Jeshi la Zimbabwe limekanusha madai kwamba mapinduzi ya
kijeshi yamefanyika kuiondoa serekali, na kudai kwamba rais Robert Mugabe na
familia yake wapo salama.Katika taarifa iliyotolewa na jeshi kupitia televisheni ya
taifa, imeelezwa kwamba jeshi linalenga wahalifu wanaosababisha shida za
kijamii na kiuchumi na kuwafikisha mbele ya sheria.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya mashuhuda kusema wamesikia
takriban milipuko mitatu pamoja na milio ya risasi katika mji mkuu wa Harare,
usiku wa kuamkia Jumatano.
Inaelezwa pia na mashuhuda magari ya jeshi na wanajeshi
walikuwa katika mitaa mapema Jumatano hii saa kadhaa baada ya wanajeshi
kushikilia chombo cha utangazaji cha serekali cha ZBC.
Wakazi wamesema kwamba tofauti na kuwepo kwa taarifa ya
habari ya saa tano usiku, ZBC ilicheza muziki bila taarifa yoyote.
Msemaji wa ubalozi wa Marekani mjini Harare, alinukuliwa
akisema kwamba mitaa ya Harare ilionekana kuwa tulivu usiku wa kuamkia leo, na
hakuthibitisha kuona magari ya kijeshi. Msemaji huyo pia amesema hana taarifa
ya milipuko yoyote kutokea kama ilivyoelezwa na baadhi ya wakazi wa Harare.
Hapo jana Jumanne, chama tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF
kilimshutumu mkuu wa majeshi kwa vitendo vya uhaini baada ya kutishia kuingilia
kati mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.
Taarifa ya ZANU-PF ilitolewa katikati ya wasiwasi uliotanda
kwamba jeshi limechukuwa hatua ya kuchukuwa madaraka na kumuondoa rais wa muda
mrefu wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
Mashuhuda waliripoti kuona vifaru na maafisa wa jeshi wakiwa
mitaani na kelekea nje ya mji licha ya Harare kuwa tulivu. Balozi za nchi
mbalimbali nchini humo hazikutoa tahadhari kwa raia wake walioko nchini
Zimbabwe kwa sasa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia
alinukuliwa akisema kwamba wanataarifa hizo na wanaendelea kufanya uangalizi.
Hali ya wasiwasi ya sasa ilizuka juma lililopita wakati rais
Robert Mugabe alipomfukuza naibu wake Emmerson Mnangagwa na kumshutumu kwa
kutomti na kupanga kutwaa madaraka.
No comments:
Post a Comment