Wednesday 16 April 2014

Yanga Kuendelea kujinoa kwaajili ya simba

KIKOSI cha Yanga kimeanza kujinoa kwa ajili ya mechi yao ya Jumamosi, ambapo waliweka kambi ya siku mbili mjini Moshi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo.
Simba na Yanga wanatarajia kukutana Jumamosi ijayo mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo ndiyo itakuwa ya kufunga msimu huu wa ligi hiyo.
Kwa mujibu wa Meneja wa Yanga, Hafidh Salehe, timu hiyo iliyokuwa Arusha katika mchezo wao na JKT Oljoro, iliamua kupiga kambi mjini Moshi ambapo jana walitarajiwa kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Panoni ya Ligi Daraja la Kwanza mjini Moshi na leo itawasili jijini Dar es Salaam.
"Jana (juzi) timu ililala Moshi ambapo Kocha Mkuu Hans Pluijm ameamua tucheze angalau mechi moja ya kirafiki kabla ya kurejea jijini Dar es Salaa kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na mechi yetu na Simba Jumapili," alisema Hafidh.
Katika mchezo wa Yanga na Oljoro mechi hiyo iliingiza sh.milioni 25 huku kila timu ikipata mgawo wa sh.milioni tano.
Naye Kocha Msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa ametamba kwamba safari hii hawatakubali kufugwa tena na watani zao Simba, hivyo ni lazima wafute uteja na kuweka heshima.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa ni Desemba 21, mwaka jana, ambapo Yanga walifungwa mabao 3-1 na mahasimu wao Simba katika mechi yao ya Nani Mtani Jembe iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
"Safari hii hatutakubali tena kufungwa kirahisi namna hiyo na Simba, tumejipanga vizuri na kikosi changu kipo fiti kwa ajili ya mechi hiyo ya kihistoria," alisema Mkwasa.
Alisema kwa kuwa wamekosa kutwaa ubingwa wa Bara, hivyo ni lazima wawape zawadi mashabiki wao kwa kuwafunga Simba katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na uliojaa upinzani mkubwa.

No comments: