MAMLAKA ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Mkoa wa
Kilimanjaro, imewaomba wananchi kutoa taarifa kwa askari wa usalama
barabarani pale wanapopanda daladala ambazo madereva wake hawazingatii
sheria zilizowekwa ikiwamo kutovaa sare.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Ofisa Mfawidhi Kanda
ya Kaskazini, Fabian Nyang’oro, alisema kati ya mikakati waliyojiwekea
mkoani hapa ni pamoja na kufanya ukaguzi kwa magari yote yanayobeba
abiria ili kubaini kama yanatekeleza taratibu zilizowekwa na mamlaka
hiyo.
Alisema mikakati hiyo itaweza kufanikiwa endapo walengwa watazingatia
maagizo hayo, huku akiwaomba wananchi mkoani hapa kushirikiana na
mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa kwa askari wa usalama barabarani pindi
wanapopanda magari ambayo ni mabovu.
“Mikakati tuliyojiwekea kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 ni pamoja na
kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani,
dereva na kondakta atakayekutwa hayuko nadhifu, hajavaa sare na breki
za gari lake hazina raba, atanyang’anywa leseni yake na gari kuzuiwa
kufanya kazi,” alisema.
No comments:
Post a Comment