LIGI Kuu Bara msimu wa 2013/14
imemalizika huku straika wa Simba, Amissi Tambwe, akiibuka Mfungaji Bora
baada ya kufunga mabao 19. Lakini mchezaji huyo amekaa siku chache tu
nje ya uwanja na sasa anafanya mazoezi katika ufukwe wa Coco jijini Dar
es Salaam.
Akiwa ufukweni hapo, Tambwe hufanya mazoezi ya
kukimbia ili kuongeza pumzi za kupambana uwanjani na yale ya kujenga
stamina ili aweze kuwapenya kwa nguvu mabeki wa timu pinzani.
Yote hayo anajiandaa kwa msimu mpya unaotarajiwa
kuanza Agosti. Kwa mabao hayo 19 aliyofunga, Tambwe alimzidi straika wa
Azam FC, Kipre Tchetche aliyefunga mabao 14 huku Didier Kavumbagu wa
Yanga na Elius Maguli wa Ruvu Shooting,
kila mmoja akifanya hivyo mara 13. Akizungumza na
Mwanaspoti, Tambwe ambaye alitarajiwa kuungana na kikosi cha Burundi
kilichotarajiwa kuwasili jana jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi ya
kirafiki dhidi ya Taifa Stars ya kesho Jumamosi, alisema ameamua kufanya
mazoezi ufukweni ili kujiweka vizuri kwa msimu ujao wa ligi.
Mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam pia ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
“Kwa sababu kwa sasa mazoezi ya timu yamesimama
kwa muda, huwa naenda kwenye fukwe wa Coco na kufanya mazoezi yangu
binafsi kama kukimbia na mambo mengine,” alisema.
“Huwa sifanyi kila siku, ila sina siku maalumu, inategemea na siku hiyo nahitaji kufanya mazoezi yangu kwa namna gani.
“Hii yote nafanya kwa sababu maisha yangu
yanategemea soka hivyo lazima nihakikishe nipo vizuri muda wote ili
mambo yasiniharibikie, si unajua mpira sasa ni ushindani? Hakuna
anayekubali kuachwa kirahisi uwanjani.”
Tambwe ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni
walioonyesha uwezo mkubwa katika kuzifumania nyavu na kuongeza msisimko
wa ligi kuu, raia wa kigeni wengine waliofanya vizuri katika ligi hiyo
ni Tchetche raia wa Ivory Coast, Mrundi Kavumbagu wa Yanga na Mganda
Hamis Kiiza pia wa Yanga aliyefunga mabao 12.
Tambwe alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu
uliopita akitokea Vital’O ya Burundi sambamba na beki Gilbert Kaze. Hata
hivyo Kaze hakucheza mechi za mzunguko wa pili kutokana na kusumbuliwa
na maumivu ya goti.
No comments:
Post a Comment