Sunday, 27 April 2014

Nyumba ya teketea kwa moto Iringa

mali zilizoteketea kwa  moto
Askari  wa  kikosi  cha  Zimamoto Iringa  wakiwajibika
MOTO  mkubwa  umezuka  katika  nyumba  ya mkazi  mmoja  wa  eneo la Zizi la Ng'ombe katika Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa na kupelekea mtu mmoja kupoteza  fahamu  baada ya  nyumba yake  kuwaka  moto majira ya  saa 8 mchana  wa leo.
Mashuhuda wa  tukio   hilo  wameueleza mtandao Huu kuwa  moto  huo  chanzo chake  kimesababishwa na mtoto mdogo  ambae  alikuwa  ndani ya  nyumba  hiyo akichezea  moto ndani ya  nyumba  hiyo na  kusababisha  moto  huo kushika makochi yaliyokuwemo ndani ya  nyumba  hiyo.

Nyumba  hiyo  mali ya  Bi Grace  Mpewa  imenusurika  kuteketea  yote  baada ya  wananchi  wa  eneo hilo kuendelea  kuzima  moto  huo bila ya  kutoa taarifa  jeshi la  zima moto na uokoaji mjini hapa  kiasi cha  moto  huo kuteketeza  sehemu kubwa ya  nyumba  hiyo .

Balozi  wa  eneo  hilo la  Zizi la Ng'ombe  Edmundi Kikula  alisema  kuwa  baada ya  kuzuka  moto  huo  walifika  kutoa msaada  na  kuanza  kuzima  moto  huo  huku mmiliki wa  nyumba  hiyo bila kuwepo na kuwa mtoto  huyo baada ya  kuulizwa alidai kuwa mama  yake  ndie  aliacha  jiko la moto huo .

Alisema  kuwa  mali mbali mbali  zimeteketea kwa  moto  huo huku baadhi ya  vitu  vikiokolewa  na  kuwa walishindwa  kutoa taarifa kwa  wakati  zimamoto kutokana na kukosa  namba  zao .

Hata  hivyo  aliwataka  wananchi  wenzake  kuhifadhi namba  za Zimamoto  ili  kutoa  taarifa  kwa wakati  pindi majanga kama  hayo yanapojitokeza badala ya  kuelekeza lawama  kwa kikosi  hicho.
Kwa  upande  wake  stafu  Sajenti  wa kikosi  cha zimamoto na uokoaji mjini  Iringa ambae  alikuwepo  eneo la  tukio Bw Juma Joseph Mkuvalo  alisema  kuwa  kufika kwao  eneo hilo  ni baada ya  kuitwa na jeshi la  polisi  kufuatia  mtandao huu   kufikisha  taarifa  za  tukio  hilo.
Mkuvalo  alisema  jamii  inapaswa  kukabiliana na  matukio ya moto  pale  yanapojitokeza na kuwa huduma  hiyo haina malipo  yoyote na kuwataka  wananchi  kutumia namba  za zimamoto ambayo ni 114 ili  kutoa taarifa.

No comments: