WAKATI sherehe za miaka 41 ya Chuo cha Karate cha Okinawa Goju
Ryu cha Dar es Salaam zikifanyika leo Jumamosi, mmiliki wa Bendi ya
Machozi, Lady Jaydee atatunukiwa mkanda mweupe baada ya kufanya vyema
katika mafunzo.
Kwa mujibu wa mkuu wa chuo hicho, Sensei Wilfred
Malekia, shehere za chuo hicho zimepangwa kuanza saa 12 jioni Shule ya
Zanaki, Dar es Salaam.
Malekia alisema katika sherehe hizo mambo
mbalimbali yatafanyika ikiwamo kuadhimisha kumbukumbu za muasisi wa chuo
hicho, marehemu Camara Bomani Goju Ryu Jundokan aliyefariki mwaka 2009.
“Hii ni sherehe muhimu kwetu, itawakutanisha watu
mbalimbali waliopitia mafunzo katika chuo hiki ambao wanafanya shughuli
zao nyingine,” alisema Malekia.
Akimzungumzia Lady Jaydee, Malekia alisema kuwa
mwanamuziki huyo amejiunga na chuo hicho miezi sita iliyopita na
amekuwa akifanya vyema katika mafunzo yake.
Mbali na Lady Jaydee ambaye pia anafahamika kwa jina la Komando, wanawake wengine watatu nao watavishwa mkanda mweupe.
“Mafunzo haya ni muhimu sana katika maisha ya kila
siku, ndiyo maana katika chuo chetu, kuna wanafunzi wa rika mbali mbali
ambao wanafanya mafunzo hapa,” alisema.
Kwa upande wake, Jaydee alisema kuwa ameamua
kujiunga na mafunzo hayo kwa sababu mbalimbali ikiwamo kumpa stamina
katika kazi yake ya kuimba na kujilinda.
Alisema kuwa mazoezi hayo yanamfanya awe na uwezo wa kufanya shoo zake mbali mbali tokea mwanzo hadi mwisho bila kuchoka.
No comments:
Post a Comment