MERSEYSIDE, LIVERPOOL
KAMA Barrack Obama alivyowaambia Wamarekani katika
harakati za kampeni za uchaguzi wao mwaka 2008 kuwa wanaweza kumaliza
matatizo yao, ndivyo kocha, Brendan Rodgers, alivyowaambia mashabiki wa
Liverpool kuwa wanaweza kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England.
Juzi Jumapili usiku, harufu ya ubingwa wa ligi
hiyo ilianza kunukia katika viunga vya Anfield huku pia mashabiki
wengine wa timu hiyo duniani wakianza kuingiwa na kiwewe baada ya
Liverpool kuichapa Tottenham mabao 4-0.
Wana nafasi kubwa ya kuwa mabingwa kama wakishinda
mechi zao sita zilizobaki ambapo mbili kati ya hizo watacheza na
wapinzani wao katika mbio hizo Chelsea na Manchester City.
Rodgers ana uhakika kuwa timu yake hii ina uwezo
mkubwa wa kuhimili presha na kutwaa ubingwa hasa katika kipindi hiki
ambacho wanaongoza msimamo wa ligi hiyo.
“Bado kuna pointi nyingi za kuzisaka na lazima
kuna pointi zitakazopotezwa na timu zote kabla ya mwisho wa msimu.
Hatuna presha yoyote na tuna uhakika kwa jinsi tunavyocheza,” alisema
Rodgers ambaye alitua Anfield akitokea Swansea.
“Ndoto ya mashabiki wetu ni kutwaa ubingwa.
Imekuwa muda mrefu sana tangu walipotwaa, lakini mimi haipo katika
mawazo yangu. Tunahitaji kujiandaa tu na kufanya vizuri na kama
tukifanya hivyo tutashinda mechi zetu.
“Chelsea na Manchester City wanajua kwamba Anfield
itakuwa sehemu ngumu kuja. Tunapenda kucheza hapa, tunapata sapoti
kubwa na hilo linasababisha tuongeze ari. Tunawaheshimu Chelsea, wana
kocha wa kiwango cha juu sana na wana timu ambayo wameikusanya kwa ajili
ya kushinda Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu.
“Manchester City ni miongoni mwa wababe wapya wa
soka duniani, lakini tunadhani tunaweza kushinda mechi yoyote kwa sababu
sisi ni timu. Tuna njaa na mbinu zetu za kisoka zinaimarika kila siku.”
No comments:
Post a Comment