Wednesday, 16 April 2014

Tambe amtambia Pluijim

Kocha  wa Yanga, Hans van Pluijm na mshambuliaji wa Simba, Amis Tambwe kila moja amejigamba kuhakikisha klabu yake inamaliza msimu kwa kupata ushindi katika mchezo  wa mwisho baina ya timu hizo.
Kocha huyo Mholanzi ameipongeza Azam kwa kutwaa ubingwa na kusema waliweka changamoto na presha kubwa hasa katika mechi zao za mwisho ambazo wote walikuwa wakipambana bega kwa bega kuusaka ubingwa.
Pluijm alisema anaipongeza Azam kwa kutwaa ubingwa huo na kudai mechi tatu ziliwaharibia baada ya kutoka katika michuano ya kimataifa.
“Hatuwezi kulaumiana kwa sasa, tunawapongeza Azam kwa ubingwa, lakini uzembe wetu umetugharimu kwa kushindwa kutumia nafasi tuliyokuwa nayo hasa baada ya kutoka katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tulikuwa na michezo mingi mkononi kuliko wapinzani wetu, lakini tukashindwa kujipanga jambo ambalo lilitugharimu na kufanya tucheze kwa presha kubwa  mechi za mwishoni  ili kuusaka ubingwa, lakini tambua kila timu ilijipanga hivyo tunakubali matokeo,” alisema.
Pluijm alisema sasa hivi wanaangalia mechi yao ya mwisho dhidi ya Simba ili waweze kuibuka na ushindi na kujipanga kwa ajili ya msimu ujao na Kombe la Shirikisho.
“Tuko Moshi  leo (jana) tuna mechi  ya kirafiki na baada ya hapo tutarudi Dar es Salaam kuweka kambi kwa ajili ya mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Simba Jumamosi, naamini tutashinda mechi hiyo na mambo mengine yatafuata,” alisema Pluijm.
Naye mshambuliaji wa  Simba, Tambwe amekiri timu yao haikuwa vizuri msimu huu, lakini hawatakubali kamwe wafungwe na Yanga Jumamosi ili kuwafariji mashabiki wao.
Mrundi huyo Tambwe alisema hapingani na maneno ya mashabiki wengi kuwa timu yao haikuwa vizuri msimu huu na ndiyo maana imeshindwa kutwaa ubingwa wala nafasi ya pili, lakini amedai kuwa  mechi ya Jumamosi afe kipa afe beki ushindi lazima.
Simba, ambayo iko nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 37, pia inahitaji kuishinda Yanga ili iimiliki nafasi hiyo kwani ikifungwa, moja ya timu mbili za Kagera Sugar au Ruvu Shooting itaipiku iwapo itashinda  mechi ya mwisho na Simba kushuka chini.
“Muhimu ni kujipanga kwa ajili ya msimu ujao ili tufanye vizuri. Kuwafariji mashabiki wetu ni lazima tushinde mechi ya Jumamosi dhidi ya Yanga. Uwezo wa kushinda tunao hivyo kila mchezaji ajue ana jukumu la kuhakikishaa mashabiki wanaondoka na furaha waliyoikosa.”

No comments: