Wednesday, 6 September 2017

Mwanafunzi awekewa sh. bilioni 2.2 na bodi ya mikopo kimakosa

Eastern Cape, Afrika Kusini. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Walter Sisulu alilala masikini na kuamka tajiri baada ya kukuta akaunti yake ikiwa na Dola 1 milioni za Marekani sawa na Sh2.2 bilioni kutoka katika bodi ya mikopo ya wanafunzi.

Alijiona mwenye bahati na kuanza kuzitumbua, asijue kumbe alikuwa akichochea kugundulika haraka kwa kuwa ndani ya wiki mbili kitumbua chake kiliingia mchanga.

Hadi kugundulika kwa makosa hayo, mwanafunzi huyo aliyestahili kuwekewa Dola 100 za Marekani kwa ajili ya ununuzi wa vitabu na chakula alikuwa ameshatumia Dola 60,000.

Kilichomponza akagundulika haraka ni matumizi yake yaliyowafanya wenzake kuwataarifu viongozi ambao walipochunguza waligundua kosa la kuongezwa sifuri nne mbele ya Dola 100 alizostahili kupata.

Msemaji wa chuo hicho, Yonela Tukwayo amesema akaunti ya mwanafunzi huyo imesitishwa na kiasi cha fedha kilichobaki kimeondolewa.

Amesema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mwanafunzi huyo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Tukwayo amesema mwanafunzi huyo alipaswa kutoa taarifa baada ya kugundua kiasi kikubwa cha fedha kuwemo katika akaunti yake lakini alizitumbua na ndani ya wiki tatu aliteketeza Dola 60,000 ambazo ni wastani wa Sh120 milioni.

Chanzo: Mwananchi

No comments: