Mkazi wa Buguruni jijini hapa, Deus Johakim Magosa (45)
ambaye ni shahidi wa nane upande wa Jamhuri katika kesi namba 303 ya
mwaka 2016 ya kumjeruhi, kumtoboa macho na kumfanyia unyang’anyi wa
kutumia silaha, Saidi Mrisho inayomkabili Salum Njwete ‘Scorpion’ katika
Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini, leo alinusurika kutupwa lupango
baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga kumtuhumu kutoa
ushahidi wa uongo.
Wakili Katuga alimtuhumu shahidi huyo kutokana na kutoa
majibu tofauti wakati akimuongoza kutoa ushahidi wake na maelezo
aliyoyatoa awali Kituo cha Polisi cha Buguruni.
Awali shahidi huyo alisema mahakamani hapo kuwa hakuwahi
kusikia popote kuwa Scorpion amehusishwa katika tukio la kumshambulia
Said, lakini baadaye alipobanwa alisema ni kweli alisikia tetesi hizo
kuwa mtuhumiwa huyo ndiye aliyefanya tukio hilo. Pamoja na mambo mengine
aliyomhoji na kumbaini kuwa anatoa ushahidi wa uongo wakili Katuga
alipomgeukia hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Flora
Haule na kumwambia shahidi anazidi kuidanganya mahakama hiyo na kuitaka
mahakama hiyo imchukulie hatua kwa mujibu wa kifungu cha 164 cha
ushahidi hapa nchini (Tanzania Evidence Act).
Shahidi huyo alionekana kuwa katika wakati mgumu baada ya
wakili huyo kuwaita askari polisi na kuwataka wakae tayari kumchukua
shahidi huyo.
Hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda hakimu Flora
aliahirisha kesi hiyo mpaka Aprili 18 mwaka huu na kumuacha shahidi huyo
aondoke na kumtaka kufika tena mahakamani hapo tarehe iliyopangwa bila
kukosa ambapo Scorpion naye alirudishwa mahabusu mpaka tarehe hiyo.
Mwandishi wetu alizungumza na mmoja wa wanasheria
mahakamani hapo kuhusu ushahidi wa uongo ambapo, mwanasheria huyo
alisema unapobainika kutoa ushahidi wa uongo ukiwa ndani ya kiapo
unaweza kufungwa jela kati ya miezi sita mpaka mwaka mmoja.