Monday, 28 April 2014

Chelsea yaichinjia mbali Liverpool



Demba Ba mfungaji wa bao la kwanza la Chelsea dhidi ya Liverpool
Chelsea vijana wa darajani Stanford, jijini London, wamewanyamazisha vinara wa ligi kuu ya England, Liverpool baada ya kuwachakaza mabao 2-0 katika uwanja wao wa Anfield.
Liverpool ikiwa imeuanza mchezo huo kwa kasi na kwa dhamira ya kupata ushindi ilishuhudia jahazi lake likitota katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza.
Alikuwa ni Demba Ba aliyeanza kupeleka kilio kwa majogoo wa Liverpool pale alipounasa mpira kufuatia nahodha wa Liverpool Steven Gerrard kuteleza na Ba kupata mwanya wa kumfunga kirahisi Mignolet.
Liverpool hawakukubali kusalimu amri kwa wageni,kwani waliendelea kupeleka mashumbulizi ya hatari langoni mwa wapinzani wao wakiishia kwa kosa kosa. Liverpool wanapigania ubingwa wa ligi kuu ya England kwa mara ya kwanza katika miaka 24 iliyopita.

Willian mfungaji wa bao la pili la Chelsea dhidi ya Liverpool
Joe Allen na Luis Suarez walizidisha mashambulizi katika lango la Chelsea, kabla ya Willian aliyeingia kipindi cha pili kufunga bao la pili kwa timu yake ya Chelsea baada ya Fernando Torres bila uchoyo akiwa katika nafasi ya kufunga alimpasia Willian na kuwaachia kilio wenyeji wao Liverpool.
Chelsea katika mchezo huo ilikuwa ikipewa nafasi finyu ya kuibuka washindi. Lakini ni Jose Mourinho aliyeibuka na kicheko, huku Brendan Rodgers akiugulia kipigo cha kwanza kwa timu yake tangu kuanza kwa mwaka huu.
Kwa ushindi huo sasa, Chelsea inaachwa pointi mbili nyuma ya Liverpool ambayo inaoongoza ikiwa na pointi 80, baada ya michezo 36. Msimamo wa timu hizo ni Liverpool pointi 80, Chelsea 78, Manchester City 74, itakuwa na pointi 77 iwapo itaifunga Crystal Palace katika mchezo wao, huku Arsenal ikichukua nafasi ya nne ikiwa na pointi 70. Manchester City na Arsenal zimecheza mechi 35 kila moja huku Liverpool na Chelsea zikiwa zimecheza mchezo mmoja zaidi.

No comments: