straika wa TP Mazembe, Mbwana Samatta akiokota mpira kwenye nyavu za timu pinzani |
NYOTA
ya straika wa Mbwana Samatta imezidi kung’aa klabuni TP Mazembe baada
ya juzi Jumatano kuifungia mabao matatu ‘Hat Trick’ timu yake na
kuisaidia kushinda mabao 4-1 dhidi ya AS Vita.
Katika pambano hilo la watani wa jadi kuwania
ubingwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lililochezwa kwenye
Uwanja wa Stade TP Mazembe huko Kamalondo, Lubumbashi, Mtanzania huyo
alionekana kuwa mwiba mkali kwa AS Vita yenye makao makuu yake Kinshasa.
Samatta aliyekuwa anaichezea Simba kabla ya
kujiunga na TP Mazembe, alifunga mabao hayo katika dakika za 51, 71 na
85 huku Rainford Kalaba akiwa wa kwanza kuifungia timu hiyo katika
dakika ya nane. Bao la AS Vita lilifungwa na Patou Ebunga dakika ya 16.
Tangu alipojiunga na TP Mazembe mwaka 2011,
Samatta amekuwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa timu hiyo kiasi cha
kujizolea mashabiki wengi katika kila pembe ya Lubumbashi na
kuipeperusha vizuri Bendera ya Tanzania.
Samatta sambamba na Mtanzania mwingine anayechezea
timu hiyo, Thomas Ulimwengu waliitwa katika kikosi cha Taifa Stars
kitakachocheza mechi ya kirafiki na Burundi kesho Jumamosi Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, lakini wameshindwa kuja kutokana na majukumu yao
katika klabu hiyo.
Keshokutwa Jumapili, Samatta anatarajiwa kuichezea tena TP Mazembe dhidi ya Don Bosco katika mwendelezo wa michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment