Thursday 17 April 2014

Tambwe ampeleka Kaumbagu Simba

VITA imeanza. Straika tegemeo wa Simba, Mrundi Amissi Tambwe,  amewaambia mabosi wake kuwa kama wanataka aendelee kupachika mabao kwa kasi kubwa, basi wahakikishe wanamsajili haraka straika wa Yanga, Didier Kavumbagu, ili asaidiane naye.
Ukipima kwa haraka uwezo wa washambuliaji hao, utaona wazi Tambwe ni hatari katika kikosi cha Simba akiwa amefunga mabao 19, huku Kavumbagu akiwa amefunga mabao 10 lakini ametoa pasi kadha za mwisho ambazo wenzake wanafunga na kuifanya Yanga ifikishe mabao 60 katika ligi.
Baada ya kufikiria kwa kina uwezo wa Kavumbagu, Tambwe akatamka bila wasiwasi: “Nileteeni Kavumbagu muone mambo yangu zaidi.” Mkataba wa Kavumbagu na Yanga umebakiza wiki moja tu ili umalizike na kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mchezaji huyo yupo huru kuzungumza na klabu yoyote kuhusu usajili kwa sasa.
Bado uongozi wa Yanga haujazungumza kirefu na Kavumbagu juu ya mkataba mpya, lakini Mrundi mwenzake, Tambwe, alisema: “Simba kama inataka mshambuliaji wa kunisaidia, Kavumbagu anafaa kucheza nami na nina uhakika tukicheza pamoja nitafunga mabao mengi zaidi.”
Siku tatu zilizopita, Kavumbagu aliliambia Mwanaspoti kuwa, mkataba wake unaisha ndani ya wiki moja sasa, na yupo tayari kuzungumza na timu yoyote ili aweze kuichezea msimu ujao. 
Akizungumza na Mwanaspoti, Tambwe, ambaye anaongoza kwa ufungaji mabao (mabao 19) alisema kuwa kutokana na upungufu aliouona kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba, Kavumbagu ndiye anayehitajika kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chao.
Alisema anamjua vizuri mshambuliaji huyo kutokana na kucheza naye kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Burundi, hivyo wakikutana tena Simba basi kasi yake ya mabao itaongezeka mara dufu.
“Yanga ina mabao mengi ya kufunga katika ligi kuu kutokana na kuwepo viungo washambuliaji wengi wenye uwezo wa kupiga krosi na kuchezesha washambuliaji wao, vitu ambavyo Simba hakuna,” alisema.
“Kati ya viungo na washambuliaji wanaoongoza kwa kupiga pasi na krosi za mabao Yanga ni Kavumbagu, huyu ni mchezaji anayepambana katika kuhakikisha timu inapata ushindi, anatimiza majukumu yake vizuri na anajiamini ndani ya uwanja.”
Alipoulizwa kuhusu ombi hilo la Tambwe, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema: “Nguvu zetu hivi sasa tumezielekeza katika mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Yanga, ni vyema suala hilo la usajili tukalizungumzia baada ya ligi.”
Naye Mwenyekiti wa Usajili wa Yanga, Abdallah Bin Kleb alisema: “Huu siyo wakati mwafaka wa kuzungumzia usajili, ligi inaendelea ni vyema tukasubiri hadi muda mwafaka wa usajili na utakapofikia, tutaweka wazi kila kitu.”
Kabla ya kusajiliwa na Yanga, Kavumbagu alikuwa akichezea Atletico ya nyumbani kwao Burundi.

No comments: