Thursday, 24 July 2014

Jose akiri chelsea ni moto wa kuotea Mbali msimu huu

Mourinho ametumia pauni 80 milioni kwa usajili wa wachezaji watatu msimu huu.

Velden, Austria. Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho anaamini kuwa timu yake itakuwa moto wa kuotea mbali kwa miaka 10 ijayo katika Ligi Kuu England, baada ya kuwasajili Cesc Fabregas, Diego Costa na Filipe Luis.

Mourinho ametumia Pauni 80 milioni kusajili wachezaji hao kutoka Ligi Kuu ya Hispania (La Liga). Fabregas hakuwa na nafasi Barcelona wakati Filipe Luis na Diego Costa waliiongoza Atletico Madrid kutwaa taji la ligi hiyo msimu uliopita.

“Timu ambayo imekuwa ikishinda kwa misimu 10 inabadilika hatua kwa hatua. Tumenunua wachezaji wapya na tunajaribu kuisuka kwa miaka 10 ijayo,” alisema Mourinho katika hoteli waliyofikia Chelsea mjini Velden, Austria jana.

“Msimu uliopita tuliishia nusu fainali, na ulikuwa msimu wa ajabu,” aliongeza. “Tulikuwa na timu ya vijana wengi wakati ule. Lakini hata sasa, tutacheza kwa ajili ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa.

“Msimu ambao tunadhani tutakuwa na kikosi kizuri, ndio vijana watakapokuwa wakipata uzoefu zaidi. Wako katika hali nzuri ya kuweza kutwaa mataji.”

Licha ya kuwepo kwa ushindani wa timu kubwa za England, kocha huyo wa Blues mwenye miaka 51, alisema asingeweza kuwepo Stamford Bridge kama hawezi kufikiria kuwa Chelsea inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao.

“Kama sitafikiria hilo, nitalazimika kwenda nyumbani na kumuacha mtu mwingine kuendelea na majukumu yangu kama kocha.

“Watu wanaweza kuzungumza kuhusu ligi, lakini England ndio nchi pekee ambayo timu zake tano au sita zinazoweza kutwaa ubingwa. Soka ni ushindani wa kila mwishoni mwa wiki, na hilo pekee linatokea England.

“Unapokuwa na timu mbili za Manchester, tatu kutoka London – Tottenham, Arsenal na sisi, ikiiongezeka Liverpool, hizo ni timu kubwa sita, ambazo zote zinaweza kupambana kuwania ubingwa. Na hii ndio sababu kila mmoja anaipenda Ligi Kuu ya England.”

No comments: