Emanuel Okwi akisubiria nyaraka zake kukaguliwa ili aweze kuanza safari yake ya kuelekea Uganda |
Okwi ambaye hadi anaondoka jana saa tatu usiku
alikuwa katika mgomo wa kutoichezea timu yake kutokana na madai ya fedha
kiasi cha dola 40,000 (Sh 64 milioni) ndiye alikuwa wa kwanza kufika
uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akimtangulia Kiiza.
Mara baada ya kumuona mwandishi wa Mwanaspoti huku
akipigwa picha za kutosha alionekana kushangazwa akiuliza nani ametoa
siri ya safari yake.
Akiwa katika mshangao kuhusu kuvuja kwa siri ya
safari yao ya usiku, Okwi ambaye aliletwa na gari aina ya Noah yenye
namba za usajili T367 CJC alisema kwa kifupi kwamba anaondoka akirudi
kwao Uganda kupumzisha akili yake kufuatia msimu wa Ligi Kuu Bara
kumalizika.
Hata hivyo aligoma katakata kueleza undani wa
mgomo wake ingawa Mwanaspoti lina uhakika kwamba anaidai Yanga fedha
hizo ikiwa ni mabaki ya dau lake la usajili na hajalipwa.
“Nani amewaambia naondoka saa hizi? Hebu nitajie,
Ok kifupi narudi nyumbani kupumzika ligi imekwisha hilo ndilo ninaloweza
kusema, nimechelewa jamani naomba mniache nitaachwa na ndege,” alisema
Okwi.
Na ingawa alificha kinachoendelea kati yake na
Yanga, mmoja wa rafiki zake ameliarifu Mwanaspoti kuwa mchezaji huyo
ameondoka lakini hajamalizana na uongozi wa klabu hiyo ambao umemuwekea
ngumu kummalizia fedha zilizosalia huku akidaiwa kushindwa kuonyesha
uwezo uliotarajiwa katika kipindi cha miezi sita ya usajili wake.
Dakika 20 baadaye Kiiza naye alitua uwanjani hapo
na alipoulizwa kuhusu kuondoka kwake alisema anarudi kwao lakini hajajua
siku ya kurudi.
“Foleni zimenimechelewesha jamani, narudi nyumbani
ligi imekwisha nakwenda kupumzika ingawa nitakuwa na timu ya Taifa ya
Uganda, sijui nitarudi lini kutokana na ratiba ya mechi za timu ya
taifa,” alisema Kiiza.
No comments:
Post a Comment