Wachezaji wa Simba wakipewa maelekezo na Kocha Logarusic. |
0inShare
UKITAKA mafanikio lazima uchukue uamuzi mgumu ambao hakuna anayeweza kufikiria kabla.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic amesema
analazimika kutema wachezaji wasiopungua 11 ambao ni sawa na kikosi
kizima kinachoweza kucheza mechi ya ushindani.
Lengo la Logarusic kufanya hivyo ni ili aweze kujenga upya timu ya ushindani msimu ujao.
Logarusic sasa ana uhakika wa kubaki Simba, baada
ya kuhakikishiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo,
Zacharia Hans Pope kwani awali hakuwa na uhakika wa kuendelea kubaki
katika timu hiyo kutokana na mkataba wake kumalizika.
Kocha huyo atasaini mkataba wa miaka miwili baada ya ule wa miezi sita kufikia tamati.
Katika ripoti yake kwa uongozi wa timu hiyo,
Logarusic amewaeleza wazi viongozi wake kuwa, ili Simba iwe na ushiriki
mzuri msimu ujao wa Ligi Kuu Bara lazima nyota 11 wa timu hiyo waachwe
ili wapatikane wengine watakaoisaidia timu kufikia mafanikio.
Akizungumza na Mwanaspoti usiku wa kuamkia jana
Ijumaa dakika chache kabla ya kupanda ndege kwenda kwao Croatia kwa
mapumziko, Logarusic alisema wachezaji anaotaka kuwaacha si kwamba
hawana viwango vizuri, tatizo hawana nafasi kikosi cha kwanza.
“Simba inahitaji ubingwa, unawezaje kuupata bila
ya kuwa na wachezaji wenye uwezo? Nimekabidhi ripoti yangu tayari kwa
uongozi sioni sababu ya kuficha mambo yaliyo wazi ni kwamba nataka
kubaki na wachezaji 13 tu katika kikosi cha sasa.
“Nimewaambia viongozi nataka kurudi kuanzia Juni
kufanya kazi moja ya kurudisha heshima ya timu hii, katika hilo hao
niliowaona hawana nafasi Simba watajua kwa kuwapeleka, chini yangu
hawana nafasi, nataka wachezaji wenye uzoefu mkubwa na wanaozitumikia
timu za taifa.
“Tazama benchi nina wachezaji wengi kuliko kikosi
cha kwanza na ikitokea mchezaji mmoja anaumwa napata presha sina mtu wa
uhakika wa kumpanga,’’ alisema Logarusic.
Amemaliza kazi
Logarusic ameshapiga mstari mwekundu katika orodha
ya wachezaji 24 walioichezea Simba mzunguko wa pili wa msimu uliopita
na kubaki na 13 tu hivyo 11 wataachwa kwa makubaliano maalum au
kupelekwa kwa mkopo timu nyingine. Kabla hajaanza kuiongoza Simba,
Logarusic alikuwa na wachezaji 36 ambao aliwapunguza na kubaki 24 tu.
Sababu kubwa ya kupunguza wachezaji hao ambao hakukuwa na hata
mmoja aliyesajiliwa na kocha huyo ni uwezo mdogo huku wengi wakionekana
kutoweza kupambana uwanjani.
Hata hivyo inadaiwa kwamba baadhi ya wachezaji
wenye umri mdogo kati ya 11 wasiotakiwa na Logarusic watarudishwa Simba B
ili kukuza viwango vyao.
Wanaobaki
Ingawa nyota watakaochwa imekuwa siri nzito lakini
tathimini ya Mwanaspoti imebaini kuwa wenye nafasi kubwa ya kubaki ni
Joseph Owino, Donald Mosoti, Nassoro Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba
Ubaya’ na William Lucian ‘Gallas’ wakati viungo ni Jonas Mkude, Said
Ndemla, Ramadhan Singano, Awadh Juma, Amri Kiemba, Haroun Chanongo na
mshambuliaji ni Amissi Tambwe pekee.
Watakaoachwa.
Wachezaji walio katika hatari ya kuachwa ni kipa
Yaw Berko, Uhuru Seleman, Henry Joseph ambao mikataba yao imeisha.
Wengine ni Abuu Hashim na Bertam Mwombeki ambao inadaiwa hawana
maelewano mazuri na Logarusic huku Hassan Hatib, Ally Badru, Ramadhan
Chombo ‘Redondo’, Abduhalim Humud na Zahoro Pazi wakidaiwa kutojituma na
kuonyesha uwezo uwanjani.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga alikiri
kupokea ripoti hiyo na kusema: “Tumepokea ripoti ya kocha, kuna
wachezaji amependekeza tuwaache lakini kwa sasa hatuwezi kuweka wazi
majina yao.
“Tunataka kwanza kuyafanyia kazi kama viongozi na
baada ya hapo tutakutana nao kuzungumza jinsi ya kuachana nao, kazi hiyo
tutaifanya Jumatatu (keshokutwa).
No comments:
Post a Comment