Kwa muda mrefu sasa wapenzi, mashabiki na wadau wa soka wamekuwa
wakisema umefika wakati wa kuondoka katika soka la ridhaa na kuingia
soka la kulipwa.
Kauli hii ya kuondoka katika soka la ridhaa na
kuingia soka la kulipwa imesemwa sana, lakini uongozi wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) umeshindwa kuifanyia kazi.
Allan Goshashi |
kwa sababu sera ya maendeleo ya michezo ya Tanzania inasema vyama vya michezo vimo katika makundi matatu makubwa ambayo ni (a) vyama vya ridhaa vilivyosajiliwa na msajili wa vyama vya michezo na kujishirikisha na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), (b) Mashirikisho ya michezo ambayo yameundwa na taasisi mbalimbali ili kutoa burudani za kimichezo kwa wafanyakazi, kuwakutanisha wachezaji wao ili wafahamiane, pia kuwashindanisha katika michezo inayohusika na kupata mabingwa wao katika ngazi ya taifa, (c) Vyama vya michezo ya kulipwa ambavyo vimesajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Mwaka jana TFF ilifanya mabadiliko ya katiba yake
na baada ya hapo iliipeleka BMT ili mabadiliko hayo yapate baraka za BMT
hali iliyoonyesha TFF ni chama cha ridhaa kilichosajiliwa na msajili wa
vyama vya michezo ya ridhaa.
Chama cha mchezo wa kulipwa nchini ni Kamisheni ya
Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) ambacho kimesajiliwa Wizara ya Mambo
ya Ndani.
Vipo vyama vingine vya ngumi ambavyo vimeingia
zaidi kwenye biashara ya ngumi za kulipwa na vimesajiliwa kama makampuni
kwa msajili wa makampuni katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Vyama
hivyo ni TPBO na PST.
TFF ina wanachama, kushindwa kwake kujisajili kama
chama cha mchezo wa kulipwa ndiyo kunaposababisha hata wanachama wake
kushindwa kuingia kwenye soka la kulipwa.
Wanachama wa TFF ni pamoja na klabu zote 14
zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Nakumbuka kuna wakati katika
klabu ya Yanga kulikuwa na wanachama wa klabu hiyo waliojulikana kwa
jina la Yanga Kampuni waliokuwa wakitaka iendeshwe kama kampuni na
wengine waliokuwa wakitaka iendelee kuendeshwa kiridhaa (Yanga-asili).
Wale waliokuwa wakitaka Yanga iendeshwe kama
kampuni walishindwa kufikia lengo lao na hata leo wakitaka Yanga
iendeshwe kama kampuni watashindwa kwa sababu Yanga ni wanachama wa TFF
ambayo imesajiliwa BMT kama chama cha mchezo wa ridhaa.
Ndiyo, tunaweza kuona baadhi ya klabu zinasajili
wachezaji kadhaa kwa kuwalipa mamilioni, mishahara mikubwa, kuwapa posho
na kuwapangia nyumba, lakini ukweli utabaki bado hatuna soka la
kulipwa.
Soka la kulipwa halihitaji wachezaji wachache tu
walipwe vizuri, soka la kulipwa ni biashara kubwa katika kuiwezesha
klabu husika kutengeneza biashara na vitega uchumi mbalimbali kwa ajili
ya kujiendesha kwa ufanisi kisoka na kiuchumi.
Soka la kulipwa ni biashara, klabu zinatakiwa
kuuza hisa ili kupata mitaji ya kuanzisha vitega uchumi, pia klabu
zinatakiwa kuuza bidhaa zitakazokuwa na nembo ya klabu kama vile kofia,
jezi, fulana na vitu vingine vingi kulingana na ubunifu wa klabu husika.
Klabu inapojiendesha kibishara ina maana inaweza kuchukua mkopo
benki kama mtaji wa kuanzisha au kuendeleza miradi yake, lakini kwa
mfumo huu wa soka kuendeshwa kiridhaa klabu zetu haziwezi kufanya hivyo.
Ni wazi bado tuna safari ndefu ya kuwa na soka la
kulipwa kwani pia ni klabu chache ambazo angalau zinaonekana zinaweza
kukidhi kigezo cha kuingia katika soka la kulipwa.
Lakini hata hivyo TFF kuendelea kusajiliwa BMT
kama chama cha mchezo wa ridhaa kunafanya safari ya kupata kweli soka la
kulipwa kuwa ndefu na ndiyo maana naona hatuna soka la kulipwa.
No comments:
Post a Comment