Wednesday 16 April 2014

Muungano waitesa Bunge la katiba


JADALA kuhusu muundo wa Serikali mbili au tatu umezidi kuibua mvutano baina ya wajumbe walio wengi na wachache wa Bunge la Maalum la Katiba, huku wengine wakionya kuwa vitisho havitasaidia na kwamba ni bora wagawane mbao za ukumbi huo wa Bunge kuliko kuzenguana mbele ya safari.
Mbali na mvutano huo, Bunge hilo pia lilitawaliwa na vijembe na mipasho kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Zanzibar dhidi ya mjumbe mwenzao, Ismail Jussa Ladhu, kiasi cha kumlazimisha Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kuwataka waache kile alichoita mipasho iliyovuka mipaka.
Hayo yalitokea bungeni mjini Dodoma jana wakati wajumbe hao wa Bunge hilo la Katiba wakijadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba kuhusiana na Muundo wa Muungano.
Mjumbe wa Bunge hilo, Joseph Mbilinyi (Sugu) alisema wananchi wa Mbeya mjini wanaunga mkono Serikali tatu kwani ndizo zitakazoondoa kero za Muungano zilizopo sasa.
Alisema hata wajumbe wa Bunge hilo kutoka ndani ya CCM wanaunga mkono Serikali tatu, lakini wameingiwa na hofu tangu hotuba ya ufunguzi wa Bunge hilo ya Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.
Aliwataka wabunge wa Wakristo ndani ya Bunge hilo kuwa na hofu ya Mungu katika kipindi hiki cha Kwaresima na kuacha unafiki kwa kuwadanganya wananchi vinginevyo wataungua moto.
"Wabunge wa CCM tunapokutana nao nje tunazungumza nao wanataka Serikali tatu,lakini wakija hapa wanashindwa kusema kutokana na kujazwa hofu," alisema Mbilinyi na kuongeza;
"Wajumbe wa CCM wanaharibu sana badala ya kuweka mikakati imara wameanza kuzomea kimkakati." Aliongeza kuwa kuna wajumbe wameanza vitisho kwamba Serikali tatu zikipita watagawana mbao (viti).
"Acheni kutupiga mkwara bora tugawane mbao kuliko kuja kuzenguana mbele ya safari," alisema. Mbilinyi alisema anashangazwa wajumbe wanaohoji kuhusiana na idadi ya watu waliotoa maoni ya kupendekeza muundo wa Serikali tatu kudaiwa kuwa ni wachache.
"Hata wakati wa kupima malaria au Ukimwi haupimwi kwa kutolewa lita tano za damu, bali inachukuliwa damu kidogo kwenye kidole na mtu anapata majibu ngoma (UKIMWI) imekaaje," alisisitiza Mbilinyi.
Kuhusu kauli ya Rais Kikwete kuwa endapo Serikali tatu zitapita Jeshi linaweza kuchukua nchi, Mbilinyi alisema hivyo ni vitisho kwani jeshi ni la wananchi, hivyo hakuna ubaya kama mwanajeshi anayeonekana ana tija kuwa rais.
"Wanajeshi ni ndugu zetu ni kaka zetu na tunakuwa nao klabu na hakuna ubaya na hata humu tunaye Komba (Kapteni John Komba) na Rais Kikwete ni mwanajeshi amekuwa rais, hivyo asiwawekee vikwazo vya kuwa rais," alisema Mbilinyi.
Mjumbe mwingine, Hijja Hassan Hijja, alipinga vikali muundo wa Serikali mbili na kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwalipa fidia Wazanzibari kwa kile alichodai imewaibia mali zao kwa kipindi chote cha miaka 50, ndiyo maana bado wanang’ang'ania Muungano.
"Viongozi wa Zanzibar wenyewe wanasema kuwa Muungano unawaonea, lakini inashangaza kuona leo wamegeuka kwa vile wanataka kuendelea kula tonge kwa sababu kuna watu wanafaidika na masilahi ya muungano," alisema Hijja.
Alifafanua kuwa Watanganyika kama wanataka Muungano udumu basi Wazanzibari wapewe hadhi ya nchi yao. "Suluhisho pekee ni Serikali tatu, lakini wengine ni vigeugeu," alisema na kwenda mbele zaidi akisema;
"Pale mlangoni badala ya kuweka mashine za kukagua silaha waweke zile za kupima akili za watu kwa sababu wengine ni vigeugeu."
Mjumbe mwingine, Mbarouk Salim Ali, alisema Wazanzibari bado hawana mamlaka ya kujiunga na OIC, lakini wakipata mamlaka ya kuwa nchi wataweza kujiunga na taasisi hiyo kubwa ya Kiislamu duniani na kuweza kufaidika na fursa zinatolewa na OIC.
"Wazanzibari wamechoshwa na kero za Muungano wa Serikali mbili na licha ya kuundwa Kamati mbalimbali na tume, lakini hadi sasa kero zinazidi kuongezeka kila kukicha," alisema.
Kwa upande wake, Chiku Abwao, alisema muungano wa shirikisho utaondoa manung'uniko, hivyo Watanzania hawana sababu ya kuogopa vitisho vya CCM. Alisema Serikali tatu haina gharama kwani kwa sasa Serikali inapoteza asilimia 35 ya mapato.
"Tunatakiwa kuheshimu maoni ya wananchi na si kufuata maoni ya CCM," alisema Abwao. Naye Makame Mshimba, alisema inashangaza kuona viongozi wa Zanzibar wamemsaliti Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif, kwani wote walikuwa wanaunga mkono Serikali tatu.
Mjumbe mwingine, Fahmi Dovutwa, alisema Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ndiye mwenye siri ya Serikali tatu kwani chama chake ndicho chenye sera ya Serikali ya majimbo.
"Wao ndiyo wanaojua kiini cha Serikali tatu, lakini wanashindwa kusema," alisema na kuongeza kuwa wanaotetea muundo wa Serikali tatu wameshindwa kutoa hoja za msingi.
Kwa upande wake, Pamela Massay, alisema amesikitishwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kusimamia suala la muundo wa Serikali na kucha baadhi ya vifungu vya rasimu ya Katiba ambavyo pia vina umuhimu kwa wananchi wa Tanzania.
"Nasikitika kusema kuwa mapendekezo ya walio wengi wanaotaka uwajibikaji,uadilifu na uwazi viondoke katika kipengele cha tunu za taifa letu na kusema viongezeke haki na usawa viingie pamoja na amani," alisema na kuongeza:
"Sasa mimi nahoji kama tunasema haki na usawa tunataka viwe tunu ya taifa letu halafu tunasema uadilifu usiwe tunu za taifa hili sasa kama uwazi haupo na uwajibikaji, haki na usawa tutavipataje."
Kwa upande wake, Panya Ally Abdallah, alisema muundo wa Muungano uliopo ni imara na wa kipekee japokuwa kuna kero mbalimbali zilizojitokeza.
"Watu wasitusemee kuwa tunataka Serikali tatu wakati tulitoa maoni mbele ya Baraza la Wawakilishi kwamba tunataka Serikali mbili,CUF walisema wanataka Serikali ya mkataba nawashangaa wamefika hapa na kusema kuwa wanataka Serikali tatu,"alisema Abdallah.
Kwa upande wake, Ezekiel Maige, alisema idadi ya Serikali si msingi wa kutatua matatizo yaliyopo katika Muungano. "Mimi naona matatizo makubwa yapo eneo la uchumi zaidi," alisema Maige.
Aliwashukia baadhi ya wajumbe wa Zanzibar kuwa mijadala waliyokuwa wakiitoa bungeni hapo walikuwa wakitumia lugha ambazo si za staha.
"Kusema ukweli lugha ambazo zimekuwa zikitoka kwa upande wa pili wa Muungano zina ukakasi na chokochoko na naamini pande zote mbili za Muungano zimenufaika sana na muungano na kwa kweli Zanzibar imenufaika zaidi kiuchumi kutokana na muungano huo, lakini Bara ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yenye uchumi mkubwa imekuwa ikishiriki katika miradi ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar," alisema.
Kwa upande wake Joseph Selasini, alisema kinachotakiwa sasa ni Katiba ya wananchi na si ya CCM au wapinzani. Alisema kinachofanyika sasa watu wanasema Bunge ni sawa na komedi ambayo inazidi hata ya akina Masanja.
Alisema wiki hii ni ya toba hivyo wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wametakiwa kumwogopa Mungu.

No comments: