Saturday, 26 April 2014

Urusi yawekewa vikwazo vipya na Ulaya na Marekani

Rais wa Marekani Barack Obama na viongozi wa nchi muhimu za Umoja wa Ulaya wamekubaliana juu ya hatua za kuiwekea Urusi vikwazo vipya. Maafisa wa Marekani wamesema vikwazo hivyo vinaweza kutekelezwa siku chache zijazo
Mvutano unaoendelea mashariki mwa Ukraine umesababisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi
Mvutano unaoendelea mashariki mwa Ukraine umesababisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi
Afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la AFP kuwa upo uwezekano kwamba vikwazo vipya vya Marekani vitaanza kutekelezwa Jumatatu wiki ijayo, akionya kwamba hali nchini Ukraine inaendelea kuwa yenye wasiwasi mkubwa.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya watakutana hivi karibuni kujadili vikwazo vipya vya umoja huo. Bi Merkel ameyasema hayo baada ya mkutano kwa njia ya simu baina yake na rais Obama, waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, rais wa Ufaransa Francois Hollande na waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi.
''Kutokana na mkwamo uliopo, tunapaswa kutafakari--na sio kutafakari tu, bali pia kuchukua hatua juu ya vikwazo vipya'' amesema Angela Merkel.
Watu binafsi na taasi ndio walengwa
Rais Vladimir Putin wa Urusi akikagua utayarifu wa jeshi lake (2012)
Rais Vladimir Putin wa Urusi akikagua utayarifu wa jeshi lake (2012)
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Jen Psaki amewaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba wamekuwa wakishirikiana na wenzao wa Ulaya na kwamba ni sahihi kusema kwamba wamefika mahali ambapo suala sio kuandaa bali kuratibu vikwazo vipya na kutafakari maamuzi yatakayofuata baadaye.
Inaelekea awamu mpya ya vikwazo dhidi ya Warusi na waukraine wanaotuhumiwa kuendeleza hali ya ghasia, vitawalenga watu binafsi na taasisi.
Ulaya na Marekani zimekwishawawekea vikwazo maafisa zaid ya 10, wakiwemo viongozi wa jimbo lililojitenga na Ukraine la Crimea.
Sekta muhimu hazitaguswa
Rais wa Marekani Barack Obama anaongoza shinikizo dhidi ya Urusi
Rais wa Marekani Barack Obama anaongoza shinikizo dhidi ya Urusi
Akizungumza jana ziarani Korea Kusini, Rais Obama alisema vikwazo vipya dhidi ya Urusi vilikuwa tayari, vikisubiri tu kutekelezwa.
Hata hivyo Obama aliweka wazi kwamba vikwazo hivyo havitazilenga sekta muhimu za uchumi wa Urusi kama vile uchimbaji madini, nishati na sekta ya fedha. Maafisa wa Marekani wamesema sekta hizo zitawekewa vikwazo ikiwa tu Urusi itaingiza jeshi lake ndani ya mipaka ya Ukraine.
Tangazo la Ikulu ya Ufaransa mjini Paris lilizungumzia pia vikwazo hivyo, likisema viongozi wa mataifa na serikali wamezitaka nchi saba zinazoongoza kiviwanda-G7, kuichukulia hatua Urusi bila kukawia, na kuweka uwezekano wa vikwazo vya jumuiya ya kimataifa dhidi ya nchi hiyo.

No comments: