Sunday, 27 April 2014

Morgan Tsvangirai asimamishwa uongozi MDC


Morgan Tsvangirai
Chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change MDC kimesema kimemsimamisha kiongozi wake Morgan Tsvangirai kwa kukiuka kanuni za kidemokrasia.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa MDC Tendai Biti kufuatia mkutano wa chama hicho uliofanyika katika mji Mkuu Harare.
Tangu mwaka 2009 hadi 2013 Bwana Tsvangirai alitumikia taifa la Zimbabwe katika nafasi ya Waziri Mkuu katika serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa kwa pamoja na Rais wa sasa Robert Mugabe.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilifikia kikomo mwezi julai mwaka 2013 baada ya Rais Mugabe kushinda kwa wingi wa kura katika uchaguzi wa rais na Tsvangirai kususia uchaguzi kwa madai ya udanganyifu.
Kushindwa kwake kulipunguza nguvu yake kama kiongozi ambaye alikuwa mshindani mkuu wa Rais Mugabe.
Waangalizi wanasema ndani ya MDC kumekuwa na mgogoro wa kiuongozi kwa miezi kadhaa.
Viongozi wengine wa ngazi za juu wameripotiwa kusimamishwa katika mkutano huo uliofanyika siku ya jumamosi na wanachama wengine wa chama hicho watachukua nafasi zao.

No comments: