Tuesday, 15 April 2014

Jangili La uawa kwa kupigwa risasi

JESHI la Polisi mkoani Simiyu kwa kushirikiana na askari wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, mkoani Mara, wamefanikiwa kumuua jangili ambaye pia ni jambazi sugu aliyekuwa akitafutwa miaka 17, kuanzia mwaka 1997. Jangili huyo amefahamika kwa jina la Majadiga Makabajinga au ‘Mashaka Sai’, ambaye alipigwa
risasi mgongoni wakati akijaribu kutoroka mikononi mwa askari hao.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Charles Mkumbo, alisema jangili
huyo aliuawa juzi saa tatu usiku katika Kijiji cha Mwasinansi, Kata ya Nkololo, wilayani Bariadi.
Alisema awali jangili huyo alikamatwa kwenye Kata ya Kisesa, wilayani Meatu ambapo baada
ya kuhojiwa, alikiri kuhusika na matukio ya ujangili na mauaji ya askari wanyamapori.
“Huyu jangili alikuwa maarufu kwa kuua watu ambao alikuwa akiwahisi kuwa wanatoa taarifa
zake za uharifu kwa Jeshi la Polisi, pia alikuwa kinara wa kuua faru na tembo, inadaiwa alihusika na mauaji ya faru wa JK katika Hifadhi
ya Seregeti,” alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya polisi kufanya naye mahojiano, walimtaka awapeleke sehemu aliyokuwa akihifadhi silaha alizokuwa akizitumia kufanya uhalifu huo hivyo alikubali na kuongozana nao hadi Kijiji cha Mwasinasi, Kata ya Nkololo.
“Walipofika kijijini hapo, mtuhumiwa aliwapeleka katika kichaka na kuwaonesha eneo
alilokuwa akificha silaha zake, wakati polisi wakifanya upekuzi, mtuhumiwa huyu alimpiga
kichwani askari wanyamapori Christian Mlema kwa mti na kumnyang’anya silaha.
“Alipochukua silaha hiyo, alianza kufyatua risasi hovyo ndipo askari mmoja akafanikiwa kumpiga
risasi ngongoni na kudondoka chini...askari waliendelea na msako katika eneo hilo na kufanikiwa kukuta bunduki mbili moja SMG
iliyokuwa na magazine mbili na SR zote zikiwa na risasi 50, pamoja na meno ya tembo,” alisema.
Jangili huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda kwa ajili ya matibabu lakini alifariki dunia akiwa njiani.

No comments: