|
Balozi Kijazi amesema wenyeji na Waafrika wanafaa kuwa wakikutana na kujadiliana
|
Balozi wa Tanzania
nchini India John Kijazi amesema ameridhika kwamba serikali ya nchi
hiyo imeweka mikakati ya kutosha kuwalinda wanafunzi, kufuatia kisa
ambapo wanafunzi wanne walishambuliwa mjini Bangalore Jumapili.
Akizungumza
baada ya kutembelea pahala ambapo wanafunzi hao walishambuliwa, na
mmoja wao kuvuliwa nguo, Bw Kijazi amesema huenda kisa hicho kilitokana
na suitafahamu.
“Kilicho muhimu ni tuangalie siku za usoni kwa
sababu tusipofanya hivyo tutapotea. Tunahitaji kutatua tatizo la sasa
lakini pia tuangalie mikakati ya muda mrefu,” ameambia wanahabari.
“Nimeridhishwa na hatua za kiusalama ambazo zimechukuliwa na serikali hapa. Kuna maafisa ambao wamesimamishwa kazi.”
Balozi huyo alikata kutaja kisa hicho kama cha ubaguzi wa rangi.
“Hatukutaka kuangazia masuala ya ubaguzi wa rangi na mambo
mengine kwa sababu nadhani vyombo vya habari vinapendezwa sana na hilo.
Tumejadiliana kuhusu masuala halisi na hatua madhubuti ambazo tayari
zimechukuliwa na serikali ya hapa,” amesema.
Bw Kijazi alisafiri
hadi Bangalore akiandamana na maafisa wawili wa wizara ya mambo ya nje
ya India ambapo walikutana na waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la
Karnataka Dkt G Parameshwara na wakuu wa polisi wa jimbo hilo.
Polisi mjini Bangalore wamewakamata watu tisa kuhusiana na kisa hicho.
Mkuu
wa kituo cha polisi cha Soldevenahalli pia amesimamishwa kazi kwa
tuhuma kwamba hakuchunguza kwa undani kisa hicho baada ya mmoja wa
wanafunzi hao kupiga ripoti.
Konstebo wa polisi pia amesimamishwa kazi kwa kutochukua hatua kuzuia wanafunzi hao wasishambuliwe na umati.