Wednesday, 16 July 2014

Chadema yajiandaa kuchukua dola


Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeweka bayana mkakati wake mpya wa kushika dola kwa kukita mizizi yake tangu ngazi ya shina hadi ya Taifa.
Mkakati huo, ambao Chadema ilisema unalenga kukiondoa chama hicho kutoka kwenye uanaharakati na kukifanya kuwa chama cha dola, umekuja wakati nchi ikijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka ujao.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema chama hicho tayari kimeunda matawi 196,000 kati ya 250,000 yanayokusudiwa.
“Chadema imeshajiondoa kwenye harakati na kwenda kuwa chama dola. Tumefanya harakati kwa zaidi ya miaka 20 tukiwa na lengo la kukipeleka chama kwa wananchi, ili wakielewe na wakiheshimu, lakini sasa umefika wakati wa kujiandaa kushika dola,” alisema Dk Slaa.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Chadema ilishika nafasi ya pili kwa kuingiza wabunge wengi huku mgombea wake wa urais akishika nafasi ya pili nyuma ya Rais Kikwete, ambaye ushindi wake ulipungua kutoka zaidi ya asilimia 80 hadi asilimia 61.
Mkakati wa chama
Dk Slaa alisema chama hicho kikuu cha upinzani kwa sasa kinafanya kazi katika kanda 10, nane zikiwa Bara na mbili Zanzibar na kanda hizo zimepewa mamlaka hadi ngazi ya chini (msingi).
“Baada ya kuunda kanda hizo 10 kumekuwa na mafanikio makubwa ambayo ni pamoja na kuunda misingi au mashina. Leo tuna mabalozi wa nyumba 10 nchi nzima. Mwanachama wetu akipata shida, hana haja ya kwenda kusuluhishwa na balozi wa CCM,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Katika ngazi ya vitongoji tuna matawi au shehia kule Zanzibar. Lengo letu lilikuwa ni matawi 250,000 hadi sasa tuna matawi 196,000.”
Dk Slaa alisema kuwa chama hicho kiliahirisha uchaguzi mkuu mara tatu ili kukijenga kwanza katika ngazi za chini ikiwa pamoja na kufanya chaguzi katika ngazi hizo.
Akizungumzia uchaguzi wa ngazi ya majimbo, Dk Slaa alisema ulishaanza tangu Machi 26, mwaka huu na baadhi ya wilaya zimeshakamilisha.
Aliongeza kuwa baada ya uchaguzi wa majimbo, utafuata uchaguzi wa wilaya kuanzia Julai 18 hadi 22 utakaofuatiwa na rufaa kwa wasioridhika na matokeo.

“Agosti 22-26 mwaka huu kutakuwa na maandalizi ya mkutano mkuu utakaoanza Agosti 27. Agosti 28 utakuwa uchaguzi wa Baraza la Vijana (Bavicha) na Baraza la Wazee kwa nafasi zote na Baraza la Wanawake,” alisema na kuongeza:
“Agosti 29 Kamati Kuu iliyopo itakutana ikijumuisha viongozi waliochaguliwa kwenye mabaraza. Agosti 30 kutakuwa na Baraza Kuu jipya na Agosti 31 utakuwa mkutano mkuu utakaochagua mwenyekiti wa Taifa na makamu wa Bara na Zanzibar na katibu atapendekezwa na Baraza Kuu. Lengo la Chadema kwa sasa ni kushika dola tu,” alisisitiza.
Mgombea urais
Akizungumzia suala la chama hicho kumteua mgombea uraia kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Dk Slaa alisema katiba ya Chadema ndiyo itaamua na si wanachama kuanza kutangaza nia zao kama ilivyo kwa CCM.
“Sisi kazi yetu ni kuitetea katiba ya chama, ilivyosema ndivyo tutakavyotekeleza. Kwa sasa tunajipanga kuanzia ngazi ya chini. Mambo ya kutangaza nia ni ya CCM,” alisema.
Kwa mujibu wa ibara ya 7 ya katiba ya Chadema, moja ya kazi za Kamati Kuu ni kufanya utafiti wa wagombea urais na mgombea mwenza na kuwasilisha ripoti zake kwa Baraza Kuu kwa ajili ya mapendekezo yake kwa Mkutano Mkuu ambao hufanya uteuzi.
Kuhusu Ukawa
Akizungumzia suala la wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni, Dk Slaa alisisitiza kuwa hawatarudi kwa kuwa Bunge hilo linaendeshwa kwa ubabe. “Nawahurumia sana viongozi wa Serikali na ninawasamehe bure kwa kuwapotosha wananchi. Sisi haturudi bungeni kujadili Katiba kwa kuwa kuna ubabe,” alisema Dk Slaa.
“Tulianza kujadili pole pole tukidhani kuwa tutafikia mwafaka. Ndiyo maana kila lilipotokea tatizo tulikwenda kwa Rais tukiamini kuwa yeye ni raia wa kwanza. Lakini hatujapata suluhisho.”
Mbali na kurudi bungeni, Dk Slaa alisema kuwa hata wajumbe wa Ukawa walioitwa kwenye kamati ya maridhiano inayokutana Dar es Salaam, pia hawatakwenda.
“CCM wanapinga serikali tatu kwa kuwa wanajua Rasimu ya Katiba imepunguza idadi ya wabunge kutoka 340 hadi 75 na wabunge wa viti maalumu hadi 25… Msingi wa Rasimu ile ni serikali tatu, ukiuondoa umevuruga kila kitu. Ukibomoa msingi wa nyumba ukuta utasimama?” alihoji na kuongeza:
“Hiyo kamati ya maridhiano hatutashiriki hata kama wametoa majina kwenye vyombo vya habari. (Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel) Sitta alishatutukana na viongozi wa dini nao walitukana, halafu leo wanatuita kwenye maridhiano.”Sitta ameitisha mkutano huo Julai 24 mwaka huu ambao utafanyika jijini Dar es Salaam.

No comments: