Friday, 25 April 2014

Hali ya wasi wasi yatanda nchini Ukraine

Vifaru na wanajeshi wa Urusi karibu na mpaka wa Ukraine.
Vifaru na wanajeshi wa Urusi karibu na mpaka wa Ukraine.

Jeshi la Urusi linaendelea na harakati zake kwenye mpaka wake na Ukraine ili kujibu operesheni ziliyoanzishwa na viongozi wa Kiev dhidi ya wapiganaji wenye silaha wanaounga mkono serikali ya Urusi mashariki mwa Ukraine.

Hali iliendelea kutanda jana alhamisi, baada ya shambulio liliyotokea katika mji wa Slaviansk, ambalo lilisababisha vifo vya watu watano kutoka upande wa wapiganaji wenye silaha wanaounga mkono serikali ya Urusi, viongozi wa Ukraine wamethibitisha.

Wanajeshi wa Ukraine wakishika ulinzi katika mji wa Slaviansk, mashariki mwa Ukraine.
waziri mkuu wa Ukraine, Arseni Iatseniouk ameituhumu leo Urusi kutaka kuanzisha vita vya tatu vya dunia kwa kuunga mkono wapiganaji wenye silaha mashariki mwa Ukraine, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kujiunga pamoja dhidi ya chokochoko hizo za Urusi.
“Majaribio hayo ya jeshi la Urusi kwa kuishambulia Ukraine yatasababisha mgogoro kusambaa barani Ulaya. Urusi inataka kuanzisha vita vya tatu vya dunia wakati dunia haijasahau vita vya pili vya dunia”, amesema waziri huyo mkuu, wakati wa kikao cha baraza la mawaziri.
Arseni Iatseniouk, amesema uungwaji mkono wa Urusi kwa magaidi nchini Ukraine ni uhalifu wa kimataifa, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kujiunga pamoja dhidi ya mashambulizi ya Urusi.

Rais wa Marekani, Barack Obama akiionya Urusi
Wakati huohuo rais wa Marekani Barack Obama ameituhumu Urusi kuwa chanzo cha vurugu nchini Ukraine na kizuizi kwa makubaliano yaliyoafikiwa mjini Geneva, huku waziri wake wa mashauri ya kigeni John Kerry akiionya Urusi dhidi ya vikwazo zaidi iwapo itaendelea na msimamo wake wa kuchochea vurugu na kuendelea kuunga mkono wapiganaji mashariki mwa Ukraine.
Marekani imeionya nchi ya urusi kuhusiana na kitendo chake cha kuingilia mambo ya ndani ya nchi ya Ukraine na kwamba jumuiya ya kimataifa itachukua hatua zinazostahili kukabiliana na urusi.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema kuwa Urusi inauhadaa ulimwengu kwa kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mjini Geneva nchini Uswisi.
Kerry amesema kuwa Urusi imeshindwa kuondoa majeshi yake katika mpaka na Ukraine kama ilivyokubaliwa huko Geneva hatua ambayo ni kinyume na mikataba ya kimataifa.
Ameeleza kuwa dunia inashuhudia kile kinachoendelea na hivyo lazima Urusi ichukue hatua za kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa Geneva

No comments: