Tuesday, 21 October 2014

Kutupwa segerea kwa halima mdee kwa zua Makubwa

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ameelezea mambo matano aliyokutana nayo katika gereza la Segerea Dar es Salaam alipokaa mahabusu kwa saa 24 kwa tuhuma za kuongoza maandamano yasiyokuwa na kibali Oktoba 4 mwaka huu jijini humo.
Akizungumza jana jijini hapa alisema,akiwa humo alikutana na wasichana wadogo ambao walimweleza wamefika hapo kutokana na kudai haki zao, lakini kwa kuwa wamekosa watetezi wamejikuta wakisota gerezani
Aliongeza: “Mpango wa kupunguza wafungwa wenye vifungo vifupi vifupi unaonekana kukwama, gereza haliendani na wingi wa watu waliomo.
“Kuna wasichana wadogo wengi sana, wanaochukuliwa mikoani kuja kufanya kazi za ndani, wakifika huku wanafanya kazi hizo lakini mwajili wake anaposhindwa kuwalipa na binti huyu akianza kudai haki yake mwajiri anambabikia kesi.
Mdee ambaye pia ni Katibu wa Kanda ya Mashariki wa Chadema alisema kesi za mauaji na wizi zimekuwa zikichelewa, jambo linalowakatisha tamaa washitakiwa kutokana na kukaa muda mrefu.
“Unakuta mtu kweli anajulikana kaua au mwingine kaiba, lakini upelelezi wake utachukua miaka mingi ni rai yangu kwamba umefika wakati uwepo utaratibu wa kupunguza mrundikano’ alisema .
Mdee alisema licha ya gereza kuwa sehemu ya kurekebisha tabia za watu, lakini hali kama hiyo imegeuka kuwa eneo la kufundishia mbinu chafu za kibiashara..
Wasichana wadogo wanafundishwa biashara chafu na waliowazidi umri,wakitoka wanakuwa wamoja na kuanzisha makundi ya uchangudoa” alisema.
Mbunge huyo alisema Serikali ina kazi kubwa ya kukomesha vitendo hivyo na kwamba alipokuwa mahabusu alijifunza mambo mengi.
“Nilipofikishwa kule ilikuwa imeshafika saa 11 jioni, nililetewa ugali ambao haukuwa umeiva, mchicha wenyewe umekomaa na kama ni dagaa basi hawaoshwi wakitolewa katika gunia tu, wanapikwa hivyo hivyo na michanga. Uji ndiyo usiseme sasa fedha za bajeti huwa zinakwenda wapi kama hali ndiyo hiyo,” alihoji Mdee
Mdee alisema licha ya gereza kuwa sehemu ya kurekebisha tabia za watu, lakini kwa hali kama hiyo imegeuka kuwa eneo la kufundishia mbinu chafu za kibiashara.
“Hawa dada zetu wadogo wanaowekwa huko, wanakutana na mi dada iliyokubuhu mitaani kwa vitendo vya kuendesha biashara ya ngono, ikikutana na hao inawafundisha hao wasichana mbinu chafu.”

“Unakuta inawaeleza kwamba unajua kule mtaani kuna biashara ambayo ina lipa kuliko hiyo ya kazi za ndani, hivyo mkitoka tutakwenda kuwafundisha ni kweli wakitoka wanakuwa timu moja wanaanzisha makundi ya machangudoa,” alisema Mdee
Aliongeza: “Serikali ina kazi kubwa ambayo inatakiwa kuifanya kukomesha vitendo hivi, lakini nimefurahi nimewekwa ndani kwani nimeweza kujifunza kitu nikiwa humo na ninatamani siku moja nirudi tena ingawa walinitoa mapema ili nisijue siri za humo zaidi.”

Man u yabanwa mbavu tena


Ligi kuu ya England imeendelea jana usiku ambapo Manchester United ilijikuta ikibanwa mbavu na kushindwa kufurukuta ugenini kwa Westbromwich Albion na kutoka sare ya mabao 2-2 licha kwamba ilitawala mchezo huo.

Mchezo huo wa pekee kwa ratiba ya ligi hiyo ulishuhudiwa Man United ikishindwa kupata walau ushindi wake wa kwanza nje ya uwanja wake wa nyumbani tangu timu hiyo iwe chini ya kocha Louis Van Gaal.
Ni bao la Daley Blind katika dakika za mwisho za mchezo ambalo limeiokoa Manchester United kuzama katika mpambano huo. Awali Stephane Sessegnon wa Westbrom aliitungua United kwa bao la mapema kabla ya Marouane Fellaini aliyeingia kipindi cha pili kusawazisha muda mfupi tu baada ya kuingia uwanjani.
Mshambuliaji kijana Saido Berahino aliipatia Westbrom goli la pili ambalo lilidumu hadi pale Blind aliposawazisha na kuinusuru United na kichapo katika mtanange huo uliochezeshwa na mwamuzi Mike Dean.

kocha mpya wa makipa, Mserbia Zdravkomr Djekic. ampiga chini Idd panzi

UONGOZI wa Klabu ya Simba chini Rais wake Evance Aveva, umempa mkataba wa miezi miwili kocha mpya wa makipa, Mserbia Zdravkomr Djekic.
Uteuzi wa Mserbia huyo umekuja siku chache tu tangu aliyekuwa Kocha wa makipa, Idd Pazi kuachwa katika safari ya timu hiyo nchini Afrika Kusini.
Japo hadi sasa uongozi wa Klabu hiyo haujatamka rasmi kumtema Pazi kwa hoja kuwa bado yupo katika nafasi hiyo, uteuzi wa Mserbia huyo kunathibitisha hilo.
Katibu Mkuu wa Simba, Stephen Ally, alisema jana kuwa hana taarifa ya Pazi kuachwa, hivyo ataendelea kuwepo katika benchi la ufundi.
Alisema ndio maana wamempa Mserbia huyo mkataba wa muda mfupi wa kutekeleza programu fupi ya timu yao huku Pazi akiendelea kuwa kocha wa makipa wa Simba kama kawaida.
Katika hatua nyingine, Ally alisema timu imeanza mazoezi jana jioni katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kujipanga zaidi kwa mechi dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya.
Alisema kesho timu inatarajia kwenda jijini Mbeya kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi katika uwanja wa Sokoine jijini humo, ikiwa ni mara ya kwanza Simba kucheza nje ya Uwanja wa Taifa katika msimu huu.

Mrema kawa mkali kama simba awavua uanachama wa TLP baadhi ya wanachama mamluki

MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amekunjua upya makucha yake yaliyowahi kurarua viongozi wenzake akiwa katika NCCR-Mageuzi na TLP, na sasa amefukuza hadharani madiwani wawili wa chama chake waliounga mkono nia ya Mbunge wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye ametangaza kugombea ubunge wa Vunjo.
Mrema amewavua uanachama wa TLP, Meja Mstaafu Jesse Makundi, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya Mrema; na Yorolanda Lyimo, Diwani wa Kilema Kaskazini.
Jimbo hilo linawakilishwa na Mrema tangu 2010, na amesema mara kadhaa kwamba hataki kusikia mtu akitaka ubunge katika jimbo lake. Tayari amemlalamikia Mbatia kwa rais na katika Bunge Maalumu la Katiba.
Kilichowaponza Makundi na Lyimo ni kushiriki harambee iliyoongozwa na Mbatia ya ujenzi wa maabara na mabweni katika shule za Sekondari za Pakula, Kiluani na Mwika, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika harambee hiyo, Makundi alisema anatambua uwezo wa Mbatia na kwamba, kwa sababu hiyo, anamuunga mkono katika azima yake ya kuwa mbunge mwakani.
Alisema kwa kuwa alipokea tochi ya kumulikia wana Vunjo kutoka kwa Mbatia, ameona ni busara kuirudisha kwa yule aliyemkabidhi tochi hiyo.
“Leo nimefikia uamuzi ambao naamini ndio hitaji la wana Vunjo, kwa kuwa Jimbo hili nililipokea kutoka kwa Mbatia na kwa kuwa yeye ndiye aliyenikabidhi hii Tochi, natamka hadharani kuwa Mbatia ndiye chaguo langu, yeye ndiye atakayemulika wana Vunjo,” alisema Makundi.
Yorolanda naye alidai kuwa uamuzi wa kumuunga mkono Mbatia ni wa Mungu.
“Tunamuomba Mungu amuinue aweze kuwa Mbunge wetu. Mimi ni Diwani wa TLP, nina Mbunge wangu, namuheshimu sana (Mrema), lakini namuomba Mungu amteue Mbatia chaguo letu Wana Vunjo. Nafahamu wapo watakaonukuu maneno yangu lakini kama mbaya acha iwe mbaya,” alisema.
Mrema amekerwa na kauli hizo, akawavua uanachama akidai wameonyesha utovu wa nidhamu na wamekiuka katiba ya chama chao kuunga mkono mtia nia wa ubunge wa chama kingine, katika jimbo lake ambalo naye ameshatangaza kuwania nafasi hiyo tena mwakani.
Alikuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Mwanjeni, Kata ya Mwika Kusini.
Hata hivyo, Makundi amesema uamuzi wa Mrema ni batili, kwani mwenyekiti wake huyo hana mamlaka hayo.
Mrema amekuwa analalamikia hatua ya Mbatia kutaka ubunge wa Vunjo, akisema kinachomtia kiburi ni ubunge wa kuteuliwa aliopewa na Rais Jakaya Kikwete.
Analaumu pia vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambavyo vimetangaza kuweka mgombea mmoja mmoja kila jimbo kwa ushirikiano.
Hata hivyo, UKAWA haijatangaza mgombea wa Vunjo. Licha ya Mbatia, yupo mtia nia mwingine kutoka CHADEMA, John Mrema, ambaye naye ameshatangaza kugombea ubunge huo, akisubiri uamuzi wa mwisho wa UKAWA.
Lakini Mrema amekuwa anamshambulia Mbatia kwa kuwa ndiye amekuwa anafanya mikutano ya mara kwa mara.
Akizungumza katika mahojiano maalum na na waandishi wa habari hivi karibuni, Mbatia, malalamiko ya Mrema hayana msingi wowote, na kwamba hatajibizana naye.
“Siko tayari kujibizana na mtu. Kuna kazi kubwa mbele yetu. Tuelekeze nguvu zetu kuwatumikia Wana Vunjo. Mkutano wa Septemba ndio unaomtesa. Nyinyi ni mashahidi. Tangu Septemba 6, sijafanya mkutano wowote. Kulalamika kwake ni sawa na kulalamikia kivuli. Kivuli chake kinamuhukumu. Mimi siko tayari kumjibu,” alisema Mbatia.
Kati ya 1995 na 2005, Mrema akiwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na baadaye TLP, aliwahi kuthubutu kutimua viongozi wenzake kwa mtindo huo.
Miongoni mwao ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wake, Harold Jaffu na Thomas Ngawaiya, ambao aliwaitia Kamati ya Utendaji na kuwashitaki kwa kuwashitukiza, baada ya kugundua wamepunguza utii wao kwake.
Kabla ya hapo, alijaribu kufukuza Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi, akiishitaki kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu kwamba kamati hiyo ilikuwa haimsaidii kufanya kazi. Kati ya wajumbe 22 wa kamati hiyo, aliungwa mkono na wajumbe saba tu.
Kamati Kuu, ikiongozwa na Mabere Marando, ilikataa kufukuzwa na Mrema, na baadhi yao (Ndimara Tegambwage na Profesa Mwesiga Baregu) wakamshauri ajiuluzu akagoma; kukazuka mtafaruku mkubwa ulioenea kwa njia na sura mbalimbali, na hatimaye ukasambaratisha chama hicho.
Aliwahi pia kuthubutu kuwafukuza Balozi Paul Ndobho na Steven Wassira aliokuwa nao NCCR-Mageuzi, akiwatuhumu kwamba walikuwa wanafanya njama za kumwengua asigombee urais, walipokuwa wanamshawishi aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba (sasa hayati) ajiunge na NCCR-Mageuzi.
Baadaye Mrema alikimbilia TLP mwaka 1999, na kwa staili hii, alifukuza viongozi wote wa Mkoa wa Kagera wa chama chake, siku alipokwenda kumzika aliyekuwa mbunge pekee wa chama hicho wakati huo, Phares Kabuye, wa Biharamulo Magharibi.
Sababu ya kuwafukuza ni kwamba waliunga mkono hoja ya upinzani kuweka mgombea mmoja wa CHADEMA dhidi ya CCM katika uchaguzi mdogo.
Wajuzi wa siasa za Vunjo ndani ya TLP wanasema Makundi ndiye alikuwa kisiki muhimu katika ngome ya kisiasa ya Mrema jimboni; na kwamba kwa kuthubutu kumvua uanachama ni sawa na Mrema kuhatarisha ubunge wake, mithili ya mtu anayekata tawi alilokalia.

Monday, 20 October 2014

T.I apangawisha serengeti Fiesta 2014 Dar


TAMASHA la Serengeti Fiesta 2014, limefungwa rasmi juzi usiku katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam huku likisindizwa na burudani nzito kutoka kwa wasanii mbalimbali wa ndani na nje nchi wakiongozwa T.I kutoka Marekani.
 Shoo ya mwisho ya tamasha la Serengeti Fiesta ambalo limedhaminiwa na kinywaji cha Serengeti Premium Lager, lilivutia maelfu ya mashabiki waliofika kushuhudia nyota wa muziki kama T.I, Davido, Naseeb Abdul 'Diamond Platinum', Alikiba, Mwana FA, Stamina, Weusi na TMK wote wakitoa shoo ya nguvu.
 Katika viwanja hivyo vyaLeaders ilikuwa ni gumzo na sehemu ya pekee kwa mashabiki waliofika kushuhudia shoo ya aina yake kutoka kwa wasanii wa kimataifa.
 Waliokuwa wa kwanza kufungua shoo hiyo jukwaani walikuwa washindi wa Super Nyota wa msimu uliopita, ambao walipagawisha vilivyo mashabiki.
Wasanii wa Tanzania walistahili pongezi kwa kufanya shoo nzuri. Wasanii hao ni Mo Music, Y-Tony, Makomando, Recho, Vanessa Mdee, Barnaba, Linah, Shaa, TMK Wanaume Family, Tip Top Connection, Ommy Dimpoz na Ya Moto Band.
 Hata hivyo umati uliofurika viwanjani hapo ulipagawa zaidi, baada ya wasanii nyota kama Micharazo kupanda jukwaani na nyimbo kama Baadaye na Kimya.
 Stamina alishangiliwa zaidi baada ya kudhihirisha kipaji chake kwamba yeye kweli ni msanii bora wa miondoko ya muziki laini nchini. Wasanii wengine waliopagawisha vilivyo ni pamoja na Mwana FA, Young Killa, Weusi, Ney wa Mitego kabla ya Ali Kiba kutangaza kwa mashabiki kwamba mfalme arudi tena jukwaani. Kiba alishangiliwa na mashabiki waliokuwa wakimfuatilizia wakati akiimba wimbo wake wa Mwana Dar es Salaam.
 Kabla ya T.I kupanda jukwaani, Diamond na Davido waliwapagawisha vilivyo mashabiki na wimbo waliouimba kwa kushirikiana wa My number one remix.
 Muda uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki ni wakati msanii bora duniani T.I alipopanda jukwaani na kusababisha mashabiki kupiga makelele alipoanza kupiga shoo.
 T.I alishangaza mashabiki vilivyo wakati alipotumbuiza nyimbo kama Whatever you like, What you know, I’m never scared, Big shit poppin, Swagga like us, No mediocre na Live your Life ambazo ziliwafanya mashabiki wapige mayowe muda wote alipokuwa akitumbuiza.
 T.I aliwashukuru mashabiki na akawarudisha kidogo Afrika wakati alipoimba wimbo wa Ejeajo ambao alishirikiana na P-Square, aliendelea kuwashukuru mashabiki wa muziki wake nchini na kusema anatamani angekuja nchini kabla ya jana.
 Akizungumza na waandishi wa habari Meneja Chapa wa kinywaji cha Serengeti Fiesta, Rugambo Rodney alimpongeza T.I kwa kuonesha shoo nzuri.
 Rugambo alisema; ”Mwaka huu ziara ya Serengeti Fiesta ilikuwa na mafanikio makubwa na kwamba imeweka historia baada ya kujivunjia rekodi zake katika matamasha yaliyopita ya Serengeti fiesta nchini Tanzania.
 "Nina furaha na kwa niaba ya wenzangu, napenda kumshukuru kila mdau aliyefanikisha kufanyika kwa tamasha hili…mashabiki, wasanii, vyombo vya habari, waandaaji, hoteli na mawakala wote."

Manyika JR aibuka kuwa mchezaji bora wa wiki kwa mujibu wa GOAL.COM

Goal Player of the week: Manyika PeterKipa huyo licha ya udogo wake wa umri kwa kucheza pambano kubwa kama hilo alionyesha kutokuwa na wasiwasi na aliwakatisha tamaa mashabiki wa Yanga kwa kudaka krosi zote
KIPA chipukizi wa Simba Manyika Peter ,ameibuka kuwa mchezaji bora  wa wiki baada ya kuonesha kiwango kizuri katika mechi iliyowakutanisha wapinzani wa jadi Simba na Yanga iliyochezwa Jumamosi kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam.
Manyika ameingia kwenye historia ya kuwahi kucheza mechi ngumu ya watani wa jadi akiwa ni mchezaji mwenye umri mdogo zaidi na kufanya vizuri kwa kumaliza dakika zote 90 bila kufungwa na washambuliaji wa Yanga Geilson Santos JAJA,Hamisi Kiiza na Andrey Coutinho.
Kipa huyo licha ya udogo wake wa umri kwa kucheza pambano kubwa kama hilo alionyesha kutokuwa na wasiwasi na aliwakatisha tamaa mashabiki wa Yanga kwa kudaka krosi zote pamoja na kona zilizokuwa zinaelekezwa kwenye lango lake.
Katika muda wote wa dakika 90 Manyika Peter,alionekana kutulia na kuwapanga vyema mabeki wake nahodha Joseph Owino na Hassani Isihaka na kupangua kwa umahiri mkubwa mashuti ambayo yalikuwa yakielekezwa langoni mwake.
Pambano hilo ndilo lililokuwa la kwanza kwa kipa chaguo la tatu kuidakia Simba tangu aliposajiliwa msimu huu na hiyo ilitokana baada ya makipa Ivo Mapunda na Hussien Sharifu kuumia siku chache kabla ya mpambano huo wa watani wa jadi.

Polisi Kimara wadaiwa kuuza ekidhibiti

Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius WamburaKITUO cha Polisi Kimara Mwisho Jumamosi kilifungwa baada ya askari wa kituo hicho kuwekwa mahabusu kwa madai ya kuuza kidhibiti cha mirungi waliyoikamata.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kilichoomba kuhifadhiwa jina kwa usalama wake, askari wa kituo hicho waliwekwa mahabusu mwishoni mwa wiki katika Kituo cha Mbezi Luis jijini Dar es Salaam, baada yakwenda kinyume na maadili ya kazi na kusababisha kifungwe Jumamosi na kufunguliwa jana majira ya saa tatu asubuhi.
Chanzo hicho, kilisema askari hao walimkamata mtuhumiwa aliyekuwa na mzigo wa mirungi, ambaye inadaiwa walimlazimisha awape sh 200,000 ambazo alikubali.
Hata hivyo, waliendelea kudai kiasi nyingine kwa madai kuwa sh 200,000 alizotoa awali zilikuwa ni kwa ajili ya OCD, na kwamba na wao wanataka za kwao ili mambo yaishe.
Mmiliki wa mirungi hiyo, aliwaomba wampe nafasi ili aende nyumbani akachukuwe fedha kwa sababu kipindi hicho hakuwa nazo, ambako walimruhusu.
Aliporudi hakuwakuta, hivyo kuamua kuwapigia simu, lakini wakawa wanamsumbua kwa kila maeneo waliyokuwa wakimueleza wako alipofika hakuwakuta.
Baada ya kuona usumbufu huo, aliamua kwenda kituo cha Mbezi kutoa taarifa, na askari hao kuitwa na walipoulizwa mzigo walioukamata uliko, walikiri mbele ya OCD kuwa wameuza, kitendo kilichosababisha watiwe rumande.
Mmoja wa polisi wa kituo hicho cha Mbezi ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa madai kuwa si msemaji, alisema hayo ni majungu kwani hakuna tukio hilo.
“Huyo muongo, mmemhoji vizuri…hata kama kilifungwa kitakuwa kimefungwa kwa sababu nyingine na hatuwezi kumueleza kila mtu.
“Wakihitaji kujua kimefungwa kwa sababu gani waje huku tutawaambia, watu kama hao muwe na tahadhari nao, namba zetu zipo kwanini wasitupigie baadala yake wanakuja huko, ina maana wamekuja kutuchomea,” alisema polisi huyo.
Aliongeza kuwa kituo cha Kimara kinafanya kazi saa 12 na sio 24 kama walivyozoea wananchi, ingawa baadhi ya siku kinatoa huduma saa 24 kwa sababu panalazwa mahabusu.
Alipotafutwa Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita muda mrefu bila ya kupokelewa.