CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga mkakati mpya wa kuengua wataka urais
wanaume kwa kuingiza hisia za kijinsia kama walivyofanya kumdhibiti
aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, alipotaka kugombea tena
nafasi hiyo mwaka 2010.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wameliambia waandishi wetu Jumapili
kuwa mkakati huo unalenga zaidi kumng’oa Mbunge wa Monduli, Edward
Lowassa, ambaye anaonekana tishio kwa wenzake wanaotajwa kutaka urais.
Kwa mkakati huo, kundi la wana CCM walio karibu na Rais Jakaya
Kikwete, wameanza kuzungumzia jinsi ya kumpitisha Dk. Asha-Rose Migiro
agombee urais katika uchaguzi mkuu ujao 2015.
Kisingizio wanachotumia katika kampeni yao ya siri, ni kusaka kura za wanawake.
Katika mkakati huo, wanamwandaa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard
Membe, kuwa Waziri Mkuu. Tayari Membe ameshatangaza kuwa hatagombea
ubunge mwaka 2015.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Membe ndiye alikuwa akipigiwa chapuo
zaidi miongoni mwa makada wa CCM ili kurithi mikoba ya Rais Kikwete,
lakini kutokana na uhusiano wa kifamilia uliopo baina ya wawili hao,
sasa ameshawishiwa kuwa atakuwa waziri mkuu endapo Dk. Migiro atashinda.
Wiki hii, Jumatano iliripoti mkakati
wa kumzima Lowassa asigombee urais, ambao unaendeshwa na mtoto wa kigogo
akishirikiana na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Dk. Migiro ambaye kwa sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria, na pia
Mkurugenzi wa Idara ya Mahusiano ya Nje wa CCM, tayari ameanza
kuzungushwa mikoani ili kumjengea uwezo na uzoefu wa kisiasa.
Miongoni mwa wana CCM wanaotajwa kuutaka urais 2015 mbali na Lowassa
na Membe, ni Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (Mahusiano), Stephen Wasira, William Ngeleja na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
“Ukiwalinganisha Membe na Lowassa kwa nguvu na umaarufu ndani ya CCM,
hata vigogo wengine wanaotajwa kuutaka urais, utaona hakuna wa
kumshinda Lowassa, sasa ndani ya chama wameamua kumchezea rafu.
“Kwa vile ana mtandao mrefu ndani ya CCM, wanafahamu wakikata jina
lake itakuwa balaa, hivyo wameona waibuke na hoja ya zamu ya wanawake
kama walivyomzima Samuel Sitta asigombee uspika wakampa Anne Makinda,”
alisema mtoa habari wetu.
Chanzo hicho kinaongeza kuwa mlengwa ni mtoto wa kigogo ambaye
anaendesha mkakati wa kumchafua Lowassa ili 2025 ndiye awe mgombea urais
baada ya Dk. Migiro kumaliza uongozi wake endapo atachaguliwa kwa
vipindi viwili.
Pamoja na mkakati huo, kundi la Membe limeshauriwa kuendelea na
harakati za kujiimarisha ili kuhadaa makundi mengine ndani ya chama
yaamini kwamba naye ni miongoni mwa watakaochukua fomu za kuomba
kuteuliwa kuwania urais.
Hata hivyo, wakati CCM ikiendesha mkakati huo dhidi ya Dk. Migiro
ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, baadhi ya wasomi wamemchambua mwanamama huyo wakisema hana
uwezo huo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, alisema kuwa Dk. Migiro haonekani kubadilika licha ya
kuwa na elimu kubwa.
“Nilimtembelea ofisini kwake akiwa UN kama Naibu Katibu Mkuu,
nilikuwa na kazi za kitaifa kabisa kwa masuala yaliyoshirikisha mabalozi
wa Ulaya, lakini aliponiona aliniuliza kwanini sitaki kurejea CCM.
“Huyu hawezi hata kubaini hapa tunazungumzia masuala ya kitaifa au
kimataifa, yeye akili yake inawaza CCM tu kila wakati, hajaonyesha
kutofautisha u-CCM wake na taaluma ili aweze kusaidia katika nyanja za
kitaifa na kimataifa,” alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa aliposikia kuwa Dk. Migiro ndiye aliyeandaa
rasimu ya kwanza na ya pili ya katiba kwa upande CCM ambazo zinaleta
shida kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba zikikinzana na rasimu ya
Tume ya Jaji Warioba, amedhihirisha kabisa udhaifu wake.
“Ukiangalia rekodi zake akiwa UN, huwezi ukaona matokeo yoyote, ndiyo
maana Ban Ki moon hakutaka tena asaini mkataba kwa awamu nyingine kwani
hakuwa na msaada kwake,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Azavery Lwaitama ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Bukoba ambaye
alisema kuwa Dk. Migiro sio mtu mwenye umaarufu wowote ambao unaweza
kumfanya amweke katika orodha ya watu wanaoweza kuwa viongozi wa nchi
hii.
“Aliteuliwa kuwa Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, akafanya kazi
kipindi kifupi na baadaye akafanywa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati
wa awamu ya Rais Kikwete.
“Kutokana na kunong’onezana kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Ban Ki moon na Rais Kikwete, Dk. Migiro aliteuliwa kuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa na baadaye kwa utaratibu huo huo wa
kunong’onezana akarejeshwa tena nchini,” alisema.
Dk. Lwaitama aliongeza kuwa vyombo vya habari vya nje viliandika
vizuri kuhusu uwezo wa Dk. Migiro wakati akiwa Umoja wa Mataifa, lakini
Watanzania hawakujishughulisha kuangalia yaliyoandikwa.
“Nilitarajia kuwa yeye atakuwa na mawazo tofauti katika mjadala wa
rasimu iliyopo bungeni, lakini amerudi kwa wana CCM wenzake, anafikiri
kama wao, analeta ushabiki wa makundi ya kisiasa, kwa utaratibu huo
hawezi kuwa kiongozi anayefaa,” alisema.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ambaye ni
mwanafunzi wa Dk. Migiro, alisema haoni dalili au uwezo wowote wa yeye
kuwa kiongozi katika wadhifa huo mkubwa wa urais.
“Huyu hajawahi kushiriki uchaguzi wowote akashinda, ukiwemo hata ubunge, isipokuwa nafasi za kuteuliwa ambazo hupewa na marais.
“Angalia kwa mfano katika Bunge hili la katiba ametoa mchango gani wa
kukumbukwa na wananchi licha ya kuchangia na kubaki katika Bunge
linalotoa matusi na kuacha kujadili rasimu?” alisema Lissu.
No comments:
Post a Comment