaoongoza baadhi
ya maeneo ya Libya. Mfano wa wazi ni maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo
ambayo yamejitangazia utawala wa ndani na kadiri siku zinavyopita ndivyo
maeneo hayo yanavyozidi kutoka mikononi mwa serikali kuu kiasi kwamba
maeneo hayo hata yameanza kuchimba mafuta bila ya idhini ya serikali ya
Tripoli. Katika upande wa kiuchumi pia, maeneo mengi ya mafuta yako
mikononi mwa viongozi wa kikabila. Jambo hilo limeathiri vibaya sekta ya
usafirishaji nje mafuta nchini Libya na kupunguza mno pate la serikali
kuu. Hali hiyo kusema kweli inaufanya mustakbali wa Libya kukumbwa na
giza nene. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, si jambo lililo
mbali kuiona Libya ikigawika vipande vipande. Hali ilivyo Libya
inaonesha wazi kuwa, machafuko ya nchi hiyo yanachochewa na mikono ya
nje. Wanaochochea machafuko hayo ni yale madola ambayo kwa muda mrefu
yalikuwa yanaukodolea macho ya tamaa utajiri mkubwa wa mafuta na gesi wa
nchi hiyo. Tunathubutu kusema kuwa, hali ya hivi sasa ya Libya ni
jinamizi kwa wananchi wa nchi hiyo, lakini wakati huo huo ni ndoto nzuri
ya usingizi mnono kwa dola la Marekani na madola mengine ya Magharibi.
No comments:
Post a Comment