Sunday, 27 April 2014

BURUNDI ya haribu maadhimisho ya miaka Hamsini ya uhuru

Stars mpya majangaTIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, jana ilitibua furaha ya sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Burundi katika mechi ya kirafiki iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hadi mwamuzi Anthony Ogwayo wa Kenya anapuliza filimbi ya mapumziko, Burundi ilikuwa mbele kwa bao 1-0, likifungwa dakika ya 45 na mshambuliaji Didier Kavumbagu anayecheza soka ya kulipwa nchini katika klabu ya Yanga, akiunganisha kwa ustadi pasi ya Cedric Amisi.
Bao hilo liliwagawa mashabiki wa Yanga, ambao baadhi walishindwa kujizuia kushangilia.
Nje ya mgawanyiko huo wa mashabiki wa Yanga, wengine kushangilia bao la Kavumbagu huku wengine wakimzomea kwa kumtungua kipa wao kipenzi Deogratius Munishi ‘Dida’, zomeazomea nyingine ilikuwa ikimuandama kocha Salum Mayanga wa Stars.
Mayanga alikumbana na kadhia ya kuzomewa mwanzo mwisho kutokana na mashabiki kukerwa na kikosi alichokipanga, ambacho kilijumuisha nyota watano waliotokana na programu ya maboresho ya Stars, huku akiwaacha wanaoshabikiwa na mashabiki.
Bao la Kavumbagu lilikuja dakika moja baada ya kukosa bao jingine, kutokana na juhudi binafsi za Said Moradi, aliyeokoa mpira uliokuwa ukienda nyavuni baada ya Dida kupotezwa maboya akijaribu kudaka.
Mashambulizi hayo yalikuja baada ya Stars kupoteza nafasi mbili huku Burundi ikipoteza moja, katika mechi ambayo ilikuwa na mashabiki wachache, licha ya Rais Jakaya Kikwete kuamuru waingie bure kama sehemu ya kusherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mapema dakika ya 20, Yosso aliyetokana na programu ya maboresho ya Stars, Mohammed Seif, alikosa bao la wazi, akishindwa kabisa kupiga kichwa kumalizia krosi ya winga Simon Msuva, ambaye alikuwa mwiba kwa mabeki wa Burundi.
Intamba Mu Rugambaa, ikalipa shambulizi hilo dakika 10 baadaye, kwa kulifikia lango la Stars, lakini Cedric Amisi akashindwa kufunga, baada ya shuti lake kumbabatiza kipa na mabeki kuondoa hatari langoni mwao.
Mapema kabla ya pambano kuanza, mashabiki wa soka waliokuwa tayari na tiketi mkononi walikuja juu wakitaka warejeshewe pesa zao, hasa baada ya Rais Kikwete kuamuru waingie bure uwanjani hapo.
Baada ya mashabiki hao kuja juu, ndipo walipotakiwa kujikusanya ndani ya uzio wa uwanja ili kuonyesha tiketi zao tayari kwa kurudishiwa pesa zao, lakini katika namna ya kustajabisha, dereva wa gari lililodaiwa kubeba fedha za marejesho aliwasha gari hiyo na kutoweka uwanjani hapo bila kurejesha fedha.
Uamuzi wa dereva huyo kukimbia na ‘haki za watu’ uliwakera mashabiki, ambao walianza vurugu ndogo zilizokuwa zikitulizwa na askari polisi, ambao walikabiliwa na upinzani kutoka kwa mashabiki hao, wakiwaambia; “tuueni, tuueni, tunataka haki zetu. Rais karuhusu tuingie bure uwanjani.”
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Stars wakisaka bao la kusawazisha, lakini walikuwa ni Burundi tena, ambao iliwachukua dakika 12 kupata bao maridadi, likifungwa na mshindi wa kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu ya Vodacom, Amisi Tambwe, baada ya Dida na mabeki wake kuokoa shuti la Kavumbagu.
Bao hilo liliamsha shangwe uwanja mzima, kana kwamba limefungwa na Stars, kutokana na mashabiki wa Simba nao kushangilia bao la nyota wao huyo, huku Yanga nao wakiendeleza ushangiliaji wao kwa wageni waliouanza mapema.
Wakati wachezaji wa Stars wakitafakari kilichotokea, huku kocha Mayanga akifanya mabadiliko matatu kwa mkupuo, Burundi walijipatia bao la tatu, likiwekwa kimiani na Ndikumana Yusuf dakika ya 62 kwa shuti la mbali alilopiga akiwa katikati ya duara la kuanzishia mpira na kumtundua Dida aliyetoka langoni.
Baada ya mabao hayo, Stars walipoteana mchezoni kiasi cha ‘kuwapa kusema’ mashabiki ambao waliwazomea mwanzo mwisho, huku wakiwashangilia Burundi waliokuwa kama wako dimba la nyumbani.
Hadi filimbi ya mwisho, Stars ilitoka bila kutikisa nyavu za Burundi, huku wageni hao wakifunga mara tatu na kutibua sherehe za muungano miongoni mwa Watanzania.
Stars: Deogratius Munishi ‘Dida’, Omari Kindamba, Edward Peter, Aggrey Morris, Said Moradi, Said Juma/Himidi Mao, Simon Msuva, Frank Domayo, Ayoub Lipati/Haruna Chanongo, Mohamed Seif/Jonas Mkude na Ramadhani Singano.
Burundi: Arthur Arakaza, Kiza Fataki, Rugonumugabo Stephane, Issa Hakizimana/Nkurukiye Leoprd, Rashid Leon/ShabanHussein, Ndikumana Yusuf, Steve Nzigamasabo/Idd Jumapili, Cedric Amis, Didier Kavumbagu, Pascal Hakizimana na Amisi Tambwe.
Katika hatua nyingine, askari polisi Raphael Maganga, jana aliibiwa pikipiki namba T 454 CUP, aliyokuwa ameipaki ndani ya uwanja.

No comments: