RAIS
Jakaya Kikwete amehujumiwa na viongozi wakuu wastaafu waliomlazimisha
kuachana na msimamo wa muundo wa muungano wa serikali tatu na kukumbatia
serikali mbili zilizopendekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Taarifa kutoka kwa baadhi ya vyanzo vya habari vilivyo karibu na
rais, Ikulu na makao makuu ya CCM, zimelithibitishia gazeti hili kwamba
hadi Bunge Maalumu la Katiba linaanza, Rais Kikwete alikuwa na msimamo
ule ule wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Baadhi ya viongozi wastaafu, wakiwamo marais na viongozi waandamizi
wa CCM, walishinikiza rais aachane na serikali tatu, kwa vitisho kwamba
zitaua muungano.
Baadhi ya wastaafu hao walimficha Rais Kikwete kwamba kwa kuwa yeye
aliingia madarakani akiwa rais wa muungano wa serikali mbili, halikuwa
jambo la busara kwake kujiingiza kwenye historia ya kuwa rais aliyevunja
muungano.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, shinikizo hilo liliambatana na jingine la
kumtaka asizindue Bunge kabla ya rasimu ya pili ya katiba mpya
kuwasilishwa bungeni, ili apate fursa ya kudhoofisha hoja ya serikali
tatu.
Mara baada ya Rais Kikwete kukubaliana na “washauri wake”, serikali
ililazimika kuingilia kati ili Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta atengue
kanuni, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba awasilishe rasimu kabla
ya rais kuzindua Bunge, jambo ambalo limesababisha mvurugano unaotishia
kuvuruga kabisa mchakato wa katiba mpya.
Hata hivyo, hali hiyo inasemekana kumnyima amani Rais Kikwete ambaye
ndiye aliyepokea na kusaini rasimu hiyo, kwa maana kwamba aliridhia.
Uamuzi huo umefanya rais aonekane kiongozi asiye na msimamo thabiti katika masuala muhimu.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai hatua hii
imemfanya ashindwe kuacha urithi makini na muhimu katika utawala wake wa
miaka 10, kama ambavyo alikuwa amedhamiria.
Wadadisi wanasema wastaafu walimzuia rais kutekeleza azima yake kwa
sababu ya hofu tu, wakidhani kwamba katiba mpya yenye mfumo mpya inaweza
kufumua mambo yaliyofichika na kuwaingiza matatani.
Wanadai kwamba muungano wenye mfumo mpya una kila dalili za kuiondoa
CCM madarakani, na kuhatarisha maslahi ya watawala waliopo na waliopita.
Hoja hii, kwa mujibu wa vyanzo vyetu, ndiyo ilimkuna Rais Kikwete hata akabadili msimamo.
Kwa hali halisi ilivyo, na mchakato unavyoendelea, ahadi ya Rais Kikwete kuwapa Watanzania katiba mpya mwezi huu imeshindikana.
Alipohutubia taifa na kutangaza kuanzisha mchakato wa katiba mpya
miaka mitatu iliyopita, alisema kwamba lengo lake lilikuwa kuzindua
katiba mpya katika maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya muungano
iliyofanyika jana.
Hadi Bunge Maalumu la Katiba linaahirishwa juzi, zilikuwa zimepita
siku 68 kati ya 70 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, huku kukiwapo
mgawanyiko mkubwa wa wajumbe na kutishia uhai wa muungano, hasa baada ya
wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia Bunge
baada ya kukerwa na hujuma na matusi kutoka kwa wajumbe wenzao wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Hadi sasa Bunge la Katiba limefanikiwa kujadili sura mbili za rasimu
bila ya kuzipigia kura. CCM imekataa maoni ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba yanayopendekeza mfumo wa muungano wa serikali tatu, wakatetea
mfumo wa serikali mbili.
Mapendekezo hayo ni kinyume kabisa cha yaliyomo kwenye rasimu ya Tume
ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa ili ijadiliwe na wajumbe hao na
kisha kutunga katiba mpya.
UKAWA wanadai kuchoshwa na vitisho na matusi kutoka kwa wajumbe wa
CCM na viongozi wa serikali, wakisema kuwa kwa hali ilivyo katiba bora
ya wananchi haiwezi kupatikana kwa shinikizo la muundo wa serikali
mbili.
Katika hili, Rais Kikwete analalamikiwa kuwa ndiye mvurugaji wa
kwanza wa mchakato ambao aliuasisi na kuahidi kuwapatia wananchi katiba
bora kabla ya kuondoka madarakani.
Wakati akilihutubia Bunge la Katiba na kulizindua rasmi Machi mwaka
huu, Rais Kikwete aliibeza rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, akisema
takwimu zao kuhusu watu waliotoa maoni ya muundo wa muungano zinatiliwa
shaka.
Alisema kuwa muundo wa serikali tatu unaopendekezwa hautekelezeki
kwani rais wa dola hiyo hatakuwa na mamlaka kwa vile hana ardhi,
rasilimali na hivyo hataweza kukopa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, katika hali kama hiyo, jeshi linaweza
kupindua serikali na hivyo ukawa mwanzo wa kuvunjika kwa muungano, huku
akisisitiza kwamba wao kama CCM muundo ambao unaweza kutatua kero
zilizopo ni ule wa sasa wa serikali mbili.
Kauli hiyo ya rais iliibua mjadala mkubwa, na hivyo kufifisha ndoto
za kupatikana kwa katiba bora kwani ilionyesha wazi kwamba mapendekezo
ya wananchi ya serikali tatu yaliyomo kwenye rasimu hayatazingatiwa.
Hali hiyo imeendelea kujitokeza kwenye Bunge Maalumu la Katiba baada
ya wajumbe wote wa CCM kuendeleza msimamo wa rais wa serikali mbili na
kumshambulia Jaji Warioba binafsi kwa matusi mazito wakidai ana ajenda
ya kuvunja muungano kwa kupendekeza serikali tatu.
Hatua ya Rais Kikwete kubadilika na kuvuruga mchakato aliyouasisi na
kuusimamia kwa mafanikio makubwa, imeelezwa kusababishwa na mambo
makubwa mawili, likiwemo hilo la kuburuzwa na viongozi wastaafu.
Duru nyingine za kisiasa katika suala hilo la kukwama kwa mchakato wa
katiba, zinahusisha na rasilimali ya gesi na mafuta zilizopatikana
nchini, ambapo inadaiwa mataifa makubwa yanayotaka kuwekeza ndiyo
yanaishinikiza serikali isibadili muundo wa muungano uliopo.
Vyanzo vyetu vya habari vinaeleza kwamba mataifa hayo tayari yameweka
msimamo wa kuisaidia CCM kifedha ili kuhakikisha inapigana kufa au
kupona kutobadili muundo wa muungano katika katiba mpya.
Inaelezwa kuwa muundo wa shirikisho la serikali tatu unaopendekezwa
kwenye rasimu ya katiba mpya, unatoa fursa ya wazi kwa wananchi wa
serikali washirika kusimamia rasilimali zao tofauti na ilivyo katika
muundo wa sasa ambapo mambo mengi yamefanywa siri na serikali.
Hadi sasa majaliwa ya kupatikana kwa katiba mpya yametoweka baada ya
UKAWA kujiondoa, na hivyo kulifanya Bunge la Katiba kushindwa kufanya
maamuzi ya kupitisha ibara na sura za rasimu kutokana na theluthi mbili
ya wajumbe kutoka Zanzibar kushindikana.
No comments:
Post a Comment