Tuesday 15 April 2014

Serikali isipeleke siasa katika nyumba za ibada

Katika kuthibitisha kwamba hotuba yake siyo tu ililenga kujenga hofu, bali pia kuwagawa wananchi, Waziri Lukuvi alidai kwamba Wazanzibari hawawezi kujitegemea na wanaotaka kuwa na nchi yao wana ajenda ya siri ya kutaka wapate nafasi ya kujitangaza kuwa nchi ya Kiislamu, mbali na kutaka kufanya fujo na kusababisha machafuko.

Tunalaani vikali hatua ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi kufanya kampeni za kisiasa kanisani kwa kuwataka waumini kupinga muundo wa serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa madai kwamba muundo huo utasababisha nchi yetu itawaliwe na jeshi eti kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kulipa mishahara ya wanajeshi.

Alisema jeshi haliwezi kukaa na bunduki bila fedha na kwamba hiyo serikali ya tatu, ambayo jeshi litakuwa chini yake haitakuwa na vyanzo vya mapato ya kueleweka na kuuliza: Sasa hao wanajeshi watalipwa nini? Wenye mitutu ya bunduki watakubali kuishi bila fedha? Tunadhani maswali hayo yanathibitisha jinsi Waziri Lukuvi asivyokuwa na nia njema kwenye mchakato wa Katiba kwani anashindwa nini kutambua kwamba majukumu ya Bunge la Katiba ni pamoja na kuboresha Rasimu ya Katiba. Moja ya maboresho hayo ni kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili Serikali ya Muungano inayopendekezwa iweze kujitegemea na kutimiza majukumu yake, ikiwamo kulipa mishahara ya wanajeshi na watumishi wake wengine.

Kauli hiyo hatari na ya kichochezi aliitoa juzi katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu katika ibada ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa askofu wa kanisa hilo wa Jimbo la Dodoma. Katika hotuba yake ambayo bila shaka ililenga kupandikiza hofu kwa wananchi waliohudhuria ibada hiyo, waziri huyo aliwaasa waumini waliombee Bunge lifanye kile alichokiita uamuzi sahihi wa kupitisha muundo wa serikali mbili, huku akiwataka kuipuuza Rasimu ya Katiba katika suala la Muungano wa serikali tatu ili kuepusha nchi yetu isiingie vitani.

Katika hotuba hiyo, ambayo ilijaa shari na maudhui ya kisiasa yanayoweza kuvuruga mchakato mzima wa Katiba mpya unaoendelea hivi sasa, Waziri Lukuvi alidai kwamba muundo wa serikali tatu ukipita hata makanisa yatafungwa kwa vile nchi haitakuwa na amani tena. Alisema Bunge sasa liko katika hali mbaya sana kutokana na watu aliodai wanataka madaraka kwa nguvu na wanatafuta jinsi ya kuvunja Muungano kwa kudai kuwapo Serikali ya Tanganyika, huku akiwabeza kwamba hiyo Tanganyika wanayoidai ni jina tu ambalo Wajerumani walikaa mezani wakabuni na kutuletea.

Katika kuthibitisha kwamba hotuba yake siyo tu ililenga kujenga hofu, bali pia kuwagawa wananchi, Waziri Lukuvi alidai kwamba Wazanzibari hawawezi kujitegemea na wanaotaka kuwa na nchi yao wana ajenda ya siri ya kutaka wapate nafasi ya kujitangaza kuwa nchi ya Kiislamu, mbali na kutaka kufanya fujo na kusababisha machafuko. Pamoja na kudai kwamba hayo ni mawazo yake binafsi, alisema yanafanana sana na mawazo ya Watanzania wengi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete.

Tumezungumzia kwa kirefu kauli zilizotolewa na Waziri Lukuvi ili kuonyesha jinsi Serikali inavyoonekana kukata tamaa katika suala la kupatikana kwa Katiba mpya kiasi cha kulazimika kupeleka mjadala wake katika nyumba ya ibada. Waziri Lukuvi anasahau kwamba alihudhuria ibada hiyo kama mwakilishi wa Serikali, hivyo hotuba aliyoitoa ilikuwa ikiwakilisha mawazo, maono na msimamo wa Serikali na siyo mawazo yake binafsi kama anavyodai. Haiingii akilini kwamba kauli alizotoa hazikuwa na baraka za Serikali. Vinginevyo, Waziri Lukuvi angekuwa tayari amewajibishwa na mamlaka iliyomteua.

No comments: