Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema utawala haramu
wa Israel umeua idadi kubwa ya watoto na kubomoa mahospitali katika
mashambulizi yake ya kinyama yanayoendelea katika Ukanda wa Ghaza. Mfuko
wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imetoa taarifa hiyo na kuongeza
kuwa, baada ya kupita wiki mbili za mashambulizi ya Israel huko Ghaza,
asilimia 33 ya waliouawa shahidi katika mashambulizi hayo ni watoto.
Msemaji wa UNICEF Christopher Tidey amesema, kwa ujumla hadi sasa Israel
imeshaua watoto 121 wa Kipalestina katika Ukanda wa Ghaza na kwamba
watoto waliojeruhiwa ni zaidi ya 904. Jumla ya Wapalestina waliouawa
shahidi katika mashambulizi ya Israel huko Ghaza ni zaidi ya 610 huku
wengine wasiopungua 3,600 wakijeruhiwa. Aghlabu ya wahanga wa
mashambulizi hayo ya Israel ni raia wasio na hatia wakiwemo wanawake na
watoto. Wakati huo huo, vituo vya afya vipatavyo 18 vimeharibiwa Ghaza,
huku wahudumu 20 wa afya wakijeruhiwa wakati mashambulizi ya Israel
dhidi ya Wapalestina yakiendelea. Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema
kuwa limesikitishwa mno na kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya vituo
vya afya katika hujuma za utawala haramu wa Israel dhidi ya Ghaza. WHO
imesema wahudumu wa afya ni lazima walindwe wakati wote, na kuruhusiwa
kufanya kazi zao. Fadella Chaib kutoka WHO amesema kuwa, idadi kubwa ya
majeruhi imezidi uwezo wa vituo vya afya ambavyo awali vilikuwa vikitoa
huduma kwa hali ya kawaida. Katika hujuma yake Ghaza, Utawala wa
Kizayuni wa Israel mbali na kuwaua watoto na kubomoa mahospitali pia
unatumia silaha za maangamizi ya umati zilizopigwa marufuku duniani.
Vitendo hivyo vyote vya Israel ni kinyume cha sheria za kimatiafa na ni
jinai za vita lakini madola ya Magharibi yanayoongozwa na Marekani si tu
kuwa hayalaani jinai hizo bali yanaunga mkono Israel na kuipa kinga
isichukuliwe hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment