UKAWA wapata mpinzani
KAMATI ya Tanzania
Kwanza nje ya Bunge Maalumu la Katiba, inatarajia kufanya maandamano na
mikutano nchi nzima wakipinga kitendo cha baadhi ya watu kutumiwa na
nchi za Magharibi kwa lengo la kuigawa nchi vipande, kutawala Visiwa vya
Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Bw. Augustino Matefu, alisema lengo la ziara yao nchi nzima
ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu upotoshaji unaofanywa na Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA) juu ya mchakato wa kupata Katiba Mpya
unaoendelea nchini.
Alisema wao kama vijana wazalendo, wameamua
kuweka utaifa mbele vyama baadaye ili kulipinga jambo hilo kwa hoja,
gharama zozote kwani baadhi ya watu wanaounda umoja huo, wamefikia hatua
ya kuwatusi waasisi wa Muungano, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeib
Amaan Karume.
"Sisi Tanzania Kwanza nje ya Bunge, tunawasihi
Wazanzibari wawakatae UKAWA ambao wamewakashifu waasisi wetu wa Muungano
hivyo tuwaone kama wahaini wa Muungano na tutawapinga kwa maandamano na
mikutano yao," alisema.
Aliongeza kuwa, mikutano ya hadhara na
maandamano ambayo wataifanya, itafanyika kikanda ambapo viongozi wa
kanda husika watatoka nje na ndani ya Bunge hilo ambapo Kanda ya
Kaskazini itaongozwa na Dkt. Harrison Mwakyembe.
Kanda ya Nyanda za
Juu Kusini itaongozwa na Profesa Mark Mwandosya, Kanda ya Magharibi
(Mwigulu Nchemba), Kanda ya Kati (Saidi Nkumba) na Kanda ya Kusini
(Pandu Ameir Kificho).
Nyingine ni Kanda ya Mashariki (Nape Nnauye), Kanda ya Mwanza (Paul Makonda), Pemba (Hamad Rashid) na Unguja Juma Sadifa.
Bw.
Matefu aliongeza kuwa, vyama vingine vya siasa ambavyo vinaiunga mkono
Tanzania Kwanza kutoka upinzani ni Chama cha Kijamii (CCK), CHAUSTA,
TADEA, TADEA na CHAUMA.
Alisema Bw. Rashid ambaye ni mbunge wa CUF,
ataongoza maandamano na mikutano akisaidiwa na Bw. Renatus Muhabi ambaye
ni Naibu Katibu Mkuu wa CCK.
Kwa upande wake, Bw. Muhabi alisema
yeye haiungi mkono UKAWA ila anaungana na Tanzania Kwanza nje ya Bunge
hilo na kusisitiza kuwa, Rais alipaswa kutoa fursa kwa wananchi waweze
kupigakura ya kuwachagua wajumbe wa Bunge la Katiba badala ya kuwachagua
yeye.
"Mimi sipo upande wa UKAWA wala CCM ila ninachotaka ni
makundi haya yawe pamoja tuweze kufanya mjadala wa kupata Katiba bora na
kuangalia ni jinsi gani Bunge hili linaweza kuendelea bila kuwa na
matabaka," alisema.
No comments:
Post a Comment