Saturday, 26 July 2014

Jeshi la kanda wajiandaa kupambana na Boko Haram

Mataifa manne ya Afrika Magharibi yameazimia kuunda kikosi cha pamoja ili kukabiliana na kitisho kinachoongezeka cha kundi la itakadi kali za Kiislamu la Boko Haram, linaloendesha shughuli zake hasa nchini Nigeria.
Kila moja ya mataifa hayo ya Nigeria, Niger, Chad na Cameroon, litachangia wanajeshi 700 kwenye kikosi kinachonuwiwa kuboresha mapambano ya kanda hiyo dhidi ya wapiganaji hao.
Mataifa hayo manne yanayopakana na ziwa Chad, eneo ambalo ni ngome ya Boko Haram, tayari yanabadilisha taarifa za kijasusi na yanaratibu kwa pamoja usalama wa mpakani katika eneo, lakini kuunda kikosi cha pamoja chenye ukubwa huu itakuwa hatua kubwa zaidi katika ushirikiano wao.
Tangazo la kuundwa kikosi hicho lilitolewa wakati wa mkutano wa mamawziri wa ulinzi kutoka mataifa hayo manne, lakini hakukuwa na taarifa zaidi juu ya muda au eneo vitakakopelekwa vikosi hivyo. Wapiganaji wa Boko Haram wameua maelfu ya watu tangu mwaka 2009, walipoanzisha juhudi zao za kuunda taifa la Kiislamu nchini Nigeria.

Raia zaidi wateketezwa
Matukio ya uripuaji mabomu na mashambulizi mengine yamekuwa jambo la kawaida kaskazini mwa Nigeria, lakini Boko Haram ilianza kupamba vichwa vya habari kimataifa miezi iliyopita, baada ya kuwateka wanafunzi zaidi ya 200 kutoka shule mjini Chibok. Utekaji huu ulipelekea kutolewa miito ya kuchukuliwa hatua, na ahadi kutoka kwa marais wa kanda hiyo kuanzisha vita kamili dhidi ya wapiganaji hao.
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau.
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau.
Niger na Cameron zimeimarisha hasa usalama katika maeneo ya mipakani, lakini hakukuwa na ishara zozote za mashambulizi makubwa yanayovihusisha vikosi vya kanda. Shirika la kutetea haki za binaadamu la Huma Rights Watch lilikadiria wiki iliyopita kuwa wapiganaji hao wameuwa zaidi ya raia 2000 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.
Jana Jumatano, miripuko miwili katika mji wa kaduna, ambayo iliwalenga mhadhiri maarufu wa dini ya Kiislamu na rais wa zamani wa Nigeria, ilisababisha vifo vya watu wasiopungua 42 katika vurugu za hivi karibuni zinazolaumiwa kwa kundi la Boko Haram.
.
Gavana Kaduna ahofia jimbo lake
Maandamano ya kutaka kurejeshwa kwa wasicha wa shule.
Maandamano ya kutaka kurejeshwa kwa wasicha wa shule
Polisi ilisema shambulio la kwanza lilifanywa na mripuaji wa kujitoa muhanga akiulenga msafara wa Sheikh Dahiru Bauchi, kiongozi wa dini ambaye ameukosoa vibaya uasi wa miaka mitano wa Boko Haram.
Shambulio lingine lililotokea saa mbili baadaye na kuuwa watu 17 lilimlenga Muammadu Buhari, moja wa wapinzani maarufu nchini Nigeria, ambaye pia aliiongoza Nigeria kama dikteta wa kijeshi kuanzia mwaka 1983 hadi 1985.
Gavana wa jimbo la Kaduna Mukhtar Ramalan Yero alitangaza amri ya saa 24 ya kutotembea usiku, na msemaji wake alieleza wasiwasi wa gavana huyo, juu ya kuripuka kwa machafuko katika mji huo maarufu kwa mapigano ya kidini katika miaka ya karibuni, kwa sababu walengwa wote wa mashambulizi hayo, Bauchi na Buhari, wanashikilia nyadhifa muhimu machoni mwa watu.

No comments: